The House of Favourite Newspapers
gunners X

Wafanyabiashara 200 Watanzania Wawekwa Karantini Kenya

0

WAKATI maambukizi ya Virusi vya Corona yakizidi kushika kasi nchini, zaidi ya Watanzania 200 wanaofanya biashara nchini Kenya, wamekamatwa na kuwekwa karantini wilayani Kiteto baada ya kurejea kwa kupitia njia za ‘panya’.

 

Hatua hiyo imekuja baada ya wafanyabiashara hao ambao pia ni wakazi wa mipakani kutimuliwa nchini humo kutokana na agizo la Rais Uhuru Kenyatta kuwataka watu kutotoka nje kuanzia saa moja usiku hadi saa 12 asubuhi.

 

Kenya ambayo hadi April 15 mwaka huu ilikuwa na watu 208 walioambukizwa Corona ambao kati yao tisa walifariki, Machi 27 mwaka huu ilitangaza amri ya kutotoka nje kuanzia saa moja usiku hadi saa 12 asubuhi ili kudhibiti virusi hivyo.

 

Hata hivyo, wafanyabiashara hao wa bodaboda, umachinga na mbuzi, wanadaiwa kurejea nchini kimya kimya hali iliyomlazimu Mkuu wa Wilaya ya Kiteto, Tumaini Magesa kufuatilia watu hao na kuwekwa karantini ili kukabiliana na maambukizi ya Virusi hivyo nchini.

 

Hadi Aprili 15 mwaka huu, Tanzania ilikuwa na wagonjwa 59 wa Corona, kati yao saba wamepona na wanne wamefariki.

 

Akizungumza na IJUMAA, Magesa alisema wakazi hao wanatoka katika vijiji vitatu vya Njiapanda, Engusero na Losoit.

 

Alisema alipata taarifa kuwa kuna makundi ya watu tofauti, yamewasili wilayani humo yakitokea nchi ya Kenya wakikwepa maambukizo ya virusi vya Corona ambavyo sasa vimekuwa tishio duniani.

“Sio rahisi kupata taarifa hizi, mimi nimezipata kwa kutumia vyombo vyangu…nimekutana na kijana mmoja ambaye ametoa ushirikiano mzuri.

 

“Alinifafanulia kuwa huwezi kukuta boma la Kimasai lenye mifugo mingi katika kijiji cha Njia Panda, lisiwe na kijana anayeishi Kenya,” alisema DC Magesa.

 

Alisema vijana hao wanafanya shughuli za umachinga, kuendesha bodaboda na kurejea Tanzania.

“Ingawa kule Kenya wanakwenda kisheria, lakini sasa Corona ndio imewaibua na kuja nchini bila kuwekwa karantini. Sasa tayari tumewaweka karantini, tunafuatilia afya zao, lakini pia familia zao tunazifuatilia kujua maendeleo yao kiafya ingawa hadi sasa hakuna mwenye maambukizi,” alisema.

 

Alisema katika siku za karibuni, biashara ya mbuzi ilishamiri wilayani Kiteto ambapo vijana wengi walisafirisha kwa malori mbuzi hao na kuwapeleka Kenya kabla ya kuathiriwa na ugonjwa huo wa COVID- 19.

 

Alisema mbali na wananchi katika Kijiji hicho, pia kuna baadhi ya wananchi wachache wanaoishi nchini Oman na wengine 17 kutoka Mataifa mbalimbali ambao wameolewa na vijana wa jamii ya kifugaji ya Wamasai.

 

“Kila wilaya tumetenga maeneo kwa ajili ya wagonjwa wa Corona, mpaka sasa hatuna mgonjwa hata mmoja, ila tuna eneo la shule ya Sekondari Kiteto, Engusero, Matui na Sunya ambako yatatumika kabla ya wanafunzi hawajarejea shuleni” alisema.

 

Kuhusu vifaa vya kujikinga na virusi vya Corona kama vile barakoa, sanitizer na hata ndoo za maji kwa ajili ya kunawa mikono, mkuu huyo wa wilaya alisema, Serikali haina mpango wa kuwanunulia wananchi vifaa hivyo, hivyo wachukue tahadhari kujinunulia wenyewe.

 

Hata hivyo, Magesa alisema pamoja na jitihada wanazofanya kutoa elimu juu ya tahadhari ya Virusi vya Corona, changamoto kubwa iko kwa watu wanaouza pombe za kienyeji ambao wanashirikiana kunywa pombe kwenye chombo kimoja kwa kupokezana.

 

“Tunalo tatizo la baadhi ya watu wanaokunywa pombe za kienyeji, hawa wameendelea kutokuwa na tahadhari kwani hata kama watanawa mikono yao mwanzo, wakianza kulewa wanazidiwa na pombe na kugaragara chini kwenye vumbi, hivyo kutozingatia kukabiliana na CORONA,” alisema.

 

Aidha, Diwani wa Kata ya Kasimba, Paulo Tunyoni (CCM) alisema kuna changamoto kubwa katika kukabiliana na ugonjwa huo kwa sababu jamii hiyo ya kifugaji wilayani humo, inaamini kuwa COVID- 19 ni ugonjwa wa watu wa mjini.

 

Aidha, baadhi ya wakazi wa wilaya hiyo, waliiomba serikali kuboresha huduma za maji ili kukabiliana na Corona kwa sababu hadi sasa asilimia 48 pekee ya wakazi wa Kiteto ndio waliopata maji safi.

Stori: Mohamed Hamad, Kiteto

Leave A Reply