The House of Favourite Newspapers

WAJANE WACHARUKA TUNATAKA MAITI ZA WAUME ZETU!

0
WAJANE WACHARUKA
Ni simanzi na masikito.

WANAWAKE ambao waume zao walitekwa kwenye matukio ya mauaji yaliyokuwa yakiendelea maeneo ya Mkuranga, Kibiti na Rufiji mkoani Pwani kimafia, wameangua vilio kufuatia kutoonekana kwa waume zao na kudai hata kama wamekufa, basi wapewe maiti zao.

Wakizungumza na Uwazi wakiwa nyumbani kwao kwa nyakati tofauti, akina mama hao waliomba kama kuna mahali wanashikiliwa, waachiwe kwa vile wanaishi katika hali ngumu ya kimaisha na kujiona kama wajane.

IGP Sirro.

Jumapili iliyopita, Uwazi lilifika nyumbani kwa Mwenyekiti wa Kitongoji cha Ikwiriri, Kazi Bakari Mtoteke ambaye alitekwa na watu wasiofahamika Juni 7, mwaka huu na mpaka leo haijulikani alipo wala kama ni mzima au mfu. Mke wa kiongozi huyo, aliyejitambulisha kwa jina la Fatuma Athuman Binga, alisema amehangaika sana ili kujua mumewe alipo bila mafanikio, hivyo wanajipanga kumuona IGP Simon Sirro au rais.

ALITEKWA NA WALIOVAA KININJA

Alisema mumewe alitekwa na watu walioficha sura zao kwa vitambaa kama maninja na kabla ya kuondoka naye, kulitokea purukushani kali, hilo linatia wasiwasi, ni kina nani wale? . “Alichofanyiwa mume wangu ni pigo kwa familia, watoto wake wanamlilia kila siku. Siku hiyo ya tukio, majira ya saa mbili kasoro usiku, mume wangu baada ya kumaliza kufuturu aliniaga anakwenda msikitini kuswali.

“Baada ya dakika kama tano tangu alipotoka nikasikia watu wakiongea nje ya nyumba, nikajua huenda mume wangu alikuwa bado hajaenda msikitini labda alikuwa akiongea nao.

“Wakati nikitafakari nikashtukia mmoja amesukuma mlango na kuingia ndani na wenzake wanne nao wakafuatia, nilishtuka sana nilipowaona wamevaa soksi nyeusi usoni kama maninja, nikajua tumeshavamiwa na wauaji,” alisema mama Binga.

Alifafanua kuwa watu hao walimtaka mumewe hivyo walimtisha na kumuamuru ampigie simu ili aje na alifanya hivyo baada ya kutishiwa bastola.

WAJANE WACHARUKA
Mmoja wa marehemu hao.

“Ukweli sikuwa na jinsi zaidi ya kuwaeleza ukweli kuwa mume wangu alikuwa msikitini. Wakati nikiendelea kuongea nao huku nimechanganyikiwa, simu yangu iliyokuwa pembeni iliingia meseji ambapo wakashtuka na mmoja wao akasema kumbe una simu eeh, hebu mpigie mumeo mwambie kuna wageni nyumbani aje haraka.

“Wakaniwekea bastola puani, wakaniambia watapasua kichwa changu, kama nafanya mchezo, ikabidi nimpigie, kweli alikuja haraka wakati huo mmoja wao alitoka nje na kujibanza sehemu fulani, mume wangu alipokuja aliingia ndani moja kwa moja ambapo ghafla walimdaka na kuanza kumpiga.

“Hapo ilitokea purukushani kwa kuwa hata yeye alijua saa yake ya kufa imefika, hivyo alijaribu kutetea uhai wake lakini hata hivyo, kwa kuwa watu hao walikuwa wengi na wenye silaha walifanikiwa kumdhibiti na kumchukua, mimi waliniambia nilale kifudifudi, nisiangalie wanachomfanyia mume wangu ambapo walitumia muda huo kuondoka naye.

 

WAJANE WACHARUKA
Mmoja wa marehemu hao enzi za uhai wake.

ALIPOULIZWA KUHUSU POLISI WALICHOKISEMA

Alipoulizwa kama polisi wanasemaje, alisema alikwenda Kituo cha Polisi cha Ikwiriri kutoa taarifa hiyo ambapo walifungua jalada la uchunguzi wa tukio hilo na kumuahidi kumtafuta mume wake lakini hakupata jibu lolote hadi sasa.

“Mpaka sasa sijui kama mume wangu yuko hai au amekufa lakini naomba kwa Mungu, mume wangu awe hai maana ameniachia mzigo wa watoto wanne wanaohitaji kuendelezwa kimasomo na mimi sina uwezo wa kuwalea peke yangu. Lakini kama amekufa, basi tunaomba mwili wake ili tumzike. Namuomba Mkuu wa Jeshi la Polisi, Simon Sirro anisaidie kufanikisha kupatikana kwa mume wangu akiwa hai au
hata kama ni maiti.”

AMEONA MAITI NYINGI

“Siku hizi kila ninaposikia kuna maiti imeokotwa sehemu, nakimbia kwenda kuangalia, maana huenda akawa ni mume wangu. Hata niliposikia kuhusu zile maiti 15 zilizokutwa kwenye viroba baharini, nilikwenda kuziangalia lakini ya mume wangu haikuwepo,” alisema huku akifuta machozi, kitendo kilichofanya mmoja wa watoto wake nao kulia kwa kwikwi.

MKE WA DAKTARI ANENA

Mke mwingine wa daktari wa tiba mbadala, Mubaraka Daruweshi ‘Muba’ aitwaye Fatuma ambaye alitekwa nyumbani kwake, Agosti 13, mwaka huu, Temeke jijini Dar, alisema amekuwa katika wakati mgumu hadi sasa, kwani hakuna taarifa zozote kuhusu alipo mumewe huyo.

“Kila siku nakwenda Kituo cha Polisi Chang’ombe kuulizia kuhusu mume wangu, lakini wanasema bado wanaendelea kufuatilia suala hilo, lakini hawana majibu kama amepatikana au la.

“Mume wangu kachukuliwa chini ya mtutu wa bunduki, familia inateseka. Sijui hata niseme nini, lakini nilikuwa ninaomba kama kuna sehemu mume wangu amewekwa, niambiwe, kama amekufa basi nipewe mwili wake, maana hivi ninateseka sana kisaikolojia na kiuchumi,” alisema mwanamke huyo.

STORI: RICHARD BUKOS NA ISSA MNALLY| UWAZI

 

Bomoabomoa Yapitia Kanisa la Nabii Bilionea Sinza

Leave A Reply