Wajue Nyota wa Afrika Walioshiriki Albamu ya Beyonce

MWANAMUZIKI maarufu wa Marekani, Beyonce,  amefichua nyimbo zilizomo kwenye albamu yake mpya itakayoambatana na filamu mpya ya The Lion King ambayo imejumuisha wasanii nyota wa muziki kutoka Afrika.

Albamu hiyo imeshirikisha wasanii wa Nigeria Tiwa Savage na Mr Eazi katika wimbo wa ‘Keys to the Kingdom’, wengine ni Tekno na Yemi Alade katika kibao ‘Don’t Jealous Me’.

Burna Boy ana kibao cha kipekee au solo cha  ‘Ja Ara E’, huku msanii wa Cameroon, Salatiel, akionekana akiimba na Beyonce na Pharrell Williams katika kibao cha  ‘Water’.

Wasanii wengine wa Afrika ni pamoja na Wizkid wa Nigeria, Shatta Wale wa Ghana, Busiswa na Moonchild Sanelly kutoka Afrika Kusini. Alipotangaza mpango huo kwa mara aya kwanza wiki iliyopita, Beyonce alisema:  “Ilikuwa ni muhimu kuwa muziki usiimbwe na wasanii nyota na wenye vipaji bali uandaliwe na waandaaji wa Afrika.

Ubora na moyo (mapenzi) vilikuwa vitu muhimu kwangu.

“Ni mchanganyiko wa kila kitu, si sauti moja tu. Kuna ushawishi kutoka kila kona, kutoka kwenye R&B, hip-hop na Afro Beat.”

Albamu hiyo kwa jina la ‘The Lion King: The Gift’, inatarajiwa kuzinduliwa Ijumaa hii.

Inajumuisha pia vibao vya ushirikiano na wasanii wa Marekani kama Kendrick Lamar, Pharrell Williams, Childish Gambino, na binti yake Beyonce, Blue Ivy,  miongoni mwa wengine.  Ni kibao tofauti kilichotumika kuisindikiza filamu hiyo ya The Lion King, Spirit, chenye mistari ya Kiswahili.  Hata hivyo,  kimejumuishwa pia kwenye albamu hiyo.

Wiki iliyopita, Beyonce aliachia kibao hicho kipya chenye maneno ya Kiswahili ya “Uishi kwa muda mrefu mfalme”  ambamo sauti nyembamba inaimba kisha sauti nzito inaitika “Uishi”.  Kionjo hiko kinajirudia mara mbili na kisha wimbo kuendelea kwa Kingereza.

Filamu hiyo mpya ya Lion King imetengenezwa na kampuni kubwa ya Disney nchini Marekani.

 


Loading...

Toa comment