The House of Favourite Newspapers

Wakati umefika kila Mtanzania aweke mbele amani na utaifa

0

Uchaguzi mkuu wa nchi hapa kwetu tunaweza kusema ni shughuli inayofanyika kila baada ya miaka mitano.

Uchaguzi una sehemu ndogo katika maisha yetu kuliko amani. Tukikaa bila amani tutavurugikiwa, tutashindwa kufanya uzalishaji na hakika tutakufa, kwa sababu ni lazima kula kila siku.

Jamii nyingi duniani zimeishi kwa muda mrefu bila kuwa na haki ya kushiriki katika uchaguzi na watu wake hawakufa kwa njaa.

Kwa mantiki hiyo, uchaguzi ni zoezi muhimu linalopata ulazima wake katika jamii iliyoamua kujenga utawala wa kidemokrasia. Kwa hiyo, ingawa uchaguzi si lazima ili tuendelee kupumua kama binadamu, unakuwa ni lazima ili demokrasia ikomae nchini.

Hivyo napenda kutoa uchauri kwa wananchi wenzangu wa nchi hii kwamba tuupe uchaguzi huu wa sasa, umuhimu unaostahili. Wakati tunatafakari nani wa kumchagua, tusije tukajisahau sisi ni nani, na nini tunatakiwa kufanya, kwa sababu tu ya uchaguzi.

Ndiyo maana nimekuwa nikilaumu baadhi ya matendo yasiyofaa yanayofanywa na watu wanaojiita wanasiasa, matendo ambayo yanaashiria kupungua kwa heshima na uadilifu na kuhatarisha amani.

Uchaguzi mkuu ni jambo la mara moja katika kipindi kilichopangwa na taifa au asasi, kwa hiyo inawezekana kusema kwamba utakuja uchaguzi kisha utapita, na watu wataendelea na utaratibu wao wa maisha kama walivyozoea.

Kama watu walikosa ustaarabu wakati wa uchaguzi mkuu na wakawa wanatenda mambo kama hawana akili sawasawa, ni tatizo kwani itawachukua muda mrefu kuwa na akili za kawaida baada ya uchaguzi.

Huko nyuma nimewahi kuonesha kwamba, tumekuwa tukijenga utamaduni wa chaguzi za kudumu, hali inayonitia wasiwasi nikiangalia uchafu unaoambatana na hizo chaguzi. Rushwa, maneno ya kashfa, matusi ni mambo ambayo yamekuwa yakitawala kampeni.

Baadhi ya vyama katika kampeni vimekuwa vikisomba hisia za sehemu kubwa ya nchi hii na kuhamasisha kila aina ya vitendo vya ugomvi, majungu, fitina na ulaghai.

Hadi leo vitendo hivyo vimeacha vidonda na makovu ambayo yataonekana hata baada ya kupiga kura Oktoba 25, mwaka huu. Hadi leo bado yako malumbano miongoni mwa makada waliomuunga mkono huyu na wale waliomuunga mkono yule.

Sehemu ya visasi na vinyongo vilivyojengeka wakati wa kura za maoni za mwaka huu katika vyama vikuu,  Chama Cha Mapinduzi (CCM) na Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) ni muendelezo wa uhasama uliozaliwa miaka kadhaa iliyopita, kisa kura za maoni.

Kila baada ya miaka mitano chama tawala kinapata misukosuko na Chadema pia kunakuwa na mtikisiko.

Hata hivyo, kiukweli vyama vya upinzani sasa vimeanza kukua na hautapita muda mrefu tutaanza kushuhudia vikifuata utamaduni wa chama tawala wa chaguzi za aina hii.

Ukali wa mabishano umeanza kujitokeza katika baadhi ya vyama vya upinzani kama tulivyoona kwa Chadema hasa baada ya aliyekuwa katibu mkuu wao Dk. Wilbrod Slaa kujitoa baada ya Edward Lowassa kukaribishwa na kupewa nafasi ya kugombea urais, ni wazi CCM na Chadema ni wapinzani kama walivyo Simba na Yanga.

Sasa, ikija kutokea tukawa na vyama vikubwa vitatu, kisha vikashiriki katika uchaguzi mkuu, hali itakuwa ya ushindani zaidi. Si vigumu kuona jinsi ambavyo miaka mitano yote inavyoweza kukumbwa na homa ya chaguzi.

Laiti ingekuwa kwamba kila tunapoingia katika uchaguzi mkuu tunafanya uchaguzi na wala si uchafuzi hili lingekuwa jambo la heri.

Sumu na uvunjifu wa amani inayoingizwa katika mishipa ya fahamu ya Watanzania ni hatari kwani huwa haiondoki kwa urahisi. Itakuwa ikiongezeka kila siku. Kwa hali hiyo nawaomba wanasiasa na wananchi wote tunapoelekea kwenye uchaguzi mkuu, kila mmoja amani ya nchi aweke mbele. Vyama vitakufa lakini Tanzania haitakufa kamwe, kila mmoja aweke utaifa mbele kwa kudumisha amani, huo ni wosia wa Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere.

Jipu limepasuka, siwezi kuwa adui kwa kusema ukweli.

Leave A Reply