The House of Favourite Newspapers

Walimu Waitaka Serikali Ilipe Malimbikizo ya Trilioni 1.060/-

cwt

Kaimu Katibu Mkuu wa chama cha Walimu Tanzania (CWT) , Ezekiah Oluoch

CHAMA cha Walimu Tanzania (CWT) kimepongeza jitihada za Serikali ya Awamu ya Tano ya kuanza kulipa madeni ya walimu, lakini imekumbushia deni lake linalofikia Sh trilioni 1.060 kutokana na malimbikizo ya kuanzia mwaka wa fedha wa 2013/14 hadi Desemba mwaka jana.

Hayo yalisemwa Dar es Salaam jana na Kaimu Katibu Mkuu wa chama hicho, Ezekiah Oluoch wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu madai ya walimu na upungufu wa walimu shuleni.

Oluoch alisema kuanzia mwaka wa fedha wa 2013/14 hadi Desemba mwaka jana, katika mwaka wa fedha wa 2016/17 serikali imewalipa walimu 182,882 jumla ya Sh bilioni 124.6 sawa na asilimia 10.5 ya deni linalodaiwa katika kipindi hicho.

Alisema CWT inapongeza jitihada hizo, japokuwa hazijakidhi matarajio ya walimu ya kulipwa kwa asilimia mia.

Akizungumzia deni hilo katika kipindi hicho, alisema limeendelea kukua na kufikia Sh trilioni 1.06 sawa na asilimia 89.5 ya kiasi kilichokuwa kinapaswa kulipwa ambacho hakijalipwa.

Akizungumzia mchanganuo wa madai ya walimu, Oluoch alisema mafao ya walimu wastaafu 6,044 pamoja na tozo ni Sh 556,048,000,000, madeni yasiyohusiana na mishahara zaidi ya walimu 150,000 wanadai jumla ya Sh 180,000,000,000.

Alisema madeni ya mishahara ya walimu waliopandishwa madaraja Januari hadi Machi 2016, walimu 85,945 wanadai jumla ya Sh 301,374,312,000 na kwamba deni hilo linaongezeka kila mwezi kwa kiwango cha Sh 25,114,526,000 kuanzia Januari hii hadi Juni, 2017 ambapo lisipolipwa hadi Juni, 2017 kutakuwa na ongezeko la Sh 150,687,156,000 ambayo haikuingizwa kwenye deni la hadi Desemba, 2016.

Naibu Katibu Mkuu huyo wa CWT alisema ni matumaini yao kuwa serikali itachukua hatua za haraka, kuwalipa walimu madeni yao na kuwaajiri walimu wote waliohitimu, badala ya kuwaacha mitaani ambapo wataajiriwa wakiwa wamesahau mbinu za ufundishaji.

“Walimu wanajua kwamba fedha zipo, kinachotakiwa ni utashi wa Rais John Magufuli. Akiamua hata leo, fedha zote za walimu zitalipwa hata wiki hii,” alisema Oluoch.

Comments are closed.