TAARIFA mpya kutoka Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), inasema idadi ya watu waliopoteza maisha kwenye ajali ya moto iliyotokea juzi Jumamosi, Agosti 10, 2019, mkoani Morogoro nchini Tanzania imefika 75.
Idadi hiyo imeongezeka baada ya majeruhi wengine wanne kufariki dunia katika Hospitali ya Muhimbili jijini Dar es Salaam walikohamishiwa kwa matibabu zaidi.
Muhimbili ilipokea majeruhi 46 kutoka Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Morogoro kwa ajili ya matibabu zaidi, hata hivyo, saba kati yao wamefariki.
Akitoa taarifa kuhusu majeruhi wa tukio hilo, leo Jumatatu Agosti 12, 2019, Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano wa Hospitali hiyo, Aminiel Aligaesha, amesema kwa sasa idadi ya majeruhi wanaoendelea kupatiwa matibabu ni 39.
“Tumepoteza wenzetu wengine wanne na miili yao imehifadhiwa katika chumba cha kuhifadhia maiti, hivyo kama kuna ndugu wa karibu waje kwa ajili ya kuwatambua ndugu zao,” amesema.
Kuhusu hali za majeruhi, amesema wanaendelea vizuri na wapo wanaoonyesha matumaini ya kupona.
Comments are closed.