The House of Favourite Newspapers

UNAPATA TABU SANA KWENYE MAPENZI? SOMA HAPA!

WAKATI MUNGU ni mwema, Jumapili nyingine tunakutana kwenye eneo letu la kupeana darasa la masuala ya uhusiano. Nafurahi kuona mkiendelea kunitumia jumbe mbalimbali kuonesha kwamba mambo tunayoyajadili hapa, yanaleta matokeo chanya kwenye maisha yenu ya uhusiano.

 

Wakati mwingine ni vizuri kujifunza kupitia maandishi. Unaweza kujiona upo sahihi kwenye uhusiano wako na mambo yanaenda kumbe kuna vitu unakosea bila mwenyewe kujua.

 

Unaishi kwenye ulimwengu wako, unajiona uko sahihi mwisho wa siku unaishia kufeli katika safari ya uhusiano. Nikirudi kwenye somo la leo kama linavyojieleza hapo juu, licha ya kuwa mpenzi au mchumba sahihi anapatikana kutokana na mambo mengi ikiwemo tabia na mengineyo lakini wakati mwingine huwa tunasema ni bahati kama si fursa.

 

Wengi sana wamekuwa wakikutana na bahati ya kupendwa na kujikuta wakicheza na muda. Amekutana kabisa na mtu ambaye ni sahihi maishani mwake lakini kutokana na sababu zake binafsi, anaamua tu kumpotezea yule mtu na kufanyafanya ‘blaablaa’.

 

Anajikuta akifanya mchezo wa mapenzi. Bado anatamani ale ujana, mathalan binti ana umri wa miaka 18, 19 hadi 25, umri ambao unamruhusu kabisa kuingia kwenye uhusiano ‘serious’ lakini yeye anapuuzia tu. Unakuta binti ana umri ambao unamruhusu kabisa kuanza kutengeneza maisha, anakutana na kijana ambaye anamhitaji lakini wapi bwana. Anataka kurukaruka na njia, anaona kuwa kwenye uhusiano serious ni kubanwa.

Watu wa aina hii wapo wengi. Si wanawake tu hata wanaume. Wanakataa kuingia kwenye uhusiano serious wakiamini muda bado upo. Hawataki kubanwabanwa. Wanataka kula ujana kwanza halafu mambo ya kuingia kwenye uhusiano wa kwenda kwenye ndoa ni baadaye sana.

 

Ndugu zangu, ni vyema sana kuishi huku ukiitafakari safari yako ya uhusiano. Jiwekee malengo na kuangalia sana suala la muda. Muda haukusubiri, unakwenda kasi sana hivyo ni vyema kuangalia bahati yako ipo wapi na uitendee haki. Umekutana na mtu ambaye unamuona ana tabia njema, ana kila sifa ya kuwa mwenza wako acha kupoteza muda. Acha kusema kwamba umri bado unakuruhusu maana baadaye utakuja kujuta kwa kuchelewa kuingia kwenye uhusiano serious.

 

Unaweza kuja kujuta na kuona uliichezea bahati maana uliwahi kukutana na mtu sahihi, mnyenyekevu, mpole, mkarimu, mcha Mungu na mwenye kila aina ya sifa halafu wakati huo unakuta hayupo tena. Utakuta tayari pengine ameshaingia kwenye uhusiano na mtu mwingine.

Unaweza kukuta wakati huo tayari mwenzako ameoa au kuolewa na mtu mwingine na wewe ukabaki kusema; ‘ningejua’. Kumbe mtu sahihi alikuja kwako tena kwa wakati sahihi lakini wewe ulikuwa bize na ujana.

 

Au pengine wakati huo ulikuwa na mtu ambaye pengine si sahihi sana lakini ulikuwa tu ukimng’ang’ania kwa sababu tu labda ni mtu wa maonesho au mtu ambaye ana fedha zake na pengine hana tabia njema na anaweza hata kukuumiza kwa kuwa na watu wengi au kukuacha kabisa.

 

Ndugu zangu masuala haya ya uhusiano yanahitaji hekima, yanahitaji jicho la tatu kung’amua na kujua mtu gani ni sahihi tena kwa wakati. Usipoteze muda, kaa chini na utafakari nani ni sahihi kwako kwa wakati na uchukue hatua mapema. Kuwa na msimamo.

 

Usikubali kuyumbishwa na tamaa za mali na mambo mengine. Cha msingi angalia mtu sahihi kwako na ufanye naye maisha kwa wakati. Kwa leo inatosha! Unaweza kunifuata kwenye mitandao ya kijamii, Instagram na Facebook natumia Erick Evarist, Twitter natumia ENangale.

 

JIUNGE NA FAMILIA YA GLOBAL TV UPANDE MTANDAO WA MAFANIKIO

Bofya hapa kujiunga na familia ya Global TV Club ==> Global TV Family Club

Comments are closed.