The House of Favourite Newspapers

Waendesha Bodaboda Korogwe Tanga Wapewa Mafunzo ya Usalama Barabarani

0
Shirika la Amend Tanzania kupitia ufadhili wa Ubalozi wa Uswiss nchini limetoa mafunzo na elimu ya usalama barabarani kuhusu sheria na alama za barabarani kwa  madereva bodaboda wa Wilaya ya Korogwe mkoani Tanga sambamba na kukumbushwa umuhimu wa kukatia bima pikipiki zao pamoja na kuwa na leseni ya udereva.
Akizungumza na madereva bodaboda hao, Hamisi Mbilikila kutoka Ofisi ya Mkuu wa Usalama Barabarani Mkoa wa Tanga ametumia nafasi hiyo kueleza ni muhimu kwa waendesha bodaboda na baji kuzingatia sheria za Usalama Barabarani na lengo la Mafunzo hayo ni kuendelea kuwakumbusha wajibu wa kufuata Sheria na hatimaye kuepuakana na ajali.
“Nimefuatana na Mratibu wa Shirika la Amend  lengo ni kuja kutoa elimu ya usalama barabarani kwa waendeshaji wa vyombo vya moto hapa Korogwe na takwimu zinaonesha kwa Mkoa wa Tanga  , Wilaya ya Korogwe kuna ajali nyingi za barabarani ukilinganisha na Wilaya nyingine katika mkoa wetu.
“Tunataka mjifunze sana kuhusu elimu ya usalama barabarani kwasababu riziki zenu mnazipata kwa kutumia vyombo vya moto, hivyo mnapaswa kuviheshimu vyombo hivyo pamoja na sheria za usalama barabarani.Ukienda kinyume tu utakuta na faini na matokeo yake hata fedha uliyotegemea kupeleka nyumbani inaishia barabarani.”
Ameongeza  pia ni muhimu kwa madereva bodaboda kuvaa kofia ngumu, kukata leseni,kuwa na bima pamoja na kutobeba abiria zaidi ya mmoja kwani sheria hairuhusu dereva kuendesha bodaboda bila kufuata taratibu zilizowekwa kisheria na kwa upande wa bima ni muhimu kwani ikitokea ajali bima itasaidia katika kufanya matengenezo ya chombo kilichoharibiwa na leseni inasaidia kumtambua anayeendesha ni dereva.
“Tunakuja kutoa elimu ya usalama barabarani kwa kushirikiana na Amend kwa kutambua tunaowajibu wa kuhakikisha mnaendelea kuwa salama na hakuna anayekufa kwa ajali kwasababu tu hajui sheria za Usalama Barabarani.Tunaomba wale ambao wamepata elimu hii wakawe mabalozi kwa wengine,tunataka elimu hii ifike kwa watu wengi zaidi.”
Ametumia nafasi hiyo kutoa shukrani kwa Amend na Ubalozi wa Uswiss kwa kuona umuhimu wa kutolewa kwa elimu ya usalama barabarani kwa madereva bodaboda kwani kufanya hivyo ni kuendelea kumpunguza ajali za barabarani katika Mkoa huo wa  Tanga.
Kuhusu kupakia mshikaki,amewataka madereva bodaboda kutobeba abiria zaidi ya mmoja kwani mbali ya kupata fedha kidogo lakini inaharibu pikipiki kutokana na uzito mkubwa na matokeo yake anatumia fedha nyingi katika matengenezo kuliko hela aliyopewa.
“Mnapakia mshikaki abiria wanne lakini unapewa Sh.2000 wakati hao watu wanne wangepakiwa na pikipiki moja moja na kila mwenye bodaboda akapata hela.Pia tunatamhua pikipiki ni usafiri wa haraka lakini baadhi ya  bodaboda wamesababisha muwe mnasemwa.”
 Kwa upande wa madereva bodaboda katika Wilaya ya Korogwe wamelishukuru Shirika la Amend kwa kuona haja ya kutoa Mafunzo hayo kwa kushirikiana na Kikosi cha Usalama Barabarani Mkoa wa Tanga huku wakiendelea kuomba elimu hiyo kuendelea kutolewa kwa madereva bodaboda wengi zaidi.
Wakati huo huo Mratibu wa Shirika la Amend Ramadhan Nyanza amesema wameona kuna kila sababu ya kuliangalia kundi hilarious kwani pamoja na kutoa huduma ya kusafirisha abiria lakini ndio kundi ambalo linapata ajali.
Amesisitiza elimu ya usalama barabarani ambayo wanaitoa inalenga kuendelea kuwajengea uwezo madereva bodaboda kuwa makini wawapo barabarani sambamba na kupewa mafunzo ya huduma ya kwanza ili ajali inapotokea iwe rahisi kutoa huduma ya kwanza na hivyo kunaweza kusaidia kuokoa maisha ya aliyepata ajali.
Leave A Reply