The House of Favourite Newspapers

Wadada wa Mjini…Eti bora Kuwa ‘Single Mother’ Halafu?

0

SINGLE mother ni kamsemo ambapo kadiri siku zinavyozidi kwenda kanazidi kushika hatamu. Si msemo wa asili yetu bali tumeuchukua kutoka kwa Wazungu ambapo mama anaamini katika kulea peke yake watoto bila kuwa na baba. Mwanamke hataki usumbufu. Anaamua kuzaa kadiri pale anapojisikia, tena kwa mtu anayemtaka.

 

Yaani haijalishi anazaa na kijana wa umri wake, mzee au hata kijana mdogo maarufu kama benteni. Yeye ni uamuzi wake. Kwenye akili yake anaamini, ana kila kitu hivyo atachagua mtu wa kuzaa naye.

 

Ni kweli, fedha anazo utamuambia nini? Ana kazi yake nzuri, anapata mshahara wa kuweza hata kumlea mwanaume utamueleza nini? Anataka yeye kuwa na mwanaume fulani na si mwanaume kumpangia masharti ya kuwa naye. Ana jeuri ya fedha. Ukileta za kuleta, anakupiga chini. Haangalii thamani ya penzi kwamba limetoka wapi na lina ukubwa kiasi gani, anachoangalia yeye ni furaha ya moyo wake.

Usipitwe na Matukio, Install App Yako ya Kijanja na Namba Moja Tanzania ya Global Publishers

Android ===>Google Play

iOS ===>Apple Store

Leo atakuhitaji kwa sababu amejisikia kutembea na kijana mdogo, anafanya hivyo na ikiwezekana anakuzawadia mtoto mmoja. Kesho atakuwa na hamu ya kuzaa na mtu mzima mwenye familia yake, anafanya hivyo na ikiwezekana naye anamzawadia mtoto mmoja. Mwanamke wa hivyo ndiyo huhamasisha wenzake wawe kama yeye. Anapokuwa na mashoga zake, maneno yake ni haya: “Mwanaume asikupe stress, kwani
kitu gani? Tafuta hela halafu umuendeshe unavyotaka.

 

Ukiwa na cash ya kutosha mwanaume hakupi shida. Utafanya unavyojisikia. “Utazaa pale utakapohitaji kuzaa. Utazaa na mtu unayemtaka na si anayetaka mwanaume. Ukiwa na hela mwanaume hakusumbui kulea watoto, wewe unapata faraja yako ya kuwa na watoto halafu unawalea mwenyewe, kama ni shule utawasomesha na mahitaji yote utawapa, wanaume uliozaa nao watoto wako watawasikia kwenye bomba.

 

” Ndiyo maana siku hizi tunao wanawake wengi wanaoamini katika hilo. Ndugu zangu, japo si vibaya mwanamke kutafuta fedha lakini anapaswa kutambua umuhimu wa familia na maisha kwa ujumla. Unaweza kuwalea watoto sawa ila watoto watapata malezi mazuri zaidi watakapokuwa na baba yao. Hizi si desturi zetu. Tuache kuiga. Kuigaiga huku wakati mwingine tunaweza kwenda hata kinyume na mpango wa Mungu. Maendeleo ya sayansi na teknolojia yasitusahaulishe kwamba kuna Mungu ambaye ndiye mwenye uweza wa yote.

 

Kuna vitu mtoto anapaswa kuvipata kwa baba yake, si mjomba wala baba mkubwa au baba mdogo. Ustawi wa tabia njema kwa mtoto unajengwa na wazazi wote wawili. Fedha zisikupe jeuri kwani hata wewe unapoishi na kuitwa mke wa mtu kuna heshima yake. Unapata hadhi katika jamii.

 

Unatambulika kama mke wa mtu. Kuna wakati watoto watahitaji ‘ukali’ kidogo wa baba ili kuwatengeneza kitabia. Wanahitaji ufuatiliaji wa karibu kitabia hususan watoto wa kiume. Ukiwalea peke yako ni rahisi kukuzidi ujanja na mwisho wa siku kuishia katika makundi yasiyoeleweka. Utakuwa na kazi nzuri, una fedha za kutosha lakini hazisaidii katika kuwalinda kitabia.

 

Matokeo yake utatengeneza watoto wahuni, wavuta bangi na hata madawa ya kulevya. Kesho na kesho kutwa haupo duniani, hutakuwa umewaacha salama. Watoto watakosa misingi mizuri ya kujitegemea na matokeo yake utakuwa umehusika katika kuharibu kizazi chako. Tukutane wiki ijayo! Waweza nifuata kwenye kurasa zangu katika mitandao ya kijamii. Facebook natumia jina la Erick. Evarist, Twitter ni ENangale na Instagram ni Erick Evarist

Love Story: Erick Evarist Maoni & Ushauri +255 768 811595

Leave A Reply