The House of Favourite Newspapers

WAKO MGUU NJE, NDANI DIRISHA DOGO LA USAJILI

Mats Hummels.

HUKU dirisha dogo la usajili likiwa limefun guliwa, Januari hii, tayari kumeanza kusambaa taarifa za mastaa mbalimbali wa soka kutaka kuhama au kuuzwa. Kutokana na ukweli kuwa baadhi ya timu baada ya kujitathmini kwenye mzunguko wa kwanza wa ligi, zimeanza kuhaha kuanza harakati za kujiimarisha.

Pia kuna baadhi ya wachezaji, baada ya kuona wanakosa nafasi kwenye timu zao wameanza kuhaha kusaka timu. Mastaa wafuatao wana uwezekano mkubwa kwa kuhama timu zao na kujiunga na timu nyingine.

Sergej Milinkovic-Savic

1. MATTS HUMMELS (BAYERN MUNICH KUJIUNGA CHELSEA)

Ametamba kwa miaka mitano akiwa beki tegemeo wa Bayern na timu ya taifa ya Ujerumani. Hummels amekuwa na wakati mgumu kwenye timu ya Bayern Munich msimu huu kutokana na kulaumiwa kwa kushuka kiwango kiasi cha kuanza kuwekwa benchi na kocha wa timu hiyo, Niko Kovac.

 

Hummels alitupiwa lawama nyingi pamoja na mwenzake Jerome Boateng kutokana na Ujerumani kufanya vibaya kwenye Fainali za Kombe la Dunia.

 

Kibaya zaidi kocha wa Ujerumani, Joachim Low naye amesema kuwa Hummels hayupo sawa kwa sasa. Hata hivyo, kuna taarifa kuwa kocha wa Chelsea, Maurizio Sarri anataka kumsajili. Habari zaidi zinaeleza kuwa Chelsea ipo kwenye hatua za mwisho za kumnasa Hummels.

 

2. SERGEJ MILINKOVICSAVIC (LAZIO KUJIUNGA NA MANCHESTER UNITED)

Milinkovic-Savic amekuwa anafuatiliwa na Manchester United kwa muda mrefu. Mserbia huyo amekuwa anacheza soka ya kiwango chajuu katika ligi ya Serie A akiwa na timu ya Lazio.

 

Alifanya vizuri msimu uliopita wa 2017/18, akitoa asisti 12 na kufunga mabao matatu kwenye mechi 25 za Serie A. Hata hivyo, makali ya kiungo huyo mwenye umri wa miaka 23 yamepungua kwa kiasi fulani msimu huu na kufanya bei yake kuwa chini.

 

Kocha wa zamani wa Manchester United, Jose Mourinho ndio alikuwa anamtaka zaidi kiungo huyo ingawa sasa timu hiyo ipo chini ya Ole Gunnar Solksjaer, ambaye tangu ametua, timu hiyo imekuwa inafanya vizuri.

 

3. AARON RAMSEY (ARSENAL KUJIUNGA JUVENTUS)

Ramsey ni staa mwingine, ambaye yupo katika harakati za kuhama baada ya kushindwa kufikia muafaka wa mkataba mpya na Arsenal. Kiungo huyo wa Wales anamaliza mkataba wa kuchezea Arsenal mwishoni mwa msimu huu.

Akiondoka mwishoni mwa msimu huu ina maana Arsenal haitapata chochote. Uongozi wa Arsenal inasemekana upo katika harakati za kutaka kumuuza kiungo huyo mwezi huu wa Januari. J u v e n t u s inasemekana ndio inapewa nafasi ya kumchukua Ramsey, ingawa kuna taarifa kwa Bayern Munich nao wanamtaka kiungo huyo.

 

Ramsey amekuwa kati ya wachezaji muhimu wa Arsenal tangu aibuliwe akiwa na umri wa miaka 18 mwaka 2008 na ana nafasi ya kupandisha kiwango chake atapojiunga na Juve, ambao wana rekodi ya mafanikio kwenye Serie A na Ulaya.

 

4. FABREGAS (CHELSEA KUJIUNGA MONACO)

Jina la Fabregas limekuwa linatajwa sana kama miongoni mwa mastaa, ambao wamekuwa wakitajwa sana kuwa wanataka kuhama timu zao. Kiungo huyo mwenye umri wa miaka 31 ni miongoni mwa mastaa wenye rekodi ya kutoa asisti nyingi kwenye Ligi Kuu England. Staa huyo wa zamani wa timu ya taifa ya Hispania, ataondoka bure mwishoni mwa msimu endapo hatouzwa kipindi hiki cha usajili wa January.

 

Fabregas amekuwa anacheza soka la kiwango cha
juu katika kipindi cha miaka 10. Pamoja na kuwa umri umemtupa mkono anatajwa kuwa miongoni mwa wachezaji wa nafasi ya kiungo bora duniani. Klabu zinazotajwa sana kumtaka sana staa huyo ni pamoja na Monaco, AC Milan na Manchester City. Hata hivyo, watu walio karibu na Fabregas wanadai kuwa staa huyo anatazamiwa kujiunga na Monaco kwani anatakiwa na kocha Thierry Henry ili aende kuisaidia timu hiyo isishuke daraja kutoka kwenye Ligue 1.

Comments are closed.