The House of Favourite Newspapers

WAJAWAZITO WAPATATISHIO JIPYA!

UPEPO wa maisha ya Maria na Consolata Mwakikuti, pacha walioungana ambao walifariki dunia hivi karibuni na kuzikwa mkoani Iringa baada ya kuishi kwa miaka 21 duniani bado unavuma kwa kasi huku ukionekana kuwaacha wajawazito kwenye tishio jipya la kuhisi nao wanaweza kupata watoto walioungana kama wao, Uwazi habari ambayo iyakuacha na fundisho kubwa.

Tangu Maria na Consolata warudi mavumbini walikotokea yamesemwa mengi, lakini Uwazi limechimba na kubaini kuwa pacha hao wameacha hofu kwa wajawazito.

Kinachowatia hofu watu wengi waliofuatilia maisha ya pacha hao hadi kifo chao ni namna walivyozaliwa, gharama za malezi yao na mtazamo wa kitabibu unaoonesha kuwa pacha wa aina hiyo ni vigumu kuishi, mambo ambayo kila mtu na hasa akina mama wajawazito wanaomba Mungu kila siku yasiwakute.

“Hawa pacha wameacha funzo, naogopa kupata jaribu kubwa la aina yao; Mungu anisaidie nijifungue mtoto kamili,” alisema Joyce Emmanuel, mama mjamzito mkazi wa Makongo Juu, mkoani Dar alipoongea na Uwazi.

UWAZI NA DAKTARI

UWAZI: Dokta Chale (Godfrey anayehudumu katika Hospitali ya Temeke alipoongea na Uwazi kwa njia ya simu), habari za kazi?

DK CHALE: Njema za kwako?

UWAZI: Unaongea na mwandishi wa Uwazi; Dk tangu pacha walioungana Maria na Consolata wamefariki kumekuwa na mijadala mingi mitaani na kwenye mitandao ya kijamii, lakini mwisho wa siku watu wengi na hasa wajawazito wamekuwa wakihofu sana kujifungua watoto wa aina hiyo unaweza kuliongelea hili kitalaam?

DK CHALE: Unachosema ni kweli hata sisi katika kazi zetu za kitabibu wanawake wengi sasa wamekuwa wakipenda kupima kutaka kujua kama watoto wanaotarajia kuwazaa wako salama.

UWAZI: Unadhani ni kwa nini?

DK CHALE: Ndio hiyo hofu uliyosema ambayo imechangiwa na watu wengi kuwaona Maria na Consolata, lakini duniani si jambo jipya.

UWAZI: Ni kweli duniani si jambo jipya, lakini limekua vipi mwaka huu hapa kwetu kiasi cha kuwa tishio?

DK CHALE: Ukaribu wa tukio una maana zaidi, nadhani unajua, kumuona mtu na kusimuliwa kuna utofauti. Watanzania wengi wamewaona Maria na Consolata wamewasoma sana kwenye vyombo vya habari ndiyo maana wamekuwa na uelewa mkubwa juu ya pacha walioungana.

UWAZI: Nini kifanyike.

DK CHALE: Hakuna haja ya kuogopa kwa wajawazito, akina mama na jamii kwa ujumla juu ya jambo hili kikubwa ni kuzingatia kanuni za afya ili kukinga madhara yasimpate mtoto anayetarajiwa kuzaliwa.

NI ZIPI HIZO KANUNI ZA AFYA?

Dk Godfrey Chale alisema mama mjamzito hutakiwa kutumia dawa za ‘folic acid’ kabla na baada ya ujauzito ili kuepuka kujifungua mtoto mwenye tatizo la kichwa kikubwa (Hydrocephalus) na mgongo wazi (spina bifida).

“Kama una mpango wa kupata mtoto siku za usoni unashauriwa kutumia virutubisho vya aina ‘folic acid’ hata kama unayo afya ya kutosha na unapata mlo kamili.

“Na mara baada ya kupata ujauzito endelea kutumia kirutubishi hiki kwa muda wa wiki 12 za ujauzito,” alishauri Dk. Chale. Alisema dawa hizo huepusha mama kupata mtoto mwenye tundu la uti wa mgongo, kichwa kikubwa na midomo iliyopasuka.

“Vipo vyakula vingi ambavyo vina mchanganyiko wa Folic Acid mfano spinach, sprouts, broccoli, maharagwe (green beans), na viazi, juisi ya machungwa na maparachichi,” alisema.

Dk Chale alisema iwapo mama aliwahi kupata mtoto mwenye tundu kwenye uti wa mgondo, au anatumia dawa za kifafa, kisukari au seli mundu (sickle cell anemia) ni vyema akatumia dozi ya juu ya folic acid.

TAKWIMU

Aliongeza kuwa inakadiriwa watoto 200,000 huzaliwa na matatizo haya kila mwaka duniani na zipo sababu mbalimbali zinazosababisha matatizo haya. “Kwa asilimia 60 hadi 70 hakuna sababu iliyothibitishwa wengi wanasema ni sababu za urithi na vinasaba. Sababu nyingine ni vimelea maradhi, dawa au sumu,” alisema.

Dk. Chale alibainisha kuwa baadhi ya dawa ambazo kitaalamu huitwa ‘teratogenic drug’ ambazo zimekuwa mwiba mkubwa kwa wajawazito na kusababisha wengi wao kujikuta wanaathiri watoto wao wakiwa tumboni, dawa hizi huweza kupita katika kondo la nyuma (placenta) na kumuathiri mtoto aliye tumboni.

“Ili kumaliza tatizo hili wanawake wote wajawazito wanashauriwa kumwona daktari kabla ya kutumia dawa ya aina yoyote ile, hata hivyo, ni vema wakawa wawazi ila wengi wao wamekuwa wasiri kueleza hali zao wanapokuwa kwa daktari, baadaye anaandikiwa dawa zenye madhara kwa ujauzito lakini daktari akijulishwa atajua dawa ipi ni salama kwa mjamzito,” alishauri.

Alizitaja dawa zinazoweza kusababisha matatizo hayo na namna zinavyoweza kuleta madhara ni zile za antibayotiki kama tetracycline na klorofeniko. “Kitaalamu madawa haya hayatakiwi kutumiwa na mama mjamzito kwani kwa kufanya hivyo katika kipindi cha awali husababisha mifupa na meno kuwa na matatizo,” alisema Dk Chale.

DAWA NYINGINE

Alizitaja dawa nyingine kuwa ni metronidazole (flagilly) ambapo alisema kama mama atazidisha dozi inaweza kuleta madhara makubwa. Alisema dawa ya phenytoin inayotumika kutibu magonjwa ya akili-mfumo wa fahamu kama kifafa huweza kuleta madhara katika ubongo, seli za nyuma ya koo na matatizo ya maumbile ya uso.

DAWA ZA SARATANI

Dawa nyingi za kutibu saratani zina kemikali hivyo nazo huingia na kuzuia ukuaji wa seli. Alisema kuzidisha dozi ya kirutubisho kiitwacho vitamin A-retinol husababisha watoto kuzaliwa na maumbile yasiyo ya kawaida. Kama vile mdomo sungura (cleft) na uti wa mgongo kuwa wazi, au tumbo kuwa bila ngozi na matatizo sehemu za uso.

“Hizi ni dawa za vitamin A lakini hutakiwa kutumika kwa umakini mkubwa kwani zikizidi husababisha matatizo kwa mtoto aliye tumboni,” alisema Dk Chale.

UWAZI NA KUMBUKUMBU

Septemba 15, mwaka huu katika kitongoji cha Changanyikeni kijiji cha Gissambalang, Wilaya ya Hanang’, Mkoa wa Manyara mwanamke mmoja aliyetambuliwa kwa jina la Mwanjaa Masagati alijifungua mtoto wa kike mwenye vichwa viwili vilivyokuwa na uso wa mbele na nyuma.

Hata hivyo, mtoto huyo alifariki dunia baada ya kuishi kwa muda wa saa moja. Katika tukio jingine, pacha wa kiume (Elikana na Eliud) walizaliwa Kata ya Uyole jijini Mbeya wakiwa wameungana sehemu ya kiunoni.

Pili Hija (24), mkazi wa Jang’ombe, Zanzibar alijifungua watoto walioungana, huku mmoja akiwa ni kiwiliwili. Pili alijifungua pacha hao Agosti 18, 2013, nyumbani kwake na baadaye kupelekwa kwenye Hospitali ya Mnazi Mmoja, Zanzibar baada ya watoto kuonekana si wa kawaida.

Pacha hao walifanyiwa upasuaji Agosti 29, 2013 katika Hospitali ya Taifa Muhimbili Kitengo cha Tiba ya Mifupa (Moi) chini ya Daktari Bingwa wa Upasuaji wa Watoto, Dk Zaituni Bokhary.

Mtoto aliyebaki ni yule aliyezaliwa akiwa na kichwa, ilibidi kumuondoa asiye na kichwa kwa sababu asingeweza kuwa binadamu kamili.

HUYU HAPA DAKTARI BINGWA MUHIMBILI

Dk Cyriel Massawe, Daktari Bingwa wa Magonjwa ya Wanawake na Afya ya Uzazi wa Hospitali ya Taifa ya Muhimbili amesema mwanamke mjamzito hashauriwi kunywa dawa ya aina yoyote ile kama hajapata ushauri kutoka kwa daktari kwa kuwa baadhi ya dawa huainishwa kwamba huwenda inaweza kuchangia kuvuruga uumbaji siku za mwanzo za ujauzito.

Alisema: “Hali hiyo husababisha seli kushindwa kugawanyika vizuri kila moja kwenda kufanya kazi ile inayokusudiwa katika uumbaji wa mtoto hapo ndipo tatizo huanza kutokea.”

ATOA MFANO

Anatoa mfano kuwa tatizo kubwa linalowapata watoto walioungana pia linaweza kusababishwa na kutogawanyika vizuri kwa seli wakati wa utungwaji wa pacha.

“Mfano mzuri ni watoto walioungana, hawa ni wale wa mfuko mmoja. Yai moja linapogawanyika mara mbili ni nadra kutokea kosa, lakini katika uumbaji seli zikishindwa kugawanyika vizuri na kufanya uumbaji uliotimilifu hapo pacha wataungana matumbo, migongo, vichwa na sehemu zingine za mwili au mmoja asitimie kama ilivyotokea hivi karibuni,” alisema.

Aliongeza kuwa iwapo mama hakutumia vidonge au dawa za aina yoyote basi yawezekana tatizo ni la kiasili na hali hii hutokea katika hatua za mwanzo wa ujauzito na hata mwanamke akienda hospitali huambiwa kwamba atajifungua watoto pacha lakini hali huwa ndivyo sivyo.

“Dawa zinazoleta madhara si zile zinazotumika mara kwa mara, lakini kwa bahati mbaya wapo wanawake wanajigundua kwamba wamebeba ujauzito na hawa wanajikuta wakitumia dawa hizo ambazo mwishowe zinawaletea madhara,” alisema Dk Masawe.

WANAUME NAO WANENA

Baadhi ya wanaume walizungumza na Uwazi, walionesha hofu ya kubeba jukumu la malezi pale pacha walioungana wanapozaliwa.

“Serikali itoe elimu ya kutosha kwa jamii, ni mzigo mzito sana kuhudumia watoto wa aina hii, kibaya zaidi nyuma ya ughali wa huduma zao pacha hao ni nadra kuishi,” alisema Shukuru Juma alipochangia maoni yake katika mtandao wa kijamii wa Facebook

Aidha, Uwazi katika kufuatilia mijadala mbalimbali kuhusu pacha walioungana lilibaini kuwa pamoja na kifo chao Maria na Consolata wameacha funzo kwa wazazi na walezi walio wengi kuonesha upendo kwa walemavu kwa sababu uhai ni matokeo ya Mungu.

“Wengi waliamini Maria na Consolata wangekufa lakini hawakufa, waliowatenga wameona maisha yao kwa zaidi ya miaka 20, wameacha nyayo za upendo na uvumilivu, leo kila mtu anawaongelea, ni bahati kwao ambayo ni vigumu kupatikana kwa wengi, Mungu awalaze peponi,” alisema msichana mmoja aliyejitambulisha kwa jina moja la Rose.

TUJIKUMBUSHE

Maria na Consolata ni pacha walioungana waliozaliwa mwaka 1997 katika Wilaya ya Makete, mkoani Njombe, walifariki dunia Juni 2, mwaka huu na kuzikwa Juni 6, eneo la Tosamanganga, nje kidogo ya mji wa Iringa.

STORI: MWANDISHI WETU, UWAZI

Comments are closed.