The House of Favourite Newspapers

Wadau wa Kilimo Ludewa Wakutana na DC Mwanziva

Mkuu wa Wilaya ya Ludewa Victoria Mwanziva, ameongoza Mkutano wa Wadau wa Kilimo Wilayani Ludewa- ambao umetoa mafunzo maalumu kwa Maafisa Ugani wote wa Wilaya ya Ludewa, na kuwakabidhi Pikipiki Maafisa Ugani zitakazo warahisishia maafisa hao kuwafikia wakulima na kuwapa huduma iliyo bora.

Aidha mkuu wa Wilaya ya Ludewa- Victoria Mwanziva amempongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. Samaia Suluhu Hassan kwa kuhimiza uboreshaji wa Sekta ya Kilimo kwa vitendo na kwa ujumla Wilaya ya Ludewa imepokea pikipiki 58 kwaajili ya maafisa ugani ili waweze kuwafikia wakulima kwa urahisi sambamba kutoa vifaa vya kupima udongo ambavyo maafisa ugani hao huvitumia kuwapimia udongo wakulima katika maeneo yao pasipo malipo yoyote.

“Ndugu zangu tuna kila sababu ya kumuunga mkono Mheshimiwa Rais wetu kwa kuwajibika kila mtu kwa nafasi yake kwani sisi kama Wilaya tumehakikisha wakulima wetu wanapata pembejeo kwa wakati na kuwaimarishia masoko tumeendelea kuimarisha vyama vya ushirika kwani kwa kufanya hivyo mkulima ataendelea kuinuka na kukuza uchumi wake binafsi, Wilaya na Nchi kwa ujumla”, amesema Mwanziva.

Wilayani Ludewa- kuna jumla ya hekta 465,030 zinazofaa kwa kilimo cha mazao mbalimbali lakini mpaka sasa zimetumika hekta 167,105 sawa na asilimia 34% pekee ndizo zinazolimwa na kupelekea kubakiwa na ziada ya Hekta 297,925- hii imewasilishwa na Idara ya Kilimo kwenye mkutano huu.

Wilaya ya Ludewa- imegawanyika katika kanda tatu za uzalishaji ambazo ni Ukanda wa Juu, Ukanda wa Kati na Ukanda wa Chini na mazao ya biashara yanayostawi katika Halmashauri ya Wilaya ya Ludewa ni Kahawa, Parachichi, Chai, Pareto, Korosho na Alizeti-
Ardhi ya Ludewa ina rotuba na huzalisha mazao mengi mchanganyiko ikiwemo- Ngano, Mahindi, Maharage, Viazi Mviringo, Apple/Tofaa, Viazi Vitamu, Karanga, Soya, Mpunga, Mhogo, Mtama, Ufuta nk

Naye Mkurugenzi wa Halmashauri ya wilaya hiyo Sunday Deogratius amesema pamoja na kuhitaji wawekezaji katika Kilimo lakini pia wanahitaji mazao yanayozalishwa wilayani humo yaweze kuongezewa thamani ambapo badala ya kusafirisha mazao ghafi yasafirishwe yaliyochakatwa kabisa kama zao la Mahindi, Chai, Kahawa, Pareto, Alizeti na mazao mengineyo hivyo kuna uhitaji mkubwa wa kupata wawekezaji wa kuongeza tija kwenye mnyororo wa thamani wa kila zao.

Gervas Ndaki- Katibu wa Chama Cha Mapinduzi Wilayani humo amesema kwa mujibu wa Ilani ya uchaguzi ya chama hicho ya mwaka 2020/2025 ibara ya 37 imeeleza kuwa katika kipindi cha miaka mitano Chama kitasimamia mapinduzi katika sekta ya kilimo na kuhakikisha kinakuwa kilimo chenye tija na kinachotumia teknolojia ya kisasa.

“Kila tunachokifanya ni utekelezaji wa ilani yetu ya uchaguzi kwani imetuambia tutambue maeneo na aina ya kilimo kinachokubali katika maeneo husika na imeweka msisitizo huu kwakuwa asilimia 65 ya watanzania wote ni wakulima hivyo kilimo ni chanzo kikubwa cha uchumi wetu hivyo hatuna budi kukitilia mkazo katika kuboresha kilimo hiki” amesema Ndaki.

Mkutano huu wa wadau umeleta wadau wa Sekta ya Kilimo Wilayani Ludewa umehudhuriwa na Uongozi wa Serikali na Chama Cha Mapinduzi, na wadau wa Sekta ya Kilimo wakiwemo Wawakilishi wa Taasisi zinazofanya kazi kwenye Sekta ya Kilimo kama SAGCOT, TARI, TFRA, TFC, TCB.
Kampuni zinazofanya mawasilisho ni sambamba na Intracom, Mtewele General Supply, City Coffee, Pyrethrum Company of Tanzania (PCT), Kibo Seeds, East West Seeds na mengine mengi kwa lengo ka kutoa Elimu kuhusu kazi na bidhaa zao.

Wanachama wa vyama vya Ushirika (AMCOS) nao walishiriki na kiujumla Mkutano umeleta chachu na hamasa mpya kwa Ma-Afisa Ugani kwani walibainishwa Ma-Afisa ugani bora na kupewa vyeti na utambulizi rasmi wa kazi zao Wilayani Ludewa.

Naibu Waziri wa Wizara ya Kilimo Mheshimiwa David Silinde alipata wasaa wa kuzungumza na hadhira hiyo kupitia simu na alizidi kuahidi ushirikiano kutoka Wizara ya Kilimo.
Kilimo ni uti wa mgongo wa Wilaya ya Ludewa na kwa pamoja sekta hii itaendelea kupiga hatua kwa ushirikiano na mikakati endelevu ya kuongeza tija katika uzalishaji Wilayani Ludewa.