TAASISI ya Ukaguzi wa ndani Tanzania (IIA) imeanza kuanzimisha mwezi wa wakaguzi wa ndani ulimwenguni ambao huadhimishwa kila ifikapo Mwezi Mei ya kila mwaka. Akizungumza leo na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam, Rais wa IIA Tanzania, CPA Zelia Njeza amesema katika mwezi huu wa maadhimisho taasisi yao imepanga kutembelea taasisi mbalimbali wadau na kufanya shughuli anuai zinazo lenga kuboresha na kuitangaza tasnia ya ukaguzi wa ndani.
CPA Njeza amewaeleza waandishi wa habari kuwa tayari taasisi yake imeichambua taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) na kuainisha madhaifu ambayo yameoneshwa katika taarifa hiyo na watatumia mwezi huu wa maadhimisho kuwanoa wakaguzi wa ndani ili kupunguza dosari ambazo zinajitokeza katika taarifa za CAG.
Zalia alisema kikawaida taasisi yao baada ya kuipitia na kuchambua dosari hizo huitumia katika kuandaa mada na semina kwa wakaguzi wa ndani ambao ni wanachama wao pamoja na wadau ili kuboresha zaidi shughuli za kikaguzi.
Alibainisha kuwa mkaguzi wa ndani ni kioo ndani ya taasisi ambacho kimelenga kusaidia taasisi husika katika shughuli zao za kila siku ili iweze kutimiza malengo yake.
Amesema miongoni mwa shughuli wanazozifanya katika maadhimisho ya mwze wa wakaguzi wa ndani ni pamoja na kuwashindanisha wakaguzi wa ndani ili kuboresha shughuli zao na kusherekea mwezi huu.
“…Tumeandaa mashindano ya wakaguzi na katika shindano hili IIA itatoa zawadi kwa wakaguzi watakaofanya vizuri katika mashindano hayo, tunaomba pia wadau wetu katika kipindi hiki watoe maoni kwa vigezo vipya vya sifa za ukaguzi ili kuboresha zaidi baada ya maboresho tulioyafanya kwenye eneo la vigezo vya ukaguzi,” aliongeza CPA Njeza.
Aidha rais huyo wa IIA ameishukuru Serikali kwa ushirikiano ambao wamekuwa wakiutoa kwa taasisi ya IIA, kwenye eneo la utekelezaji wa shughuli zetu, tunafanya kazi bila kupata vikwazo vyovyote.
Kwa upande wake, Gavana wa IIA-Tanzania, Bw. George Binde alisema taasisi hiyo inaungana na wakaguzi wote ulimwenguni kuadhimisha mwezi wa wakaguzi wa ndani kwa kueleza umuhimu wa shughuli za ukaguzi wa ndani.
Alisema ndani ya mwezi huu, IIA imeandaa shughuli mbalimbali kusherekea mwezi wa ukaguzi ikiwemo, kutembelea katika vyuo vya elimu ya juu vya ukaguzi Tanzania, lengo kubwa likiwa nikuhamasisha wanafunzi umuhimu wa tasnia ya ukaguzi na kuwajengea utayari na moyo wa kupenda kufanya kazi ya ukaguzi wa ndani.
Aidha, Bw. Binde alisema katika vyuo hivyo, kuna baadhi ya vyama vitazinduliwa yote ikiwa ni kuweza kuwaleta karibu zaidi wanatasnia hiyo hata katika ngazi za vyuo, kurahisisha uchaguzi wa masomo kwa wanavyuo wanaoitaji kuja kufanya kazi za shughuli za ukaguzi wa ndani hapo baadaye.
Alisema mbali na mafanikio yani kufikisha ujumbe mahususi kwa wadau wa shughuli za ukaguazi katika, mazingira ya kazi za wakaguzi bado ni changamoto hivyo kutaka kufanyika kwa juhudi za kuyaboresha zaidi ili waweze kufanya kazi yao vizuri.