Wafanyabiashara Waipongeza Serikali Kushughulikia Changamoto za Kikodi
Wafanyabiashara wanachama wa Jukwaa la Wafanyabiashara wa Afrika Kusini nchini Tanzania (SABFT), wametoa pongezi za serikali za nchi zote mbili kwa kushughulikia changamoto ya kero za kikodi zilizokuwa zikiwakabili kwa muda mrefu.
Akizungumza jijini Dar es Salaam jana wakati wa mkutano wa wafanyabiashara hao, uliofanyika kwa udhamini wa Benki ya Absa kwa kushirikiana na Shirika la Ndege la Afrika Kusini (SAA), Mwenyekiti wa Jukwaa hilo, Bw. Manish Thakrar alisema changamoyo ya kodi kutozwa mara mbili imekuwa kilio cha muda mrefu kwao lakini kutoka juhudi zinazoendelea kufanywa kwa ushirikiano wa serikali za Tanzania na Afrika Kusini, chemba za biashara na wadau wengine ni imani yao hadi kufikia mwisho wa mwaka huu kero hizo zitakuwa zimeondolewa kabisa.
Alisema Jukwaa la Wafanyabiashara wa Afrika Kusini nchini Tanzania (SABFT) lilianzishwa miaka 24 iliyopita kwa lengo kubwa la kuwaunganisha wawekezaji kutoka nchini huko na wawekezaji wa Tanzania wenye ni ya kuwekeza nchini Afrika Kusini hivyo kunufaika na fursa zinazopatikana katika pande zote mbili.
“Kipindi kutoka mwaka 1997 kupitia mpango wa ubinafsishaji, kimsingi kumekuwa na ongezeko kubwa la uwekezaji wa wafanyabiashara kutoka Afrika Kusini katika miradi mikubwa katika sekta za mawasiliano, uzalishaji, vinywaji na vyakula, hivyo kutoa fursa za ajira kwa watanzania pia kunufaisha wafanyabiashara wa ndani.
“Natoa shukurani za kipekee kwa Benki ya Absa Tanzania kwa udhamini mkubwa katika tukio hili, lakini pia tunaipongeza benki hii kwa jinsi inavyoweka juhudi katika kutoa huduma na bidhaa pamoja na masuluhisho mbalimbali katika kusaidia mahitaji ya kifedha kwa wafanyabiasha wa Afrika Kusini na wa Tanzania”, alisema Bw. Thakrar.
Akizungumza wakati wa mkutano huo, Mkurugenzi wa Masoko ya Fedha za Kigeni wa Benki ya Absa Tanzania, Bi. Irene Rwegalulira akimwakilisha Mkurugenzi Mtendaji wa benki hiyo, Bw. Obedi Laiser alisema, wamejipanga vizuri katika kuhudumia wateja wao kutoka nje ya Tanzania kwa ubunifu zaidi ikiwa na masuluhisho tofauti ya huduma za kibenki kwa wateja wadogo, wa kati na wakubwa.
“Majukwaa kama haya yana faida sana kwani sisi benki tunakuja kama kiunganishi ili tuweze kuwasaidia katika biashara zao zinazohitaji huduma za kifedha kama vile mikopo, fedha za kigeni, pamoja na ushauri wa namna bora ya kufanya biashara nchini Tanzania kulingana na taratibu na miongozo ya serikali.
“Absa inafanya biashara sambamba na lengo kuu la kuanzishwa kwake ambalo ni Kuiwezesha Afrika na Tanzania ya Kesho Pamoja, hatua moja baada ya nyingine, huku tukiongozwa na ahadi mpya ya chapa ya benki yetu isemayo ‘Story yako ina thamani’ hivyo kwa kutoa huduma bora za kibenki kwa wafanyabiashara hawa, tunaamini tunasaidia kuandika story za mafanikio za wateja wetu kwa manufaa yao na maslahi mapana ya Tanzania na Afrika Kusini”, alisema Bi. Irene.
Jukwaa na Wafanyabiashara wa Afrika Kusini kwa sasa lina jumla ya wanachama 100 kutoka katika sekta mbalimbali kama vile mabenki, madini, mawasiliano, viwanda vya uzalishaji, maduka makubwa na nyinginezo.