The House of Favourite Newspapers

Wahamiaji Haramu 32 Wanaswa Wilayani Pangani

0

ASKARI wa Hifadhi ya Taifa ya Saadani kwa kushirikiana na Jeshi la Polisi wilayani Pangani wamefanikiwa kuwakamata wahamiaji haramu 32 waliokutwa wakiwa karibu na hifadhi hiyo wakisafirishwa kupelekwa nchi za kusini mwa Afrika.

Akizungumza na waandishi wa habari kuhusu kukamatwa kwa wahamiaji hao, Kamishna Msaidizi wa Uhifadhi wa Hifadhi ya Taifa ya Saadani, Grace Lobora, alisema kwamba wahamiaji hao walikamatwa Septemba 27 mwaka huu usiku.

Alisema waikamatwa baada ya kupata taarifa kutoka wananchi wa Kijiji cha Buyuni kupitia Mwenyekiti wa Kijiji hicho, Diwani Akida, ambaye aliwaeleza uwepo wa mazingira yasiyoridhisha kwenye eneo lake hasa eneo la bahari baada ya boti moja kukwama.

 

Alisema baada ya kupata taarifa hiyo wao, kama wahifadhi wana jukumu la kulinda maliasili na kuangalia usalama kwenye miji yote inayowazunguka, waliandaa kikosi-kazi cha kwanza ambapo kilikwenda eneo la tukio na kuwakuta wahamiaji hao eneo la bahari karibu na hifadhi hiyo katika kijiji cha Buyuni.

Alisema baadaye waliamua kutuma kikosi cha pili na ndipo walipofika na kufanikiwa kuwaweka chini ya ulinzi wahamiaji 28 ambao ni raia wa Ethiopia lakini alfajiri  wakapata taarifa nyingine ya uwepo wa wahamiaji wengine wanne ambao ni raia wa Somalia na wakatuma tena kikosi na kufanikiwa kuwaweka chini ya ulinzi.

 

“Kati yao wapo wahamiaji 32 raia wa Ethiopia, 28 wa Somalia, wanne akiwemo mwanamke mmoja ambao tumewafikisha na kuwakabidhi polisi kwa ajili ya hatua zaidi,” alisema.

Awali, akizungumza kuhusiana na tukio hilo, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Tanga, Blasius Chatanda, aliwapongeza askari wa hifadhi hiyo kwa kazi nzuri ya kushirikiana na polisi wa Pangani.

 

Hata hivyo, amesema  hivi sasa wametangaza vita mpya kwa mawakala wanaojishughulisha na usafirishaji wa wahamiaji haramu mkoani Tanga na kwamba hawatasalimika watasakwa popote  nchi kavu, majini na kufikishwa mahakamani.

Leave A Reply