The House of Favourite Newspapers

Walioathirika Na Mafuriko Hanang Wapewa Mitungi Ya Gesi Ya Kupikia Bure Na Oryx

0
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge na Uratibu Jenista Mhagama ( kushoto) akiwa ameshikana mkono na Mkuu wa Idara ya Mauzo wa Oryx Gas Tanzania Shaban Fundi (kulia) baada ya Oryx kukabidhi mitungi 200 ya kilo 15 yakiwa na majiko yake kwa ajili ya waathirika wa mafuriko yaliyotokea Katesh.

Wakati nchi ikiendelea na maombolezo ya vifo, majeruhi, uharibifu wa mali kufuatia janga la maporomoko ya tope na mafuriko yaliyotokea wilayani Hanang, Mkoa wa Manyara kampuni ya Oryx Gas imefikilia busara ya kuwapunguzia ugumu wa maisha wakazi waliokuwa wakiishi maeneo hayo na kunusurika.

Katika kuunga mkono kuwafariji wananchi hao, Kampuni ya Oryx Gas Tanzania imetoa pole kwa wananchi hao kwa kutoa mitungi ya gesi 200 yenye ujazo wa kilo 15 kuwasaidia katika kipindi hiki kigumu.

Mitungi hiyo ya gesi ikiwa na majiko yake, imekabidhiwa kwa serikali kupitia kwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge na Uratibu, Jenista Mhagama na kushuhudiwa na Mkuu wa Mkoa wa Manyara, Queen Sendiga.

Akizungumza wakati wa kupokea mitungi hiyo, Waziri Mhagama ameishukuru Kampuni ya Oryx kwa mchango wake kwa wananchi wa Hanang kwani umekuja wakati muafaka kusaidia wananchi hao kwa kuwapatia nishati safi ya kupikia katika wakati huu mgumu.

Mkuu wa Idara ya Mauzo wa Kampuni ya Oryx Gas, Shaban Fundi amesema kampuni hiyo imefika Hanang Katesh kuungana na kuwapa pole Watanzania wenzao waliofikwa na janga la mafuriko na maporomoko.

“Tunajua kwa hakika wenzetu wameathirika sana katika kipindi hiki ni gharama kubwa kupata vyanzo vya moto kupikia. Oryx Gas tumekuja kukabidhi majiko 200 na mitungi ya gesi ujazo wa kilo 15 kwa waathirika wa tukio hili.

“Oryx Gas tunawaombea marehemu wapumzike kwa amani, zaidi tunawaombea majeruhi wote wapone haraka na werejee katika majukumu yao ya kila siku.”

Fundi amesisitiza kuwa kampuni hiyo itaendelea kuwa karibu na jamii ya Watanzania katika nyakati zote zikiwemo za majanga kuhakikisha wanakuwa sehemu ya kusaidia ufumbuzi wa changamoto ya matumizi ya nishati safi ya kupikia.

Leave A Reply