Wakenya waonja Joto la Jiwe

MVUTANO kuhusu uamuzi wa Serikali ya Kenya kufunga mipaka kati yake na Tanzania, umezidi kuchukua sura mpya baada ya hatua hiyo kutajwa kuwa shubiri kwa wafanyabiashara wa Kenya ambao wanategemea zaidi bidhaa na malighafi mbalimbali zinazozalishwa nchini.

Licha ya kwamba nchi hizo mbili wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, hutegemeana kibiashara, wachumi waliozungumza na IJUMAA wamebainisha wazi kuwa mvutano huo unaathiri Wakenya wenye kipato cha chini kwa kiasi kikubwa hutegemea bidhaa zitokanazo na mazao kutoka Tanzania.

CHANZO CHA MVUTANO

Mvutano wa kibiashara kati ya Kenya na Tanzania, licha ya kuwa na historia ndefu iliyolazimu wakuu wa nchi hizo mbili kukaa meza moja na kumaliza tofauti hizo kila mara, hali imekuwa tofauti kuanzia Mei 16 mwaka huu baada ya Rais wa Kenya, Uhuru Kenyatta kutangaza kufunga mipaka ya nchi yake na nchi za Tanzania na Somalia ili kudhibiti maambukizi ya Virusi vya Corona kwa siku 30.

Katika amri hiyo, Rais Uhuru alisema watu hawataruhusiwa kusafiri kuingia au kutoka Kenya kwenda Tanzania na Somalia, lakini mizigo itaruhusiwa.

Hata hivyo, katika amri hiyo iliyoanzia kutekelezwa kuanzia Mei 16 saa sita usiku, alisema madereva watatakiwa kupimwa kubaini kama wameambukizwa virusi vya Corona na watakaopatikana wameambukizwa, hawataruhusiwa kuingia Kenya.

WAKENYA WALIA

Aidha, pia baadhi ya Wakenya waliopo katika mipaka ya Sirari, Holili, na Hororo, wakilieleza IJUMAA kwa njia ya simu, walisema hatua iliyochukuliwa na serikali yao imeathiri pakubwa maisha yao.

“Kwa sababu sisi huku mpakani tunategemeana, kama unavyojua hadi nyama tunategemea upande wa Tanzania ambao wana mifugo mingi, kwa hiyo hatua hii inatuathiri sana,” alisema Fred Oforo kutoka Sirari.

Naye mfanyabiashara mwingine kutoka Holili, alisema ni vema wakuu wa nchi zote mbili au mawaziri wangemaliza tofauti zilizojitokeza kwa sababu maambukizi ya virusi hivyo yapo pande zote.

“Hatua wanazochukua wenzetu, zinatuathiri sisi wafanyabiashara na watu wa hali ya chini, kwa sababu huku tunanunua vitu vingi Tz ukilinganisha na hivi tunavyopata huku kwetu,” alisema.

WAKUU WA MIKOA TZ WACHARUKA

Kufuatia hatua hiyo, wakuu wa mikoa ya Tanga, Kilimanjaro, Arusha na Mara ambayo imepaka na Kenya, walitangaza kuzuia malori yote ya mizigo yanayotoka Kenya kuingia nchini, na kuagiza wamiliki wa mizigo hiyo wajiandae kupeleka malori mengine ambayo yanapakiwa mizigo hiyo upande wa Tanzania baada ya kupakuliwa upande wa Kenya.

Mei 18 mwaka huu, Mkuu wa mkoa wa Tanga, Martin Shigela, alisema “Hatuwezi kuwa na bidhaa na watu wanakaa hapa wiki nzima alafu wanaambiwa wana Corona,” alisema Shigela.

Shigela alisema wakati madereva wa upande wa Tanzania wakizuiliwa kuingia Kenya kwa madai ya maambukizi ya virusi vya Corona, upande wa Tanzania madereva 19 wa malori kutoka Kenya walipatikana na Corona.

Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Anna Mghwira naye mwishoni mwa wiki alitangaza kuzuia magari ya mizigo kutoka Kenya kuvuka katika mpaka wa Holili na badala yake magari hayo yatalazimika kupakua mzigo huo mpakani na kuchukuliwa na magari ya Tanzania.

“Malori yote yanayobeba mizigo na yanayomilikiwa na raia wa Tanzania, na yangependelea kuingia Tanzania ama yanamilikiwa na raia mwingine wa kigeni lakini bidhaa hiyo iliagizwa na Mtanzania, tafuta lori jingine ili kusafirisha mizigo hiyo inakoelekea. Malori kutoka mataifa mengine hayataruhusiwa kuingia,” alisema Mghwira

Mkuu wa Mkoa wa Mara, Adam Malima naye aliwaagiza maafisa wa Forodha katika kituo cha Sirari kuhakikisha kuwa madereva wa malori kutoka Kenya, hawaingii nchini kupitia mpaka huo.

Utaratibu huo hata hivyo haujumuishi madereva wa malori wanaosafiri kupitia mipaka ya Tanzania kwenda Rwanda, Burundi, Zambia na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo.

BALOZI KENYA AIBUKA

Aidha, Mei 19 mwaka huu, Balozi wa Kenya nchini Tanzania Dan Kazungu, alisema hatua ya Kenya kufunga mpaka na majirani zake haiwalengi Watanzania.

“Uamuzi ambao Kenya imechukua kuhusu safari za mipakani, sio kwa sababu ya Tanzania, bali adui yetu ni kirusi cha Corona,” alisema Balozi Kazungu.

WACHUMI WANENA

Wakizungumza na IJUMAA, Mhadhiri Mwandamizi wa Chuo Kikuu cha Mzumbe, Profesa Honest Ngowi alisema, hatua zilizochukuliwa ni sawa na vichaa wawili wanaokimbiza bila kuvaa nguo.

Mhadhiri huyo wa masuala ya uchumi, alisema mvutano huo, umesababisha vikwazo visivyo vya kikodi ambavyo ni gharama kubwa kwa wafanyabiashara wa pande zote mbili.

Kutokana na hali hiyo, alifafanua kuwa pande zote zinapaswa kufuata taratibu za kidiplomasia kutatua mvutano huo.

Hoja hiyo, iliungwa mkono na Mhadhiri mwa Chuo cha Diplomasia Dar es Salaam, alisema kiujumla maamuzi yaliyochukuliwa na Serikali ya Kenya si maamuzi sahihi, bali ya kukurupuka.

Alisema kabla ya Kenya kuchukua hatua ya kufunga mipaka yake, ilitakiwa kuhusisha serikali za pande zote mbili kupitia wizara ya mambo ya nje na si kuhaha kuitafuta wizara ya afya kama inavyodaiwa na balozi wake.

Alisema ni dhahiri kuwa Kenya inaitegemea zaidi Tanzania katika upatikanaji wa bidhaa za mazao ya chakula, kwa kuwa Kenya haina ardhi ya kutosha kuzalisha bidhaa hizo.

“Kule Kenya hakuna ardhi, iliyopo imehodhiwa na wachache, kwa maana hiyo, ardhi ya kilimo hakuna, ndio maana wanategemea mazao yanayozalishwa Tanzania kama vile; maparachichi, viazi, mahindi na mazao mengine ya chakula ambayo yanagusa maisha ya chini ya Wakenya.

“Kitendo cha kufunga mipaka, mbali na kuathiri wafanyabiashara, pia kitaathiri Wakenya wa hali ya chini, kwa sababu ya njaa,” alisema.

Aidha, Profesa Gaudence Mpangala kutoka Chuo kikuu cha Ruaha, naye alisema chimbuko la mvutano huo ni kutoshirikiana kwa nchi zote katika kufanya maamuzi ya baadhi ya mikakati ya kudhibiti ugonjwa huo.

TAKWIMU ZINASEMAJE?

Hadi kufikia Mei 20 mwaka huu, idadi ya watu walioambukizwa virusi vya Corona nchini Kenya wamefikia 1029 huku watu 50 wakipoteza maisha kwa maambukizi ya virusi hivyo.

Kwa upande wa Tanzania, walioambukizwa virusi hivyo wamefikia 509 huku watu 21 wakifariki kutokana na ugonjwa huo wa COVID-19.

Wakati maambukizi ya virusi hivyo yakizidi kupamba moto, Ripoti mpya iliyotolewa na Shirika la Umoja wa Mataifa la mpango wa chakula duniani (WFP), Mei mwaka huu, imeeleza kuwa tatizo la njaa linaweza kuongezeka zaidi ya mara mbili katika nchi za Afrika Mashariki na Pembe ya Afrika katika miezi mitatu ijayo kutokana na athari za virusi vya Corona.

Ripoti hiyo kuhusu athari za kijamii na kiuchumi za janga la Corona (COVID-19) iliyotolewa jana mjini Nairobi Kenya, ilisema watu walio katika hatari zaidi ya njaa ni watu wanaoishi mjini ambao wanategemea kipato cha siku kwa ajili ya mlo kutoka kwenye sekta zisizo rasmi.

Ripoti hiyo inakadiria kuwa idadi ya watu wasio na uhakika wa chakula katika ukanda huo, inatarajia kuongezeka kati ya milioni 34 na milioni 43 kuanzia mwezi huu wa Mei hadi Julai kutokana na athari za kiuchumi na kijamii za COVID-19.

Hatua hiyo inakuja ilhali nchi za Kenya, Ethiopia, Sudan Kusini, Somalia, Uganda, Rwanda, Burundi, Djibout na Eritrea, zimekumbwa na mlipuko wa nzige wa jangwani na mafuriko yanayotishia nchi hizo kukumbwa na baa la njaa.

Naibu Mkurugenzi wa kikanda wa WFP, Brenda Behan alisema watu zaidi wanatarajiwa kufa kutokana na athari za kiuchumi na kijamii za COVID-19 kuliko virusi vyenyewe huku wakimbizi na watu maskini wanaoishi mjini katika ukanda huo, wako katika.

Stori: GABRIEL MUNSHI, Ijumaa


Loading...

Toa comment