The House of Favourite Newspapers

Wakuu wa Baraza la Mitihani Kenya Wafutwa Kazi

0

1240400 Waziri wa Waziri wa Usalama na Masuala ya Ndani nchini Kenya, Meja Jenerali Joseph Nkaissery.

Serikali ya Kenya imetangaza kuwafuta kazi maafisa wakuu wa Baraza la Mitihani la nchi hiyo (KNEC) kutokana na visa vya udanganyifu vilivyoripotiwa wakati wa mitihani ya kitaifa mwaka jana.

Waliofutwa kazi ni pamoja na afisa mkuu mtendaji wa baraza hilo Bw. Joseph Kivilu na mwenyekiti wa bodi inayosimamia baraza hilo Bw. Kibiru Kinyanjui.

Bw Kivilu pamoja na maafisa wengine saba wa baraza hilo wametakiwa kuandikisha taarifa kwa polisi mara moja.

Tangazo la kufutwa kwa wakuu hao limetolewa kwenye kikao cha wanahabari kilichoandaliwa na Waziri wa Usalama na Masuala ya Ndani Meja Jenerali Joseph Nkaissery na Waziri wa Elimu, Fred Matiang’i.

KNEC (2)Waziri wa Elimu, Fred Matiang’i, Bw Matiang’i.

Watahiniwa waliopatikana na makosa ya udanganyifu mtihani wa kidato cha nne mwaka 2015 waliongezeka asilimia 70 kutoka mwaka uliotangulia. Katika mtihani wa mwaka 2015, watahiniwa 5,101 waligunduliwa kuwa walitumia udanganyifu katika mtihani.

Mwaka 2014, ni watahiniwa 2,975 pekee waliokuwa wametumia hila katika mtihani huo wakati huo visa vikiwa vimepungua kutoka visa 3,812 mwaka 2013.

Aliyekuwa naibu chansela wa chuo kikuu cha Nairobi Prof George Magoha ameteuliwa kuwa mwenyekiti mpya wa bodi hiyo na ataanza kufanya kazi mara moja.

Muda mfupi baada ya tangazo la kufutwa kwa wakuu hao kutolewa, Wakenya kwenye mitandao ya kijamii wamekuwa wakieleza hisia zao na kitambulisha mada #KNEC kimeanza kuvuma.

Leave A Reply