Binti Mlemavu Anayeandikia Ulimi Asimulia Alivyopata Mchumba – Video
Kwa kumbukumbu, ilikuwa ni Februari 3, 2012 siku ambayo walikuwa na mahafali ya kumaliza kidato cha sita katika Shule ya Sekondari ya Wasichana ya Korogwe jijini Tanga ndipo ajali mbaya iliwakuta wakiwa wanafunzi tisa baada ya mwenzao mmoja kuingia ndani ya gari la ndugu yake aliyekuja kumtembelea na ghafla gari hilo lilianza kurudi nyuma kwa kasi ndipo walipokutwa na majanga hayo.
Kilichotokea ndicho kimetengeneza taswira nyingine kabisa ya maisha ya binti Wakonta kwani gari hilo lilimgonga yeye na wenzake na kumsababishia ulemavu wa uti wa mgongo ambapo amepooza sehemu yote ya kiwiliwili.
Baada ya kupita ukimya wa muda mrefu, Risasi Jumamosi limefika nyumbani kwa Wakonta, Kigamboni jijini Dar na kufanya naye mahojiano maalum ambapo amevunja ukimya kuhusu maisha yake ya sasa. Wakonta Kapunda, mwenyeji wa Sumbawanga nchini Tanzania anaeleza mengi.
Risasi: Ni vigumu mzazi kumuacha mtoto wake aishi mwenyewe, tena akiwa katika hali kama yako, hebu tuambie, ilikuwaje hadi wazazi wako wakakuacha ujitegemee?
Wakonta: Labda nianze kwa kueleza kilichotokea hadi siku ya tukio. Nakumbuka ilikuwa mwaka 2012, nilipata ajali na kupooza siku ileile.
Baada ya hapo nilianza kuhudumiwa na mama yangu tangu kipindi hicho hadi nilipoamua kuishi peke yangu. Unajua ukikaa na mtu mwenye tatizo kama langu ni kama vile unaishi na mtoto mchanga, maana kila kitu ninahudumiwa.
Ilifika wakati fulani mama yangu akawa hawezi kwenda mahali, akakaa muda mrefu kwa sababu yangu. Kuna kipindi nilimuona mama yangu hawezi hata kulala usiku. Hali hiyo iliendelea hadi miaka kama saba hivi.
Ilifika hatua mama yangu akaanza kuugua magonjwa mbalimbali kwa sababu ya kukosa usingizi ukizingatia na umri wake umeenda.
Hali hiyo ilikuwa inaniumiza sana, kwa hiyo nikasema moja ya ndoto zangu ni kumuweka mama yangu huru, hivyo nilipopata nafasi ya kujitegemea, nikasema siwezi kusubiri. Nilimuomba mama yangu nikajitegemee kwani nilitaka arudi nyumbani ili akaishi na baba. Mwanzoni haikuwa rahisi mama yangu kunikubalia. Kwanza aliniona kama ninatania, lakini mwisho alinikubalia.
Risasi: Tangu umepata matatizo ni muda mrefu umepita, umewahi kuwaza kujiendeleza kielimu au kufanya jambo mbali na uhamasishaji?

Wakonta: Mwaka jana wakati tunazindua Taasisi ya DR Mengi (Mungu amlaze mahali pema peponi) ya walemavu, nilibahatika kukutana na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa ambaye aliniambia anataka nirudi shule na muda wowote nikiwa tayari nimwambie.
Kwa hiyo mwaka huu niliomba Chuo cha TIA (Dar) na nimepata nafasi hivyo muda wowote nitaanza chuo.
Kwenye uhamasishaji ndiyo kama nimeanza rasmi na naamini kuna watu ambao wanahitaji neno tu ili wapone, hawahitaji mtaji kwa sababu hata ukisema umpe mtaji sasa hivi hutamsaidia chochote.
Risasi: Unatumiaje muda wako kwenye mitandao ya kijamii?
Wakonta: Natumia mitandao ya kijamii kujielemisha, kutoa uzoefu wangu, kukumbusha watu vitu ambavyo wamevisahau, kuongea na watu mbalimbali na kufanya matangazo ya biashara mbalimbali.
Risasi: Unawezaje kufanya mambo yote hayo na sasa unatarajia kwenda chuo?
Wakonta: Mtandaoni kuna raha yake, muda mwingine unaweza kuingia na usipokuwa makini ukashangaa unazidi tu kupoteza muda wako. Nikiamka asubuhi huwa siingi mtandaoni labda kuwe na kazi ya mtu
ambayo natakiwa niiposti hivyo nitaingia mara moja nitaposti na kutoka halafu baadaye muda wa saa saba hivi ndiyo naingia Instagram kupitiapitia vitu mbalimbali.
Risasi: Unaingiza shilingi ngapi kwa siku kupitia matangazo?
Wakonta: Inategemea na tangazo lenyewe liko vipi.
Risasi: Kuna tetesi kwamba wewe ni mjamzito, hili lina ukweli kiasi gani?
Wakonta: Mimi mwenyewe nimekutana na hicho kitu mitandaoni, lakini hakina ukweli wowote kwa sababu nakumbuka mara ya kwanza niliona kwenye akaunti yangu ambayo nilikuwa naitumia muda mrefu na kipindi hicho nilikuwa natangaza bidhaa fulani hivi ambazo zinasaidia afya kwa akina mama kushika ujauzito. Kwa hiyo nadhani hii stori ilianzia hapo hivyo hata nilipoona nikachukulia kawaida tu.
Risasi: Unaendesha vipi maisha yako kwa sasa baada ya kutoka nyumbani?
Wakonta: Nafanya biashara na mitandao ya kijamii inanisaidia kuendesha maisha yangu. Pia nina website inaitwa Wakeneji. com ambayo ina vitabu na bidhaa za nyumbani kama nyanya na vitunguu, nawapelekea watu sehemu walipo.
Risasi: Unakutana na changamoto gani tangu umeanza kujisimamia mwenyewe?
Wakonta: Si rahisi kwa sababu mimi ndiyo kwanza nimeanza kuishi mwenyewe na kuna vitu vingi ningependa kuvifanya, lakini siwezi.
Kwa mfano kuna siku niliamka nikawa nataka nikanunue mafuta ya ngozi yanauzwa shilingi 45,000 na ‘delivery’ ni shilingi 5,000 hivyo inakuwa 50,000, sasa kabla sijaagiza mtoto akaja kuniambia gesi imeisha, sasa nanunua gesi au mafuta? Ikabidi ninunue gesi.
Risasi: Vipi kuhusu watu unaoishi nao hapa nyumbani wanakupa sapoti?
Wakonta: Nashukuru Mungu mabinti ambao naishi nao ni wazuri sana, naamini ni Mungu ndiye amenichagulia, kila mmoja anajua jukumu lake.
Risasi: Wakonta ni mtu wa aina gani?
Wakonta: Ni mtu ambaye hapendi kuongeaongea, naweza kukaa na hawa mabinti tusiongee hata neno moja na wala wasinione asubuhi hadi jioni na nisiwaite wala kuwauliza chochote.
Risasi: Imani yako kubwa katika hali uliyonayo ni ipi?
Wakonta: Hivi nilivyo sasa hivi ni tofauti na mwanzo, nilikuwa siwezi hata kuinua shingo kwa hiyo nina imani kubwa kuwa nitapona.
Risasi: Unaenda kusomea nini?
Wakonta: Lengo langu ni kusomea saikolojia, lakini kutokana na elimu yangu kuwa siyo kubwa, nimeona nisome vitu vingine kwanza nipate cheti halafu diploma na baada ya hapo ndiyo nifanye digrii ya saikoloji. Kwa sasa naenda kusomea Marketing and Public Relation.
Risasi: Kwa nini umeamua tena kurudi shule?
Wakonta: Elimu ambayo tunaipata shuleni ni msingi ambao hauepukiki na ni muhimu katika kile tunachokifanya.
Risasi: Nakumbuka Mzee Mengi aliyagusa maisha yako kwa kiasi fulani baada ya wewe kuwa mshindi kwa kuandika wazo zuri la biashara, kifo chake kilikugusa kwa kiasi gani?
Wakonta: Dk. Mengi nilimfahamu kwa kipindi kifupi sana, nilimfahamu kama ni mtu mkarimu mpaka unashangaa kwa nguvu na uwezo aliokuwa nao, si rahisi sana kuongea na mtu vile, ni fundisho kubwa sana ambalo nimelipata, lakini pia ni mtoaji na anatoa kwa moyo hata wewe unayepokea ule msaada unajisikia amani.
Risasi: Ni jambo gani ambalo mliliongea mara ya mwisho kabla ya umauti kumfika?
Wakonta: Kuna tiba fulani ambayo tulikuwa tunaifanya, ambayo ilikuwa niifanye dozi ya pili, lakini kwa bahati mbaya haikufanikiwa.
Risasi: Kuna mwanaume huwa unamposti kwenye akaunti yako, vipi ndiye mchumba wako?
Wakonta: Ndiyo.
Risasi: Je, unaishi naye na mlikutana vipi?
Wakonta: Anaishi Marekani, nilikutana naye tangu mwaka 2017.
Risasi: Ulikutana naye vipi?
Wakonta: Ilikuwa Januari, 2017 nakumbuka siku hiyo nilikuwa sipo vizuri sana, hivyo nikawa sihitaji kupokea simu ya mtu yeyote, ilipofika jioni mdogo wangu aliniletea simu akaniambia dada kuna namba inapiga siielewi, nikamwambia sihitaji kupokea simu, lakini baadaye nikamwambia leta niongee.
Baada ya kupokea akaanza kuniambia Wakonta mambo, nimekuona mtandaoni na nikachukua namba yako sehemu f’lani, mimi naishi Marekani na nafanya kazi na biashara zangu, akawa anaongea kawaida kabisa.
Mwisho wa siku tukawa tumeendelea kuwasiliana kama marafiki. Kuna siku alinipigia simu, akaniambia anahitaji kunioa, nikacheka na kupuuzia kwa sababu nilijua ni utani na jambo lingine lililonifanya nipuuzie ni kwamba sikuwahi kuwa na mpenzi, yeye ndiye alikuwa mpenzi wangu wa kwanza.
Hali iliendelea hadi alipokuja Tanzania, akafika hadi nyumbani kwetu, mwisho nikasema sawa, ngoja nijaribu ndipo tukaingia kwenye uhusiano.
Risasi: Baada ya kukubali, vipi moyoni mwako hukuwahi kuwa na hofu kwamba huenda akaja kubadilika na ukajiuliza kwa nini ameamua kukupenda ukiwa katika hali hiyo?
Wakonta: Binafsi sikuwa nayo, lakini watu wa pembeni ndiyo walikuwa nayo na jambo lingine ambalo nahisi lilinifanya nisijiulize maswali yote hayo ni kwamba sikuwahi kuwa na uzoefu wa maumivu ya mapenzi.
Risasi: Mipango ya ndoa ikoje?
Wakonta: (Anacheka) Hiyo ilikuwa ni gia tu ya kuniingilia, lakini nahisi pia ni kwa sababu mimi huwa sihangaikii sana mambo yajayo, hivyo ikitokea pia akanioa itakuwa vizuri zaidi.
Risasi: Umbali wenu unakuathiri vipi?
Wakonta: Hauniathiri chochote, naona kawaida tu.
Risasi: Huwa mnaonana kila baada ya muda gani?
Wakonta: Alikuja 2017, 2018 alikuja mara mbili, ameondoka mwaka huu mwezi wa nne, pia nadhani atakuja tena mwezi ujao.
Makala: Memorise Richard Simulizi ya binti


Comments are closed.