Wagosi wa Kaya Waicharaza Yanga Mkwakwani
VINARA wa ligi kuu bara Yanga leo Machi 4, wameshindwa kufurukuta katika dimba la mkwakwani jijini Tanga, baada ya kukubali kichapo cha mabao 2-1 dhidi ya wenyeji wa mchezo huo Coastal Union.
Ikishuka dimbani mara ya 22, Yanga ambayo ilikuwa inashikilia rekodi ya kutofungwa msimu, imeshindwa kuendeleza rekodi hiyo na kujiweka kwenye mazingira magumu ya kuongoza ligi hiyo.
Yanga ilianza mechi kwa kasi ikicheza soka la kushambulia na kufanikiwa kupata penati, ambayo hata hivyo mpigaji Tuisila Kisinda alikosa baada ya kipa kudaka mkwaju wake.
Iliwachukua dakika moja Coastal Union kufunga bao la kuongoza kupitia kwa mchezaji Erick Msagati dakika ya 10, baada ya mlinda mlango wa Yanga Farouk Shikalo kushindwa mpira wa krosi.
Alikuwa Kisinda aliyewarudisha mchezoni wananchi, baada ya kuisawazishia Yanga dakika ya 37’ na kwenda mapumnziko matokeo yakiwa ni 1-1.
Muuaji wa Yanga alikuwa Mudathir Said aliyepachika bao safi dakika ya 84’ baada ya ngonga nzuri kutoka kwa Wagosi wa kaya na kuihakikishia timu alama tatu.
Yanga bado inaongoza ligi ikiwa na alama 49 baada ya kucheza michezo 22, wakifuatia na watani zao Simba wenye alama 45 wakiwashuka dimbani mara 19, matokeo hayo yanawapa nafasi Simba ya kuongoza ligi endapo atashinda michezo yake viporo.