The House of Favourite Newspapers

Walanguzi wa Saruji Watangaziwa Kiama

0

WAFANYABIASHARA wanaouza saruji kwa bei ya ulanguzi, wameonywa kuchukuliwa hatua kadhaa, ikiwamo kushtakiwa na kufungiwa biashara. Onyo hilo limetolewa na serikali mkoani Morogoro, kutokana na bidhaa hiyo kuuzwa kwa bei ya juu.

 

Serikali imesema itawachukulia hatua wafanyabiashara wote wa saruji, ambao wanauza bidhaa hiyo kwa bei ya Sh. 25,000 ikiwamo kuwafikisha mahakamani kwa kesi ya uhujumu uchumi.

 

Hayo yalibainishwa jana na Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Loata Ole Sanare, wakati akizungumza na wafanyabiashara wa mkoa huo, kuhusiana na kupanda kwa bei ya saruji bila sababu za msingi.

 

Alisema serikali imefanya uchunguzi na kubaini kuwa Manispaa ya Morogoro ndiyo inaongoza kwa kuuza saruji bei ya juu kulinganisha na maeneo mengine, jambo ambalo haliwezi kukubalika.

 

“Manispaa ya Morogoro ndiyo ya kwanza kupandisha bei, inauzwa kwa bei ya Sh. 25,000… hao wachache wanataka kutuharibia mambo hapa tumeshafanya utafiti na tumewabaini,” alisema Sanare.

 

Alisema kuwa utaratibu wa kuwachukulia hatua wafanyabiashara hao, utaanza muda mfupi baada ya uchunguzi kukamilika, na licha ya kuwafikisha mahakamani pia biashara zao zitafungwa.

 

Aliongeza kuwa ameshatoa maelekezo kwa Mamlaka ya Mapato (TRA) mkoani humo, kwamba atakayekamatwa kwa kosa hilo afutiwe leseni ya kufanya biashara ya saruji.

 

Kwa upande wao baadhi ya wafanyabiashara mkoani Morogoro walioomba serikali kuzuia kusafirishwa saruji nje ya nchi, ili ipatikane kirahisi zikiwa jitihada za kukabiliana na mfumuko wa bei.

 

Thabit Islam, mmoja wa wafanyabiashara hao, alisema kuwa miongoni mwa sababu zinazosababisha kuongezeka kwa gharama ni uwapo wa foleni kubwa viwandani katika upakiaji wa mizigo na kusababisha magari kutumia muda mrefu safarini.

 

“Tunaiomba serikali izuie kuuza nje ili hapa kwetu ipatikane kirahisi, unakuta gari inakaa zaidi ya siku kumi na nne kwenye kiwanda kutokana na magari ya nje ya nchi kuja kwa wingi, kwa sababu kwenye nchi zao huko viwanda vyao vimefungwa kwa sababu bado wanasumbuliwa na magonjwa,” alisema Islam.

Leave A Reply