The House of Favourite Newspapers

Waliohukumiwa Kunyongwa Wanyongwe Au Adhabu Ya Kifo Ifutwe!

hands of a prisoner on prison bars

MWANDISHI wa safu hii aliwahi kuandika mwaka jana katika gazeti la ‘Uwazi Mizengwe’  moja ya magazeti ya kampuni yenye kutukuka kwa habari motomoto ya  Global Publishers Limited akizungumzia suala hilihili.

Mwandishi huyohuyo mwaka huu akiwa katika Gereza Kuu la Ukonga aliwahi kukutana na kuziona nyuso za watu waliohukumiwa kunyongwa kwa ajili ya makosa yanayotokana na kuua binadamu wenzao wakati wao wakiendelea kuishi!

Alikutana na watu hao katika moja ya magereza yaliyopo nchini, akaziona sura zao zenye furaha na majuto kwa waliyofanya na kusababisha kujikuta wakiwa katika kuta hizo ngumu za simenti katika magereza,  baadhi yao wakiwa wameingia humo wakiwa bado vijana wakitegemea kuoa na kuanzisha familia baadaye.

Kama walifanya hivyo kwa makusudi au kwa kutodhamiria, mwandishi wa safu hii hajui, lakini anafahamu kwamba watu hao walihukumiwa kunyongwa mpaka wafe kutokana na ushahidi uliopatikana mahakamani.

Watu aliowaona mwandishi wa safu hii mwaka huu ni baadhi ya watu zaidi ya 470 nchini  ambao wanasubiri, wamesubiri, walisubiri kwa miaka nenda-rudi kunyongwa. Ajabu ni kwamba adhabu hiyo kwa kiasi kikubwa haijatekelezwa.  Miongoni mwa watu ambao mwandishi wa safu hii aliwaona ni mtu ambaye amekuwa akisubiri kunyongwa tangu mwaka 1973!

death-penalty 

Mtu huyo ambaye alifanya kosa la kumwondoa binadamu mwenzake uhai  tangu mwaka huo ikiwa imepita miaka ipatayo 43 hadi leo hii ni mtu mzima, ni mzee wa miaka zaidi ya 60 akisubiri kunyongwa! 

Kwa nini watu hao walioua wanadamu wenzao wanaendelea kuteseka na kusubiri kunyongwa kwa miaka nenda-rudi?  Ni kwa vile watu wanaotakiwa kukamilisha mchakato wa watu hao kunyongwa  – kwa mujibu wa sheria na katiba ya nchi hii —  ni marais wa nchi hii, tangu enzi ya Julius Nyerere hadi John Magufuli!

Nyerere aliwahi kukiri kwamba alitia saini ya watu watatu kunyongwa, rais aliyemfuatia, Ali Hassan Mwinyi, hakuwahi kusema ‘alinyonga’ watu wangapi.  Vivyo hivyo Mkapa na Kikwete.

Jambo la wazi ambalo kila mtu aliye nje ya nyumba ya wagonjwa wa akili analifahamu ni kwamba marais wa nchi hii hawataki au wanaogopa kubeba lawama kwamba waliidhinisha watu kunyongwa.  Pamoja na ushahidi wote uliopatikana mahakamani, wamekuwa wanasita kuidhinisha kuuawa kwa watu ambao waliua binadamu wenzao!  Kwa nini wanasita?  Wanajua wao!

Hii ni pamoja na taasisi ambazo zinawatetea wauaji wa binadamu wenzao wasiuawe. 

death-penalty-injection

Kwa nini zinafanya hivyo?  Huenda ni kwa ajili ya huruma ya kuendeleza maisha ya binadamu.  Huenda pia ni kwa sababu wanaotetea wauaji wasiuawe, hawajawahi kupotolewa na ndugu waliouawa na binadamu wenzao ambao (wauaji) wanaendelea kuishi kwa furaha na kuwaacha waliopoteza ndugu zao wakiishi katika simanzi zisizokwisha huku wakikumbuka ndugu zao waliouawa kikatili!

Yote kwa yote, iwapo kweli binadamu wote – marais na wananchi wa Tanzania – hawataki wauaji nao wakauawa, basi sheria ibadilishwe wauaji wapewe adhabu nyingine ambayo inaendana na huruma ya watu ambao hawataki wauaji wakauawa.

death

Kama tunawahurumia walioua binadamu wenzao, basi tukiri kabisa kwamba binadamu kuua binadamu mwenzake, si lazima auawe!  Nchi kadhaa duniani zimeifuta adhabu ya muuaji kuuawa.  Kama adhabu hiyo inakiuka upendo, huruma na utukufu wa mbingu na ardhi, basi ifutwe leo na si kesho ili, pamoja na mambo mengine, wauaji wasiwe na mashaka ya kuuawa pindi wanapoua!

Kama marais wanaogopa kuidhinisha kunyongwa kwa watu ‘walionyonga’ wenzao, basi sheria hiyo ibadilishwe angalau waachiwe mahakimu waliogundua uovu huo wawe watu wa mwisho kuidhinisha hukumu hiyo.  La sivyo sheria ya kifo ifutwe kuliko kuwapa faraja watu ambao hawajapoteza ndugu zao kutetea watu waliopoteza roho za watu wengine!

Makala na Walusanga Ndaki

Comments are closed.