The House of Favourite Newspapers

Wafahamu Wagombea Urais Wanaochuana na Magufuli

0

TOFAUTI na miaka iliyopita ya uchaguzi nchini Tanzania, mwaka huu wagombea wa nafasi za urais wamejitokeza kwa wingi. Kwa mujibu wa tume ya uchaguzi nchini Tanzania, wagombea 17 wa urais wamejitokeza kuchukua fomu za kuwania nafasi hiyo ya juu zaidi.

 

Wagombea kutoka vyama mbalimbali vya upinzani na chama tawala, walianza kuchukua fomu za kugombea urais mapema mwezi huu. Mwezi Oktoba Tanzania inatarajiwa kuingia katika uchaguzi wa wabunge, wawakilishi, madiwani na rais.

 

Wagombea wa Urais na Vyama Vyao

Queen Cuthbert Sendinga – Alliance for Democratic Change (ADC)

Chama hiki kinawakilishwa na mgombea wa kike Bi Queen Cuthbert Sendinga. Bi Sendinga ni naibu katibu mkuu wa chama cha ADC Tanzania bara. Amewahi kugombea ubunge jimbo la Kawe mwaka 2015 kwa tiket ya ADC.

 

Kwa upande wa elimu, ana stashada ya biashara. Anajishughulika na masuala ya biashara, ujasiriamali na ukulima. Ameahidi kuwakomboa Watanzania wa kipato cha chini kama atachaguliwa kuwa rais.

 

Bernard Kamillius Membe – ACT Wazalendo

Bernard Kamillius Membe huyu ni mgombea wa urais mwenye ushawishi wa aina yake, amewahi kuhudumu katika nafasi mbalimbali ikiwemo ya  waziri wa mambo nje na ushirikiano wa kimataifa.

 

Mapema mwaka huu alifutwa uanachama wake kutoka chama tawala cha CCM kisha kaamua kuhamia chama cha ACT Wazalendo na kutia nia yake hii ya kugombea urais. Alizaliwa katika kijiji cha Rondo, mkoani Lindi mnamo Novemba 9 mwaka 1953.

 

Ni mhitimu wa masomo ya Sayansi ya Siasa katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam na Shahada ya Uzamili katika Uhusiano wa Kimataifa aliyoipata katika Chuo Kikuu cha John Hopkins nchini Marekani.

 

Membe anasimamia ilani ya chama chake katika uchaguzi na ikiwa atachaguliwa basi ataanza kutekeleza. Ilani hiyo inasisitiza juu yaa ujenzi wa demokrasia, ufanisi na ubora wa huduma za afya pamoja na kilimo cha kimapinduzi na mazingira wezeshi ya kibiashara.

 

Dkt. John Pombe Magufuli – CCM

Wagombea kutoka CCM John Magufuli na Samia Hassan ndiyo walikuwa wa kwanza kupitishwa na NEC.

 

Huyu ni rais wa sasa wa Tanzania na anasaka muhula wa pili wa uongozi wake. Ikiwa atapatiwa ridhaa  atamalizia kipindi cha miaka mitano ijayo na kukamilisha mihula miwili kama inavyosema katiba ya Tanzania.

 

Magufuli amekuwa katika uongozi wa nchi pamoja na chama chake cha CCM katika nyadhifa mbalimbali.

 

Amekua mbunge wa eneo analotoka huko Chato tangu mwaka 1995 kisha kuhudumu katika wizara mbalimbali ikiwemo Wizara ya Ujenzi na Ardhi. Mwaka 2015 alijitosa kuwania nafasi ya urais kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM) na kushinda nafasi hiyo, hivi sasa anatarajia kutetea nafasi hiyo na kama atashinda basi atahudumu kwa miaka mingine mitano.

 

Ana shahada ya udaktari katika kemia kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.

 

Profesa Ibrahim Lipumba – CUF

Profesa Ibrahim Lipumba, Mwenyekiti wa chama cha siasa cha CUF Tanzania. anawania nafasi hii ya urais kupitia chama chake cha CUF kwa upande wa Tanzania bara. Hii ni mara ya tano kugombea nafasi hii.

 

Anawania nafasi hii wakati ambao chama chake kimepata pigo la kuondokewa na kiongozi mwenza na mwenye ushawishi mkubwa Seif Sharif Hamad kwa pande zote Tanzania bara na Zanzibar. Hatua ambayo ilisababisha mgawanyiko wa chama hiko, huku baadhi wakimfuata Seif Sharif Hamad na kujiunga na chama cha ACT Wazalendo.

 

Lipumba elimu yake ya juu ameipata katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam akihitimu shahada ya kwanza katika uchumi mwaka 1976 na shahada ya umahiri mwaka 1978.

 

Ana shahada ya uzamivu (PhD) ya uchumi kutoka Chuo Kikuu cha Stanford nchini Marekani. Profesa Lipumba anaamini zaidi katika sera za soko huria na falsafa ya uliberali, ambayo ndiyo itikadi ya Chama cha Wananchi

 

Tundu Antiphas Lissu – CHADEMA

Tundu Lissu ni mgombea wa Chama cha Demokrasia na Maendelo (CHADEMA) kwa upande wa Tanzania Bara.

 

Lissu amewahi kuhudumu katika bunge la Tanzania akiwa ni mbunge wa Singida Mashariki, pia amewahi kuwa Rais wa Chama cha Wanasheria cha Tanzania (TLS) na Mwanasheria Mkuu wa CHADEMA.

 

Lissu kitaaluma ni mwanasheria na kwa miaka kadhaa sasa,  amejipatia sifa kama wakili mashuhuri, mwanasiasa shupavu wa upinzani na mkosoaji mkuu wa serikali.  Alipigwa risasi jirani na nyumbani kwake mjini Dodoma na kujeruhiwa vibaya mwezi Septemba mwaka 2017, na watu wasiojulikana.

 

Alikuwa nje ya Tanzania kwa matibabu kwa karibu miaka mitatu, alisafirishwa hadi Nairobi kwa matibabu ya awali, Baada ya hapo alisafirishwa hadi chini Ubelgiji alipoendelea kufanyiwa upasuaji. Sasa amarejea rasmi nyumbani na kushirikia katika kuwania nafasi ya urais.

 

Katika hutoba yake ya kutangaza nia ya kugombea Urais Lissu amesisitiza juu ya haki za binadamu na jinsi gani zimekuwa zikikiukwa basi kama atachaguliwa kuwa Rais wa Tanzania, atahakikisha kuwa kuna usawa na haki za binadamu zinafuatwa.

 

Cecilia Augustine Mwanga – Demokrasia Makini

Tume ya Taifa ya Uchaguzi imewateua wagombea wa kiti cha Rais na Makamu wa Rais kwa tiketi ya Demokrasia Makini, Bi. Cecilia Augustino Mwanga na Tabu Mussa Juma.

 

Mgombea mwingine wa kike aliyechukua fomu za uteuzi kutoka tume ya taifa ya uchaguzi ni Bi Mwanga anawakilisha chama chake cha Demokrasia Makini. Chama hiki kimesajiliwa mwaka 2001. Katika uchaguzi wa mwaka huu, sera yao wanasisitiza juu ya kilimo kwani ndio uti wa mgongo wa uchumi wa Tanzania.

 

Bi Mwanga ameahidi kuwa atafanya kampeni zake kwa kutumia usafiri unaotumika sana vijijini, kama Baiskeli na Guta.

 

Hashim Rungwe Spunda – (CHAUMMA)

Spunda aliwania urais 2010 kupitia chama cha NCCR Mageuzi lakini akapata asilimia 0.3 ya kura. Ni wakili wa Mahakama Kuu anayehudumu kibinafsi. Anatoka eneo la Ujiji, Kigoma.

 

Spunda, alikuwa mfuasi sugu wa Tanu na baadaye CCM, na baada ya kuingia kwa siasa za vyama vingi 1992 alisalia chama tawala miaka mingine mitatu kabla ya kujiunga na NCCR Mageuzi 1996.

 

Aliondoka NCCR Mageuzi 2012 na kuanzisha CHAUMMA, chama ambacho yeye ndiye mwenyekiti wa kitaifa. Aligombea urais tena mwaka 2015 kuptia chama chake cha CHAUMMA. Aliwania ubunge mara mbili bila kufua dafu, 1995 jimboni Kawe na 2005 jimbo la Kinondoni.

 

Seif  Maalim  Seif – AAFP

Huyu ni mgombea wa kwanza kuchukua fomu katka nafasi ya kiti cha urais kupitia chama cha AAFP. Amezaliwa mwaka 1974. Kama atachaguliwa anasisitiza juu ya mabadiliko nchini Tanzania kama ajenda yao inavyosema ‘mabadiliko kwa maendeleo’.

Wakati akichukua fomu Seif alisisitiza pia uchaguzi huu utakua wa ushindani na wao wamejipanga vizuri.

 

Khalfan Mohamed Mazrui – Union for Multiparty Democracy (UMD),

Huyu ni mgombea wa nafasi ya urais na mwenyekiti wa chama cha UMD. Chama hiki ni miongoni mwa vyama vidogo nchini Tanzania na hakina ushawishi mkubwa. Wameshiriki katika uchaguzi kwa miaka tofauti na si mara nyingi wanasimamisha mgombea urais.

 

John Paul Shibuda – ADA-TADEA

John Shibuda kutoka chama cha ADA-TADEA pia amepitishwa na tume.

Shibuda amezaliwa mwaka 1950. Amekuwa ni mbunge wa Jimbo la Maswa kwa muda mrefu akihudumu kwa tiketi ya CCM kisha mwaka 2010 aliamua kujiunga na chama cha CHADEMA. Baadaye  akaamua kuhamia chama cha ADA-TADEA ambapo ndipo anagombea urais kwa sasa.

 

Yeremia Kulwa Maganja – NCCR Mageuzi

Yeremia Maganja wa NCCR-Mageuzi baada ya kupitishwa na NEC. Maganja ana shahada ya uzamili ya Usimamizi wa Biashara kutoka Chuo Kikuu cha Mzumbe. Alijiunga na chama hiki mapema mwaka huu.

 

Kama atachaguliwa kuwa Rais wa Tanzania, ana sera ya kuimarisha sera na sheria za biashara ili ziwe Rafiki.

 

Philipo John Fumbo – Democratic Party (DP)

Fumbo ni mwenyekiti wa chama cha DP na amekuwa ndani ya chama hiko kwa zaidi ya miaka 15 kama mwanachama na kiongozi. Pia amekuwa mgombea wa pili kuchukua fomu za kugombea nafasi hiyo kwa tiketi ya chama cha DP.

 

Ameahidi ushindi kwa wanachama wa chama chake, na kutilia mkazo sera zao ambazo zinawabeba watu wenye hali duni.

 

Leopard Lucas Mahona – National Reconstruction Alliance (NRA)

Tume ya Taifa ya Uchaguzi imewateua wagombea wa kiti cha Rais na Makamu wa Rais kwa tiketi ya NRA,  Leopold Mahona na Hamid Ally Hassan.

 

Mahona amesimamishwa na chama chake kama mgombea wa nafasi ya urais, NRA ni miongoni mwa vyama vidogo nchi Tanzania. Mahoma ametoka vyama kadhaa vya siasa kama CUF kabla ya kujiunga na chama hiki.

 

Pia amewahi kugombea nafasi ya ubunge jimbo la Igunga kupitia chama cha wananchi CUF. Kama ilivyo kwa wagombea wengine kutoka vyama vidogo vidogo, Mahoma anajaribu bahati yake ya kuwa Rais wa Tanzania.

 

Muttamwega Mgaywa – Sauti ya Umma (SAU)

Tume ya Taifa ya Uchaguzi imewateua wagombea wa kiti cha Rais na Makamu wa Rais kwa tiketi ya SAU, Bw. Muttamwega Mgaywa na Bi. Satia Musa Bebwa. Mgwaya si mgeni katika kuwania nafasi hii. Mwaka 2010 aliwania Urais wa Tanzania kupitia chama cha Tanzania Labor Party (TLP).

 

Wakati wa kuchukua fomu, wagombea hawa walienda na aina tofauti ya kuingia bila viatu katika jengo la tume ya uchaguzi na kusema kuwa ni alama kuwa wapo pamoja na wanyonge wasiojiweza. Kipaumbele na sera ya mgombea huyu ni kilimo, anasema kuwa anataka kuwakomboa wakulima hususani wa mazao ya biashara.

 

Twalib Ibrahim Kadege – UPDP

Kadege anagombea nafasi ya Urais kupitia tiketi ya chama cha United Peoples’ Democratic Party (UPDP). Alikuwa mgombea wa saba kuchukua fomu ya nafasi hiyo. Kama ilivyo kwa wagombea wengine kutoka vyama vidogo, Kadege ana nafasi ndogo ya ushawishi wa kupata nafasi hii.

 

Maisha Mapya Muchunguzi – National League for Democracy (NLD)

Muchunguzi anasimama kama mgombea wa urais kupitia chama cha NLD. Chama hiki ndio miongoni mwa vyama vya mwisho kufanya maamuzi ya kuteua wagombea wa nafasi hii, kwa upande wa Tanzania bara na Zanzibar.

 

Kama atafanikiwa kuchaguliwa Muchunguzi anasema kuwa ataweka msisitizo wa kuendeleza wakulima na wafugaji pamoja na wavuvi wa Tanzania kuwa na mazingira mazuri ya kufanya kazi kwa faida.

Leave A Reply