WIZARA ya Afya ya Zanzibar imesema wagonjwa wawili wa corona wameongezeka visiwani humo na kufanya idadi ya wanaougua ugonjwa huo Zanzibar kufikia tisa mpaka sasa ambapo wagonjwa hao wapya hawakuwahi kutoka nje ya kisiwa hicho.
Waziri wa Afya wa Zanzibar, Hamad Rashid Mohammed ametoa kauli hiyo leo Ijumaa Aprili 10, 2020 katika mkutano wake na waandishi wa habari na kuitaka jamii kuwa makini zaidi kwa kuwa wagonjwa hao wawili wametoka ndani , hawajawahi kusafiri nje ya Zanzibar.
Jana Waziri wa Afya Tanzania, Ummy Mwalimu katika mkutano wake na viongozi wa dini alisema nchi sasa iko katika hatua nyingine ya maambukizi kwa kuwa sasa yanatokea ndani na si kwa watu wanaotoka nje.
“Tumeanza kuambukizana wenyewe kwa wenyewe. Hii viongozi wangu wa dini naomba niliweke wazi. It’s no longer imported (si maambukizi ya kutoka nje tena). Tumeanza local transmission (kuambukizana).”
“Ndani ya siku chache tutaingia community transmission. Maana yake tutapata mgonjwa ambaye hajui ugonjwa ameupata wapi?”
Alisema maambukizi katika jamii ni hatua ngumu kujua aliyeambukizwa ameupata wapi; “Lazima niwaambie ukweli nisiwafiche. Soon (karibuni) tutaingia katika community transmission. Bado tunatakiwa kuchukua tahadhari na kuongeza juhudi za kukabiliana na ugonjwa huu,” alisema Ummy.


