Wajasiriamali Wahimizwa Kushiriki Shinda Nyumba
Na Chande Abdallah
WANAWAKE wajasiriamali jijini Dar wamehimizwa kushiriki kwa wingi Bahati Nasibu ya Shinda Nyumba inayoendeshwa na Kampuni ya Global Publishers kupitia magazeti yake.
Hayo yamezungumzwa na Mhariri wa Gazeti la Uwazi, Elvan Stambuli katika semina ya ujasiriamali iliyofanyika Machi 1, mwaka huu katika Ukumbi wa Kamanyola, Sinza jijini Dar ambapo akinamama wajasiriamali walihudhuria kujifunza njia mbalimbali za kujikwamua kiuchumi na kuwa tegemezi kwa jamii kupitia kauli mbiu ya Mwanamke ni Familia.
Stambuli alisema moja kati ya njia inayoweza kumkwamua mwanamke mjasiriamali kutoka kwenye umaskini ni pamoja na kushiriki michezo mbalimbali ya bahati nasibu ikiwemo hiyo ya Shinda Nyumba.
“Mnaweza kushiriki na kushinda, mifano hai ipo, na ningependa hata nyinyi mshiriki Bahati Nasibu ya Shinda Nyumba kwani mnaweza kushinda na kupiga hatua kimaisha,” alisema Stambuli.
Semina hiyo iliyodhaminiwa na Global Publishers wachapishaji wa magazeti ya Amani, Risasi, Championi, Ijumaa, Uwazi na Ijumaa Wikienda kupitia shindano lake la Bahati Nasibu ya Shinda Nyumba, iliratibiwa na shirika la masuala ya maendeleo ya kijamii, Community Development Forum (CDF) na kuhudhuriwa na wazungumzaji kibao wakiwemo; Dk. Elie, Maznat, Harris Kapiga na wengine wengi.