The House of Favourite Newspapers

Wafanyakazi 5 wa CI-Group Wahukumiwa kwa Kuishi Nchini Kinyemela

0

Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu imewahukumu wafanyakazi watano wa Kampuni ya Uchapaji ya CI-Group Co. Ltd, kulipa Sh 52.5 milioni ama kutumikia kifungo cha miaka mitatu jela kila mmoja.

Uamuzi huo umefikiwa baada ya wafanyakazi hao kukubali makosa yaliyokuwa yakiwakabili ikiwamo kuishi nchini isivyo halali.
Hukumu hiyo imetolewa leo Jumanne, Julai 25 na Hakimu Mfawidhi, Cyprian Mkeha.

Washtakiwa hao Shashi Upadhyay (31) raia wa India, Mhasibu Didar Karim (39), raia wa Pakistani, Ashish Joshi (24), raia wa India, Manzoor Islam (31) raia wa Pakistani na Mohan Gaikwad (32) raia wa India walifanikiwa kulipa kiasi hicho cha fedha na kukwepa adhabu ya kifungo.

Hatua hiyo ilifikiwa na Hakimu Mkeha baada ya washtakiwa hao kusomewa mashtaka hayo yanayowakabili na Mwendesha Mashtaka wa Uhamiaji, Method Kagoma, kuyakubali na kuwasomea maelezo ya awali (PH) na hatimaye kutiwa hatiani kwa makosa hayo ikiwamo kuishi nchini isivyo halali.

Kagoma, alidai Julai 20, 2017, katika ofisi za Kampuni ya CI-Group Co. Ltd iliyopo wilaya ya Kinondoni, Dar es Salaam, wakiwa si raia wa Tanzania, walikutwa wakiishi nchini isivyo halali.

Amedai kuwa siku hiyo, pia walikutwa wakiwa wameingia kwenye ajira bila ya kuwa na kibali cha kufanyia kazi.

Baada ya kusomewa mashtaka hayo, walikubali na upande wa Jamhuri uliomba ahirisho la nusu saa kwa ajili ya kuandaa maelezo ya awali (PH) ambapo Hakimu Mkeha alikubali na baadaye waliporudi walisomewa maelezo ya awali ambayo nayo pia waliyakubali.

Kutokana na kukubali kwao huko, Hakimu Mkeha aliwatia hatiani na kumtaka kila mshtakiwa kulipa faini ya Sh 500,000 katika shitaka la kwanza ama kutumia kifungo cha miaka mitatu jela na kulipa faini ya Sh 10 milioni katika shtaka la pili ama kutumikia kifungo cha mwaka mmoja jela. Hata hivyo walifanikiwa kulipa.

Leave A Reply