Wafanyakazi wapigwa faini kwa kutotembea hatua 180,000 kwa mwezi China

 

Kampuni moja nchini China imeshutumiwa vikali kwa kuwapiga faini wafanyakazi wanaokosa kutembea takriban hatua 180,000 kwa mwezi.

 

Kulingana na gazeti  la Information Times, wafanyakazi wa kampuni moja ya biashara ya nyumba kwenye mji ulio kusini wa Guangzhou, wamepigwa faini ya yuan 0.01 kwa kila hatua ambayo walikosa kutembea walipokuwa wanajaribu kufikia kiwango hicho.

 

Mfanyakazi mmoja ‘Little C’, aliliambia gazeti hilo kuwa kufanyishwa kazi muda zaidi baada ya zamu kuisha imekuwa ni vigumu kwa mfanyakazi kutembea hatua 6,000 kwa siku nje ya saa za kazi.

 

“Ninafahamu kuwa kampuni inataka tufanye mazoezi zaidi,” alisema, “lakini hata sina muda wa kutosha wa kulala kwa sababu ninataka kutembea na kufikisha malengo hayo.”

 

Liu Fengmao, mwakilishi kutoka kampuni moja ya sheria, anasema kampuni hiyo haina haki kisheria kufuatilia kutembea kwa wafanyakazi kama kipimo cha kufanya kazi na hivyo sheria kama hiyo kazini itaongeza changamoto zaidi kwa mfanyakazi.

 

Bw Liu anasema wafanyakazi wana haki ya kudai kuwa kutembea nje ya saa za kazi ni kazi ya ziada au kupata jeraha ukitembea ni sawa na kujeruhiwa ukiwa kazini.

 

Information Times inasema kuwa hiki si kisa cha kwanza cha kampuni kuweka sheria ya kutembea kazini.

 

Mwezi Januari mwaka 2017 kampuni moja ya teknolojia huko Chongqing kusini magharibi mwa nchi hiyo, ilikosolewa kwa kuwalazimisha wafanyakazi kutembea hatua 10,000 kwa siku.

 

Gazeti moja la The Chongqing Evening Post lilisema kampuni hiyo ilitumia kutembea kwa wafanyakazi kama njia ya kupima uwezo wao kikazi.

Toa comment