Waganga wa Tiba Asili Kutoka Afrika Mashariki Kuweka Historia Kwenye Maadhimisho ya Mwaka Mmoja wa Mzimu wa Afrika
Katika tukio la kihistoria linalotarajiwa kuvuta hisia za watu wengi, maadhimisho ya mwaka mmoja wa Mzimu wa Afrika yanatarajiwa kufanyika katika Kijiji cha Kwa Msanja, Wilaya ya Chalinze, Mkoa wa Pwani, kuanzia tarehe 5 hadi 7 Septemba 2024.
Maadhimisho haya yamepewa umuhimu mkubwa na yatashuhudia matukio makuu yenye lengo la kuimarisha na kukuza tiba za asili katika eneo la Afrika Mashariki.
Akizungumza na waandishi wa habari leo, Dkt. Riziki Mkali Malela, aliyekuwa mstari wa mbele katika maandalizi ya tukio hili, amesema maadhimisho haya yanalenga kuwatambulisha na kuwaunganisha waganga wa tiba asili pamoja na wadau kutoka ndani na nje ya Afrika.
“Maadhimisho haya yana umuhimu wa pekee katika kuwatambulisha waganga wa tiba asili kutoka Afrika Mashariki juu ya uwepo wa mzimu huu, pamoja na kushirikiana na wadau mbalimbali kutoka ndani na nje ya Afrika,” amesema Dkt.
Riziki Mkali Malela.
Maadhimisho hayo yatakuwa na matukio matatu makuu. Kwanza, viongozi wa Chama cha Tiba Asili na Utafiti wa Mitishamba (UMAWATI) wataapishwa rasmi ili kuongoza juhudi za kuimarisha tiba asili na kuendeleza utafiti wa mitishamba katika eneo hili.
Pili, kutakuwa na utoaji wa elimu kuhusu uchimbaji na uandaaji wa dawa za asili, ambapo waganga wa tiba asili na watafiti watapata mafunzo maalum ya kuongeza ufanisi katika tiba zinazotolewa.
Tatu, zoezi la matibabu kwa magonjwa mbalimbali litafanyika bure kwa siku tatu, na wananchi watapata fursa ya kutibiwa bila gharama yoyote.
Mbali na matukio hayo, burudani za asili zitakuwepo ikiwemo nyimbo na ngoma za kikundi maalum kutoka eneo husika. Aidha, kutakuwa na zoezi la utoaji wa kafara kwa mizimu ili kuhakikisha ufanisi wa tukio hili muhimu.
“Tunawaalika Watanzania wote na wadau mbalimbali kushiriki katika maadhimisho haya. Ni fursa ya kipekee kwa jamii kufahamu thamani ya miti ya asili katika tiba na kupata matibabu kwa changamoto mbalimbali,” amehitimisha Dkt. Riziki Mkali Malela.
Kwa wale wanaohitaji usafiri, utaratibu umeandaliwa kuanzia tarehe 4 Septemba 2024, ambapo kundi la kwanza litaondoka kutoka Kunduchi Mtongani, Dar es Salaam, kuelekea katika eneo la tukio. Maadhimisho ya Mzimu wa Afrika yanatarajiwa kuwa na athari kubwa katika kukuza tiba za asili na kuimarisha urithi wa kiafrika kwa jamii za Afrika Mashariki na kwingineko.