Wakuu Wa Usalama Barabarani Watakiwa Kusimamia Sheria Na Kanuni Za Usalama Barabarani Kikamilifu

Wakuu wa Usalama Barabarani wa Mikoa na Wilaya wametakiwa kuongeza kasi katika usimamizi wa Sheria, kanuni na taratibu za Usalama Barabani ili kuwadhibiti madereva wanaokiuka sheria hizo na kusababisha ajali za barabarani.
Wito huo umetolewa na Kamishna wa Operesheni na Mafunzo, CP Awadh Juma Haji wakati akifungua kikao kazi cha Wakuu wa Usalama Barabarani wa Mikoa na Wilaya kutoka Tanzania bara na Zanzibar Machi 10, 2025 jijini Dodoma.
CP Awadh alisema kuwa kukiwa na usimamizi mdogo wa Sheria za Usalama Barabarani kutasababisha uwepo wa madereva wazembe ambao watakuwa wanaendesha bila kuzingatia sheria wala kufuata taratibu na kanuni za Usalama Barabarani hivyo kusababisha ajali na matokeo yake ni ongezeko la majeruhi na vifo kwa watumiaji wengine wa barabara.
Pia, aliwasisitiza wakuu hao wa Usalama Barabarani wa Mikoa na Wilaya kuwasimamia vema askari walio chini yao ikiwa ni pamoja na kuwachukulia hatua stahiki wale wanaokiuka maadili ya Jeshi la Polisi kwa kuendekeza rushwa na mengineyo yasiyo na maadili.
Aidha, CP Awadh ameishukuru Serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Rais Mhe. Dkt Samia Saluhu Hassan kwa kazi kubwa aliyoifanya kwa Jeshi la Polisi kwa kuliwezesha vifaa zikiwemo kamera na magari ya doria katika barabara kuu ambayo wanayatumia katika kudhibiti ajali za barabarani.
Wakuu wa usalama barabarani wa mikoa (RTOs) na wa Wilaya (DTOs) wamekutana jijini Dodoma kwa kikao kazi cha siku mbili kuanzia tarehe 10 – 11 Machi, 2025 ambacho kwa ujumla watajadili kwa pamoja changamoto za usalama barabani na kuweka mikakati ya pamoja ya namna ya kutatua changamoto hizo kwa lengo la kudhibiti ajali za barabarani.