The House of Favourite Newspapers

Wakili Hashim Rungwe… Aishauri Serikali Mambo Mazito-2

0

rungwe

WIKI iliyopita Wakili Hashim Spunda Rungwe alishauri mambo mengi ambayo anaona yanafaa serikali iyafanye ili kupiga hatua mbele za kimaendeleo na kuwaondolea njaa wananchi. Leo anamaliza ushauri wake kwa serikali ya wamu ya tano; fuatana nasi katika mahojiano kati yake na wahariri wetu yaliyofanyika hivi karibuni ofisini kwake Kijitonyama jijini Dar es Salaam:

Yapo madai kuwa mizigo mingi ilikuwa inapita bandarini bila kulipia ushuru tena vyakula vingine vikiwa havifai kwa matumizi ya binadamu, wewe kwa uzoefu wako kwani umekuwa ukitoa mizigo bandarini miaka mingi, unashauri nini ili hilo lisitokee?

Rungwe: Kama nilivyosema awali hilo siyo la kulaumu uongozi uliopo kwa sababu ni mfumo wa tangu viongozi waliopita. Lakini kusema kwamba kuna vyakula vinapita pale bandarini havifai kuliwa, hilo siyo jukumu la sisi kulizungumzia kwa sababu kuna Mamlaka ya Chakula na Dawa, TFDA, wao ndiyo wenye jukumu la kuhakikisha vyakula vyote vinavyoingia nchini ni salama, sasa ukisema kuna vyakula vinaingia nchini vyenye sumu maana yake nini? Kuhusu mizigo kupita bandarini bila kulipiwa kodi au kwa maneno mengine ukwepaji wa kodi ni kwamba mizigo ikiingia bandarini ili itoke ni lazima ilipiwe ushuru, nitashangaa sana kuambiwa kuwa kuna wanaokwepa kodi.

Yapo madai kuwa wanakwepa kulipa ushuru kupitia bandari kavu, hilo unalizungumziaje?

Rungwe: Ninavyofahamu ni kwamba wote wenye bandari kavu lazima wawe na bond (dhamana), sasa mfanyabiashara atakwepaje ushuru? Ukweli ni kwamba haya maneno mengi ya viongozi wetu kuhusu wafanyabiashara na bandari yamesababisha kupungua kwa mizigo bandarini na hiyo maana yake ni kwamba ajira nazo zitakuwa zimepungua.

Imeshauriwa mifuko ya kijamii ile inayochangiwa na wafanyakazi kwa kukatwa kodi itumbukize fedha kwenye biashara, wewe kama mwanasheria unaonaje ushauri huo?

Kwanza ni dhahiri rais hana ujuzi wa biashara. Huko nyuma tuliwahi kupata hasara kwa kuwaingiza wanasiasa kufanya kazi katika mashirika yaliyokuwa yakijiendesha kibiashara. Ushauri wangu, kama ana nia ya dhati, asijiingize kwenye biashara, serikali ilishaacha biashara. Mifuko ya jamii kuiingiza katika biashara kuna hatari zake. Watu wakistaafu kazi watataka kulipwa bila kuchelewa, sasa ukiingiza fedha zao huko zikikwama itakuwaje?

Mara baada ya kuingia madarakani Rais Magufuli amefuta sherehe kadhaa za kitaifa, hilo ulilipenda? Nini maoni yako.

Rungwe: Sikupenda kabisa mtindo wa kufuta sherehe za kitaifa, zina maana yake, kwa mfano bila Mapinduzi Zanzibar kusingekuwa na Muungano. Namshauri aache kufuta sherehe za kitaifa. Afanye hata kama ni ndogo, kwa mfano, kungekuwa na gwaride dogo pale ikulu na watu wakaona, kungekuwa na ubaya gani?

Unazungumziaje utawala wa awamu ya nne wa Rais Mstaafu, Jakaya Kikwete ambao leo unalaumiwa na baadhi ya wananchi?

Rungwe: Sitetei marais waliopita lakini ukweli ni kwamba utawala wa Kikwete ulijenga barabara nzuri za lami nchi nzima, madaraja makubwa na majengo mazuri ya umma. Kuna aliyoteleza lakini kama nilivyosema awali ni mfumo uliokuwepo na nikiujadili hapa, nitajaza kurasa zote la gazeti lako. Kifupi ni kwamba mfumo huo umeleta njaa. Sasa inatakiwa kubuni mbinu za kuwaondolea watu njaa, viongozi waache manenomaneno.

Leave A Reply