The House of Favourite Newspapers

Waingereza Wamuita Samatta Premier

BABA mzazi wa mshambuliaji wa kimataifa wa Tanzania, Mbwana Samatta, Mzee Ally Samatta, ameweka wazi kuwa majarida makubwa ya nchini Uingereza yameanza kumpigia chapuo mtoto wake kwenda kucheza Ligi Kuu ya England ‘Premier League’ kutokana na uwezo mkubwa anauonyesha kwa sasa.

 

Samatta anayekipiga kwenye Klabu ya KRC Genk inayoshiriki Ligi Kuu ya Ubelgiji kwa sasa amekuwa hashikiki katika ligi ya nchi hiyo, maarufu kama Jupiler League kutokana na kuongoza katika orodha ya wafungaji kufuatia kuwa na mabao kumi.

 

Mshambuliaji huyo amejiunga na Genk katika usajili wa dirisha dogo msimu wa 2016/17 akitokea TP Mazembe, amekuwa akihusishwa mara kadhaa kutakiwa na klabu kubwa za England kama West Ham na Everton na dau lake kwa sasa ni Sh Bil 10.6.

 

Akizungumza na Championi Jumamosi, Mzee Samatta alisema kuwa, kufanya vizuri kwa mtoto wake kunatokana na kufuata nyayo zake wakati anacheza soka lakini jambo la kuvutia zaidi kwake kufuatia kuwepo kwa taarifa za kupigiwa debe kucheza Premier.

 

 “Naona kama anafuata nyayo zangu wakati nacheza soka miaka ya nyuma maana yeye kwa sasa ndiyo anaongoza kwa kufunga mabao mengi kwa wachezaji wanaocheza Ulaya, kwangu ni faraja kubwa na nimekuwa nikimuombea aendelee kufanya vyema kama ilivyokuwa TP Mazembe kwa kuweza kuifikisha mbali.

 

“Lakini leo asubuhi (jana) kuna jarida moja la Uingereza limeandika kwamba Samatta sasa anastahili kucheza Ligi Kuu ya England kutokana na uwezo mkubwa anaouonyesha kwenye timu yake kwa kufunga mabao muhimu kitu ambacho naona kwake kitakuwa kizuri maana kuna West Ham, Everton ambao wanamhitaji ingawa hata Leicester City kabla ya kupata msiba walifanya hivyo,” alisema Mzee Samatta.

Ibrahim Mussa, Dar es Salaam

ZAHERA Awachana SIMBA Kiaina/ Awapa Kauli za Kishujaa

Comments are closed.