The House of Favourite Newspapers

Wakati mwingine uongo unasaidia kudumisha uhusiano lakini…

0

MALOVE6TUMSHUKURU Mungu kwani ni Jumamosi nyingine ametukutanisha hapa katika safu hii mimi na wewe msomaji wangu. Tunaweza kujifunza mambo mbalimbali yanayotusaidia katika maisha yetu ya uhusiano.

Bila kupoteza muda, mada hapo juu inajieleza. Wengi wetu tunaamini kwamba kwenye maisha ya uhusiano, kuambizana ukweli ni jambo la msingi. Ni jambo ambalo linaweza kudumisha uhusiano kwani kila mmoja anakuwa na amani na mwenzake kama tu mnaambiana ukweli.

Mwanaume anakuwa hamfichi kitu mwanamke. Mwanamke naye anamueleza kila kitu mwanaume. Wanaamini kwa kufanya hivyo kutasaidia penzi lao kuwa la kweli na uaminifu. Kila mmoja anakuwa na amani kwa sababu anatambua kwa wakati husika, mwenzake anakuwa wapi na anafanya nini. Kwa kufanya hivyo wanaamini haiwezi kutokea migogoro kati yao kwani hawafichani.

Kuelezana ukweli kuna maana kama wapendanao mtakubaliana na ukweli. Mmoja wenu asipokubaliana nao, ukweli waweza kuwa sumu kali itakayowagharimu. Nasema hivyo kwa sababu, kuna baadhi ya watu wana kasumba ya kutokubaliana na ukweli.

Ukisema umueleze ukweli wa kila kitu, kwake linakuwa tatizo kubwa kuliko hata usingemueleza. Mfano mdogo, mwanaume anakuwa na kawaida ya kutoka kazini na kurudi nyumbani moja kwa moja. Si mtu wa kuchelewa sana kurudi nyumbani kwake.

Mwanamke anakariri kwamba hata kama mumewe atachelewa vipi, haizidi saa nne usiku. Kuna siku atahisi kuwa ametoka kazini na kugundua atachelewa kurudi, analazimika kumuambia ukweli mkewe kwamba atachelewa kurudi nyumbani kwa sababu gani na atakuwa sehemu fulani.

Anamueleza kwamba hana uhakika kwamba anaweza kuzidisha muda wake wa kawaida wa kurudi nyumbani lakini anatoa kama taarifa ili mwenzake ajue kuwa ikitokea amechelewa, atambue kwamba atakuwa amecheleweshwa na nini.

Mwanamke anapotajiwa hiyo sehemu, badala ya kukubaliana na ukweli, anaibua jipya. Anaanza kujiongeza kuwa kwa nini hakusema mapema kwamba atapitia huko. Anahoji kwa nini amshtukize wakati tangu asubuhi alifahamu ratiba hiyo.

Jambo jema alilolifanya mwanaume linageuka kuwa shubiri. Linageuka kuwa mada ya kuijadili. Linachukua muda mrefu hadi kuliweka sawa. Mwanamke kwa kasumba yake tu hataki kukubaliana na ukweli kwamba mpenzi wake yuko mahali fulani.

Mwanamke anaanza kujiongeza kwa maneno ambayo yanakwenda kumkasirisha mpenzi wake, matokeo yake wanagombana pasipo kuwa na sababu za msingi. Hapo ndipo baadhi ya wanaume wanapotafuta kiini cha tatizo na kuona hakukuwa na haja ya kuzungumza ukweli.

Kwamba pengine jambo lenyewe halikuwa kubwa. Angeweza kulipotezea na kutomwambia, lingepita na bado angewahi kurudi nyumbani katika muda ambao mke wake au mpenzi wake ameuzoea. Siku nyingine mwanaume haoni sababu ya kumueleza ukweli.

Anaamua kumdanganya ilimradi aepushe shari. Kwamba muda ule ambao anakuwa anataka kwenda kukutana na miadi yake, hamuelezi kuwa anakwenda huko. Na ikitokea amemuuliza, analazimika kumwongopea kwa kumwambia yupo kazini.

Anamdanganya kuwa kuna kazi nyingi hivyo analazimika kuzifanya hata kama atachelewa kidogo kurudi. Anahofia akimueleza ukweli litakuwa tatizo. Hapo uongo unakuwa umeimarisha ndoa kama si penzi lao. Kila mtu anapenda amani katika uhusiano, hapendi malumbano hivyo kutumia njia haramu kuepusha malumbano haoni tatizo.

Hoja yangu hapa ni nini, mnapaswa kuambiana ukweli pale unapohitajika. Lazima wote muwe tayari kuupokea ukweli ili muweze kufika mbali. Kikubwa ni kuaminiana. Usiishi na mtu ambaye humuamini, ni hatari sana. Ni vyema ukasitisha safari ya uhusiano kama uliyenaye humuamini.

Kwa kuzingatia hilo, hakuna sababu ya kuelezana uongo lakini mkubaliane na ukweli ili muweze kuishi kwa raha mustarehe!

Tukutane wiki ijayo kwa mada nyingine nzuri!

Leave A Reply