The House of Favourite Newspapers

Wako Wapi Wenzetu?

0

STORI: MWANDISHI WETU | GAZETI LA AMANI | ARUSHA

Mungu mkubwa! Hali za wanafunzi manusura watatu wa ajali iliyosababisha vifo vya watu 35, wakiwemo wanafunzi 32, walimu wawili na dereva mmoja, wote wa Shule ya Lucky Vincent Nursery and Primary iliyopo Olasite jijini hapa, zinatia matumaini baada ya gazeti hili kuelezwa kwamba wanaendelea vizuri.

Wakati wenzao wakizikwa sehemu mbalimbali nchini kuanzia Arusha, Kilimanjaro, Tanga, Manyara na kwingineko na kuacha vilio kila kona, wao Mungu anawapigania wakiwa kwenye Chumba cha Wagonjwa Mahututi (ICU) katika Hospitali ya Mkoa wa Arusha ya Mount Meru.

WAKO WAPI WENZETU?

Kwa mujibu wa chanzo chetu ambacho ni mtu mwenye sifa ya kuingia Chumba Cha Wagonjwa Mahututi (ICU) walicholazwa wanafunzi hao, walionusurika ni pamoja na Doreen Mshana mwenye umri wa miaka 13 ambaye juzi (Jumanne) alizungumza kwa tabu akihoji: “Wako wapi wenzetu?”

Mbali na Doreen, wengine ambao nao wanaelezwa kuwa maendeleo yao kiafya siyo mabaya ni Sadia Isamel Awadhi mwenye umri wa miaka 11 na Godfrey Tarimo ambaye naye ana umri wa miaka 11.

Makamu wa Rais, Bi. Samia Suluhu akiwajulia hali watoto waliojeruhiwa kwenye ajali ya Karatu.

MANESI WAPATA WAKATI MGUMU

Mtu huyo ambaye aliomba kutotajwa jina na nafasi yake gazetini alisema kuwa, hata manesi na wahudumu wa hodi hiyo walipata wakati mgumu wa kumjibu Doreen ambapo waliamua kumwambia kuwa wenzao wapo shuleni isipokuwa yeye na wenzake waliolazwa walipata ajali na wanaendelea vizuri.

“Kimsingi wote sasa hivi wanaongea. Doreen anaongea vizuri zaidi kulinganisha na wenzake ambao bado hawajawa vizuri,” alisema mtu huyo na kuongeza:

“Maskini! Inauma sana maana kinachoonekana walipoteza fahamu na hawajui kama wenzao walifariki dunia. Kimsingi mbali na matibabu, lakini akina Doreen watahitaji msaada mkubwa sana wa kisaikolojia.”

SIMANZI, HUZUNI UPYA

Hata hivyo, juzi watoto hao walisababisha kuibuka kwa simanzi na huzuni upya nje ya wodi hiyo huku kila mtu akitaka kuingia ndani kwenda kuwaona.

Pia baadhi ya ndugu, jamaa, marafiki na watu mbalimbali walifurika wodini hapo na kuzuiwa kuingia ambapo waliishia kuangusha maombi ya uponyaji kwa watoto hao.

WAZAZI WARUHUSIWA

Kwa upande wa wazazi walioruhusiwa kuingia waliliambia gazeti hili kuwa, watoto wao wanaendelea vizuri na kwamba wanaamini Mungu atawaponya ‘soon’ hivyo wao wanamuachia Mungu atende muujiza.

WAPOTEZA KUMBUKUMBU

Kwa upande wake muuguzi aliyeomba hifadhi ya jina gazetini kwa kuwa siyo msemaji wa hospitali hiyo alisema kuwa, alifanikiwa kuwahudumia watoto hao na kubaini kuwa walipoteza kumbukumbu lakini zimekuwa zikiwarejea taratibu.

“Unajua wanaonekana walipoteza kumbukumbu ndiyo maana Doreen alihoji walipo wenzake. Inaelekea baada ya kutokea kwa tukio lile hakujua kilichoendelea hadi alipofikishwa hapa (Mount Meru Hospitali).

“Lakini kama hali ya kutokuwa na kumbukumbu itaendelea, kuna mpango wa kupelekwa kwenye matibabu nje ya nchi na hasa Marekani kama alivyosema Makamu wa Rais (Samia Suluhu Hassan) pale Sheikh Amri Abeid wakati wa zoezi la kuaga waliofariki dunia.

“Lakini yote kwa yote vyombo vya habari vitapewa taarifa rasmi kesho (jana) kuhusu maendeleo ya watoto hawa,” alisema muuguzi huyo juzi Jumanne alipozungumza na gazeti hili.

MGANGA MKUU ATAFUTWA

Amani lilifanya jitihada za kuzungumza na Mganga Mkuu wa Hospitali ya Mount Meru ambaye ndiye msemaji lakini simu yake ya kiganjani iliita bila kupokelewa na hata alipofuatwa ofisini kwake hakuwepo. Pamoja na kusubiriwa kwa zaidi ya saa sita lakini bado hakutokea kwa maelezo kwamba yupo kwenye kikao kirefu kuhusiana na tukio hilo.

MEI 6, MWAKA HUU

Watoto hao walinusurika kwenye ajali hiyo iliyotokea Jumamosi ya Mei 6, mwaka huu katika Mlima wa Rhotia kwenye Kijiji cha Marera wilayani Karatu walipokuwa wakienda kufanya mtihani wa ujirani mwema na Shule ya Tumaini Academy ya mjini Karatu.

Mama wa Mtoto Aliyenusurika kwa Mabomu Akafariki kwa Ajali Karatu

Leave A Reply