WAKATI AKIZIKWA LEO MENGI AACHA FUNZO KUBWA

DAR ES SALAAM: “Jef hivi umewahi kufika katika msiba? Je, umewahi kumuona tajiri akichimba kaburi?” Tafakari kauli hii na Amani linalokupakulia habari hii iliyojaa funzo kubwa.

Nukuu ya maneno hayo mazito ilitolewa mwishoni mwa mwaka jana na mfanyabiashara maarufu nchini marehemu Reginald Mengi ambaye wiki hii imekuwa ya maziko yake, wakati akifanya mazugumzo na mwandishi wa kituo kimoja cha televisheni cha nchini Kenya aitwaye Jef Koinange.

 

Aidha, mbali na marehemu Mengi kumhoji Jef swali hilo aliendelea kumwambia:“Mwisho wa siku ni masikini ndiyo wanaochimba kaburi, matajiri mara nyingi hawapendi hata kuonyesha hisia zao.”

FUNZO KUBWA LA MENGI

Pengine wakati akisema maneno hayo marehemu Mengi hakujua kuwa Alhamisi hii, mwili wake utapumzishwa mavumbini lakini alichomwambia Jef ndicho kilichomtokea.

Pamoja na utajiri mkubwa aliouacha mfanyabiashara huyo na kuishi karibu na matajiri wenzake wakubwa ndani na nje ya nchi, lakini ukweli aliouishi ndiyo uliomtokea kwani waliochimba kaburi lake hawakuwa matajiri wenzake bali ni masikini kama wanavyoonekana kwenye picha ukurasa wa mbele.

Funzo hili aliloliacha Mengi linapashwa kuwa somo kwa matajiri wengine na wenye kujitukuza katika maisha haya kwamba waishi wakijua kuwa mali na heshima ya mtu ni vitu tofauti.Akionesha kukwepa kujitukuza na kuheshimu mapenzi ya Mungu kwa wanadamu wote, Mengi alimwambia mwandishi huyo hivi:

 

 

“Nawapenda watu masikini maana huko ndiko nilipotokea, mimi sijioni kama ni tajiri, bado najiona masikini kama wengine.“Naamini kwamba kila kitu nilichonacho kimetoka kwa Mwenyezi Mungu, kuna wakati watu wanajisahau na kufikiria kuwa yale waliyo nayo yametokana na nguvu au juhudi zao binafsi,” alisema Mengi.

MATAJIRI WANGAPI WANAWAPENDA MASIKINI?

Kutokana na maneno hayo ya marehemu Mengi yaliyomfanya aogope kujiona tajiri na kuwadharau masikini, swali la kujiuliza; ni matajiri wangapi wanaoishi maisha ya mfano wake?

Ikumbukwe kuwa, Mengi anatajwa kuacha utajiri wa shilingi 1.2 Trilioni ambao ni mkubwa pengine kuliko matajiri wengi ambao wanaishi kwa kujitenga na masikini ambao Mengi alisema ndiyo wachimba makaburi. Bila shaka hili ni funzo kubwa kwa binadamu wote bila kujali hali na matabaka yao kwamba katika maisha haya wote ni sawa kama Katiba ya nchi Ibara ya 12 (1) inavyosema.

MENGI ALIYAISHI ALIYOAMINI

Tofauti na watu wengi ambao wanaweza kusema wanawapenda masikini bila kuonesha kwa vitendo; katika uhai wake Mengi aliyaishi aliyosema kwa kuwa mstari wa mbele kuwasaidia masikini na watu wenye uhitaji. Karibu kila mwaka mfanyabiashara huyo alikuwa akikutana na watu masikini na wenye ulemavu na kushiriki nao chakula cha pamoja, kuwatia moyo na kuwasaidia kwa misaada mbalimbali.

MASIKITI WAMLILIA MENGI MITAANI

Katika kuthibitisha kuwa mfanyabiashara huyo (Mungu amrehemu) alipanda mbegu njema mioyoni mwa watu masikini, gari lililobeba mwili wake lilipokuwa likipita kwenye mitaa mbalimbali ya watu masikini jijini Dar kama Buguruni na Kigogo, mamia wa watu wenye maisha ya chini walijitokeza barabarani na kuangua vilio wakati msafara wake ukipita.

 

Huku mvua kubwa ikinyesha wanawake kwa wanaume, walemavu, watoto na wanafunzi walijipanga barabarani huku wakipunga mikono yao kama ishara ya kumuaga aliyewapenda.

WAZIRI MKUU ATHIBITISHA UPENDO WA MENGI

Wakati mbegu ya wema aliyoipanda Mengi ikionekana dhahiri kumea kwenye mioyo ya watu, Waziri Mkuu Mstaafu wa Awamu ya Pili, John Malecela alimwelezea Mengi kuwa mtu aliyeishi sawa na msemo wa mwanafalsafa mmoja wa Morocco usemao:

“Tutakapokuwa tumekufa na tumezikwa kwenye makaburi, msitutafute kwenye makaburi yaliyopakwa chokaa, ila mtutafute katika mioyo ya wale tuliowahudumia.” Hakika mioyo ya wale aliowahudumia Mengi ndiyo hao waliomlilia mchana na usiku na kumuelezea kuwa bila yeye pengine ingekuwa vigumu kuvuka vikwazo vya kimaisha vilivyowakabili.

PENGO LA MENGI NI KUBWA

Imezoeleka kusemwa kila mtu anapokufa kwamba “pego lake halitazibika” lakini wakati mwingine yamekuwa yakizibika hata kwa meno bandia; lakini unapomtaja Mengi ni kweli pengo lake halitazibika. Mengi amekuwa mwajiri wa Watanzania wengi kupitia makampuni mbalimbali aliyokuwa akiyamiliki yakiwemo yanayojishughulisha na masuala ya kihabari.

Aidha, Mengi wakati wa uhai wake amekuwa akijitolea kwa hali na mali kuwasadia walemavu, kusaidia na kukuza masuala ya michezo na kuinua vipaji vya watu likiwemo suala la kuwatia moyo watu wasikate tamaa katika kutafuta maisha yao. Mengi alifariki ghafla Dubai, Falme za Kiarabu, Mei 2, mwaka huu na maiti yake kusafirishwa kwa ndege hadi jijini Dar ambako uliagwa Mei 6 na kupelekwa mkoani Kilimanjaro kwa mazishi.


Loading...

Toa comment