Wakala wa Kagere Amkomalia Kocha wa Simba, Anusa Hujuma

PATRICK Gakumba, wakala wa mshambuliaji namba moja ndani ya Simba, Meddie Kagere, amesema kuwa amepokea ofa nyingi kutoka timu tofauti zikitaka saini ya mchezaji huyo.

 

Kwa sasa Kagere amejenga ushikaji mkubwa na benchi kwa msimu wa 2020/21 akiwa hajamaliza dakika 90 ndani ya mechi mbili za ligi ambazo Simba imecheza mpaka sasa.

 

Mechi hizo ni dhidi ya Ihefu FC ambapo Simba ilishinda mabao 2-1 na mchezo wa pili ilikuwa mbele ya Mtibwa Sugar wakati Simba ikilazimishwa sare ya kufungana bao 1-1, Uwanja wa Jamhuri.

 

Gakumba ameyasema hayo ikiwa tayari mchezaji wake Meddie Kagere akikosa nafasi ya kuanza katika kikosi cha kwanza cha kocha Sven Vandenbroek ambaye amekuwa akimwamini zaidi  nahodha John Bocco.

 

”Uwezo wa Meddie Kagere uko palepale na mashabiki wanajua na muda utaongea, mwalimu asiyempa nafasi na janjajanja zinazofanywa ili wampoteze kwenye ramani tunajua. ‘Haya mambo yalishawatokea wachezaji wakubwa kama Samuel Etoo, Demba Ba, lakini kila mmoja alijua kilichofuatia kwa wale waliokuwa wakiwafanyia mizengwe.

“Nimepokea ofa nyingi sana wanataka kusaini mkataba wa awali lakini sisi tunaiheshimu Simba na inampa stahiki zake zote. Kocha anayemweka benchi Kagere aende kuuliza Kenya kilichomkuta kocha wa zamani wa Gor Mahia  alipojaribu kumnyima nafasi mshambuliaji huyo,” alisema Gakumba.

 

Gakumba ameongeza: “Kagere bado ana mkataba wa mwaka mmoja na Simba na utaisha mwakani mwezi wa tano. Mpaka sasa tuna ofa nyingi ambazo zinamtaka mapema ili tusaini mkataba wa awali lakini nawaheshimu Simba na wanakidhi mahitaji yake ya yote tulivokubaliana.”

 

Kagere ndani ya misimu miwili akiwa Simba amefunga jumla ya mabao 45. Alifunga mabao 23 msimu wa 2018/19 na alifunga mabao 22 msimu wa 2019/20.
Toa comment