WAJUE SAMAKI WANAOWEZA KUTIBU UGONJWA WA MOYO

 

Samaki aina ya Tetra

Samaki anayeweza kuurekebisha moyo wake huenda ndiyo suluhu ya matibabu kwa watu wenye matatizo ya moyo, kwa mujibu wa utafiti. Wanasayansi wanaowachunguza samaki wa Tetra kutoka nchini Mexico wamegundua maeneo matatu ya mfumo wa samaki huyo uliochangia uwezo wake kuunda upya tishu za ndani ya moyo.

Jeni moja imeonekana kuwa na jukumu kuu katika mfumo huo. Watafiti wanatumai utafiti wao siku moja utafanikisha uponyaji wa misuli ya ndani ya moyo kwa wagonjwa ambao wamewahi kupata mshtuko wa moyo. Maelfu ya watu huishi na matatizo ya moyo baada ya kupata mshtuko wa moyo. Kwa sababu binadamu hawawezi kuunda upya msuli ulioharibika, au kujeruhiwa kwa moyo, na mara nyingi watu hulazimika kuishi na hali hiyo au kuishia kufanyiwa upandikizaji wa moyo

Kwa utaifiti huu, uliofadhiliwa na taasisi ya British Heart Foundation, Dkt Mathilda Mommersteeg na kundi lake la wataalamu katika chuo kikuu cha Oxford walichunguza aina mbili za samaki hao aina ya Mexican tetra fish – wanaoishi mitoni, walio na uwezo wa kujiponya, na wengine wanaoishi katika mapango ambao hawana uwezo huo.

Samaki hao wa pangoni ambao kwa wakati mmoja walikuwa wakiishi katika mito kaskazini mwa Mexico walisombwa hadi katika mapango miaka milioni 1.5 nyuma na waligeuka, na kupoteza uwezo wa kuona na rangi ya ngozi kutokana na kuishi kwenye giza. Kwa kulinganisha aina hizo mbili za samaki, watafiti wamegundua jeni mbili – lrrc10 na caveolin – zilidhihirika zaidi katika samaki wanaoishi katika mito, baada ya kupata majeraha ya moyo.

Baada ya kuligundua hili, waliifungia jeni ya lrrc10 ndani ya viumbe kadhaa vilivyo na uwezo wa kujitibu, kwa zebrafish. Baada ya kufungwa na kushindwa kufanya kazi vizuri kwa jeni hiyo, samaki huyo wa zebrafish alishindwa kujirekebisha moyo. Jeraha la tishu linazuia msuli wa moyo kupiga vizuri na kupunguza uwezo wa moyo kusukuma damu mwilini. Jeni zote mbili zipo ndani ya mwili wa binaadamu.

Wahariri wa utafiti huo wanasema unadhihirisha siku moja itawezekana kuunda upya sehemu za moyo zilizoharibika ndani ya binaadamu kwa kukarabati namna jeni hizi zinavyofanya kazi. Hili linawezekana kwa dawa au mbinu za ki elektroniki katika kukarabati jeni ambapo vina saba au DNA inageuzwa, kufutwa au kabdilishwa kwa kutumia vifaa kama Crispr-Cas9.

“Ni hatua za kwanza lakini tuna furaha kubwa kuhusu samaki hawa na uwezekano wa kubadili maisha ya watu wenye matatizo ya moyo” amesema Dkt Mathilda. Hatahivyo ameongeza kwamba kazi zaidi inahitajika kutafuta jeni nyingine muhimu ambazo huenda zikatumika katika kusahihisha matatizo ya moyo. Utafiti huu umechapishwa katika jarida la Cell Reports.

Toa comment