WACHUNGAJI MATAJIRI BONGO HAWA HAPA

Nabii George David ‘Geordavie’

WATUMishi wa Mungu wakiwemo maaskofu, manabii, wachungaji na walimu wa neno la Mungu wapo vizuri na lile neno wanalolihubiri kwamba, kwa Mungu kuna raha. Kwa Mungu kuna maisha mazuri na mtu akiyataka ampokee Mungu awe Bwana na mwokozi wa maisha yake ndipo atafaidi nchi ya maziwa na asali!  

 

Yapo madai kwamba, baada ya kujikusanyia waumini wengi, baadhi ya watumishi wa Mungu wamekuwa wakiwakamua sadaka kisha wao kuishi kama wapo peponi huku waumini wao wakitaabika kwa maisha magumu. Uchunguzi wa Amani umebaini kwamba baadhi ya watumishi hao wa Mungu wanatisha kwa utajiri Bongo kama ifuatavyo;

GEORDAVIE

Askofu Mkuu au Nabii George David ‘Geordavie’ wa Kanisa la Ngurumo ya Upako la jijini Arusha, yeye anadaiwa kuwa na utajiri wa kutisha akimiliki majumba ya kifahari ya ghorofa ikiwemo analoishi na familia yake lililopo Njiro jijini Arusha.

 

Eneo hilo analoishi lenye majumba yake limepewa jina la Mji wa Daudi kutokana na kujengwa kifahari. Mbali na mahekalu ya kifahari, pia Geordavie anayerusha vipindi vyake kupitia Televisheni ya Channel Ten, anamiliki chopa (helkopta) binafsi anayoitumia kwenye shughuli zake za kuhubiri neno la Mungu ndani na nje ya nchi.

 

Pia Geordavie anayemiliki kituo cha Redio cha Ngurumo ya Upako FM cha jijini Arusha, anasifika kwa kutembea na ulinzi mkubwa na msafara wa magari ya kifahari kama Rais wa nchi yakiwemo Toyota Land Cruiser V8 Super Charger, Range Rover Sport, Land Rover Discovery na mengineyo.

JOSEPHAT GWAJIMA

Uchunguzi umebaini kwamba mchungaji mwingine anayetisha kwa utajiri ni Askofu Josephat Gwajima wa Kanisa la Ufufuo na Uzima lenye maskani yake Ubungo-Maji jijini Dar. Gwajima hakamatiki kama ilivyo kwa Geordavie kwani anatajwa kuwa na utajiri mkubwa akimiliki mjengo wenye ghorofa nne maeneo ya Salasala jijini Dar. Mchungaji huyo naye kama Geordavie anamiliki chopa kwa ajili ya kueneza Injili huku akiwa amepanga kuingiza ndege yake binafsi nchini.

 

Gwajima pia anamiliki magari ya kifahari kama Hummer H2, achilia mbali magari ya kawaida na mabasi yanayotumika kubeba waumini wake na ana mpango wa kujenga kanisa kubwa nchini Tanzania ambalo litakuwa kubwa kuliko yote Afrika.

JOSEPHAT MWINGIRA

Nabii Josephat Mwingira wa Kanisa la Efatha Ministry lililopo Mwenge jijini Dar, naye anatajwa katika orodha hii.  Nabii Mwingira anatajwa kumiliki jumba la ghorofa moja maeneo Mikocheni B jijini Dar.

Pia Mwingira anatajwa kuwa mmiliki wa iliyokuwa Benki ya Efatha ambayo mwaka huu ilisitishiwa usajili na Serikali iliyopo Mwenge jijini Dar. Anatajwa kuwa miongoni mwa watumishi wa Mungu mabilionea akimiliki baadhi ya viwanja na mashamba mkoani Pwani.    

LUSEKELO ANTHONY ‘MZEE WA UPAKO’

Mchungaji Lusekelo Anthony almaarufu Mzee wa Upako, kanisa lake la Maombezi (GRC) lipo Ubungo–Kibangu jijini Dar. Kama Mwingira, naye anamiliki mjengo wa ghorofa moja uliopo Kawe jijini Dar anapoishi na familia yake.

Mzee wa Upako anatajwa kuwa miongoni mwa watumishi wa Mungu walio vizuri kimaisha, akibadilisha magari ya kifahari kama Range Rover Sport, Land Rover Discovery, Toyota Land Cruiser V8 na mengine makali yakiwa ni tofauti na mabasi yake mengi yanayotumika kubeba waumini wake kwa ajili ya ibada. Mzee wa Upako aliwahi kula kiapo kwa mwandishi wa makala haya akisema: “Kwenye maisha yangu siamini katika umaskini kwani umaskini siyo sifa nzuri.”

DK GETRUDE RWAKATARE

Mchungaji Kiongozi, Dk Getrude Rwakatare ni mmiliki wa Kanisa la Assemblies of God Mikocheni B jijini Dar.

Mama Rwakatare ni miongoni mwa watumishi wa Mungu aliyefanikiwa kujenga nyumba mbili za kisasa, moja ipo Mikocheni B ikiwa na ghorofa moja na nyingine ipo Mbezi-Beach, Dar yenye ghorofa moja. Mbali na kumiliki majumba hayo ya kifahari, pia anamiliki kituo cha Redio cha Praise Power huku akiendeshwa kwenye magari ya kifahari kama Toyota Land Cruiser V8.

ZACHARY KAKOBE

Askofu Zachary Kakobe anatajwa kumiliki nyumba ya kawaida mno iliyopo Mtaa wa Mpakani B, Kijitonyama jijini Dar. Nyumba yake hiyo haina ghorofa, lakini inadaiwa kuwa ni mmoja wa wachungaji wenye mkwanja mrefu ambapo mapema mwaka huu Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) ilimpekua na kueleza kuwa ilimkuta na kiasi kikubwa cha fedha alichokuwa amehifadhi kanisani badala ya benki.

NICOLAUS SUGUYE

Nabii Nicolaus Suguye wa Kanisa la Huduma ya The Word of Reconciliation Ministries (WRM) la Kivule Matembele ya Pili jijini Dar naye anadaiwa kumiliki magari na majumba ya kifahari. Mbali na majumba na magari, pia Nabii Suguye anamiliki kituo cha Televisheni cha WRM TV huku akiwa njiani kuingiza ndege yake binafsi nchini.

ELIUDI ISANGYA

Huyu ni Askofu Mkuu wa Kanisa la International Evangelism lililopo Sakila wilayani Arumeru jijini Arusha. Mchungaji Isangya anatajwa kumiliki kanisa hilo kubwa, majumba, magari na ndege binafsi. Kuna taarifa kuwa alitaka kujenga uwanja wake wa ndege eneo la Sakila, lakini alinyimwa vibali.

 

WENGINE

Wengine waliotajwa kwenye listi hiyo bila kuelezwa utajiri wao ni pamoja na Nabii wa Kanisa la The Revelation lililopo Buza-Kipera jijini Dar, Yaspi Bendera na Nabii Flora Peter wa Kanisa la Yesu Kristo la Huduma ya Maombezi lililopo Salasala jijini Dar.

 

Wengine ni Nabii na Mtume Boniface Mwamposa (Buldozer) wa Kanisa la Inuka uangaze, Nabii Paul Bendera wa Kanisa la Ufunuo na Askofu wa Kanisa la Wapo Mission International, Sylvester Gamanywa ambaye pia ndiye mmiliki wa Wapo Redio. Wamo pia Mchungaji Bruno Mwakibolwa wa Kanisa la EAGT Mito ya Baraka, Kariakoo jijini Dar na Mchungaji Florian Katunzi wa Kanisa la EAGT City Centre lililopo kwenye Viwanja vya Sabasaba jijini Dar.

BREAKING: Mwinyi Alazwa Rais Magufuli Amuombea Dua

Toa comment