The House of Favourite Newspapers

Walishtuka Wakasepa, Wakatusua

0

MVUTO wa makundi mengi yanayofanya Bongo Fleva umekuwa ukipungua kila siku huku namba ya wasanii ambao wanafanya muziki wa peke yao (solo artist) ikiongezeka.

 

Ongezeko hilo linaifanya tasnia hiyo kuwa na ushindani mkubwa ambapo kila mmoja anafanya kile kilicho bora kwa ajili ya kuwateka mashabiki.


Nyuma kidogo kulikuwa na makundi mengi ambayo yalitikisa, baadhi ni Hard Blasters Crew (HBC), TMK Wanaume Family, Wateule, Daz Nundaz, Nako 2 Nako, hivi karibuni kulikuwa na Yamoto Band, Weusi na mengine kadhaa.

 

Championi Ijumaa, linakuchambulia baadhi ya wasanii ambao walijitoa kwenye makundi kisha mambo yakawaendea vyema na kuteka nyoyo za wapenda burudani wengi:

Aslay

Ndiye habari ya mjini kama utazungumzia wasanii ambao wapo ‘hot’ kutokana na mfululizo wa ngoma zake anazotoa ambazo zote ni kali na zilizopokelewa vizuri na mashabiki wake.

Kwa miaka ya hivi karibuni uwezo wake ulikuwa unamezwa na Yamoto Band iliyoundwa na Enock Bella, Beka Flavour na Maromboso.

Kuanzia Angekuona, Mhudumu, Baby, Likizo, Pusha, Rudi, Koko Tu, Tete hadi sasa Natamba, nyota yake inazidi kung’ara kila siku akiwa mwenyewe tofauti na zamani.

Kassim Mganga

Awena ndiyo wimbo ambao ulimfanya wapenda burudani wengi wamtambue kijana huyu mwenye asili ya Tanga, baada ya kufanya vizuri kwa kipindi kirefu Kassim akaangukia Tip Top Connection, alikaa kwa muda kabla ya kuangalia upepo unapoenda kwa kung’atuka kwenye kundi hilo.

Kama ilivyo kwa Aslay, Kassim naye baada ya kujitoa kwenye kundi amekuwa aking’ara na kubamba vilivyo kwa mashabiki mbalimbali wanaofutilia mziki huo ambao kwa sasa anaimba nyimbo zenye asili ya Pwani.

AY na Mwana FA

Wana ambao wamekula wote msoto wa Bongo Fleva tangu miaka ya nyuma kabla ya baadaye kuja kutusua kwenye fani hiyo. Ambwene Yessaya ‘AY’ na Hamis Mwinjuma ‘Mwana FA’ walianza harakati zao kivyao, baadaye wakajiunga na East Coast Team chini ya GK wakiwa na wenzao kadhaa kina Snare, Buff G na O-Ten. Walipochomoka hapo majina yao na kazi zao zikapata umaarufu mkubwa.

Ditto

Weka pembeni kabisa Moyo Sukuma Damu kisha rejea kwenye Wimbo wa Darubini na kusikiliza sauti ambayo ilikuwa inapishana mistari na mfalme wa Morogoro, Seleman Msindi (Afande Sele) kama hutakuwa hujui sauti hiyo basi huyo ni Ditto ambaye alianza kupata umaarufu mkubwa akiwa na Kundi la Watu Pori ambalo lilijichimbia mkoani Morogoro.

Baada ya ‘kuhit’ na Watu Pori, Ditto akaamua kuchukua hamsini zake kwa kuwa solo artist na tangu kipindi hiko amekuwa akikamua vilivyo kiasi cha kuwakamata wale mashabiki waliokuwa wanamsapoti kwa kipindi hicho hadi sasa.

Profesa Jay

Wahenga wanamjua kama Nigger Jay, Jay wa Mitulinga, wale wa kizazi cha ‘dot com’ wamemfaidi zaidi alipobadili jina na kujiita Profesa Jay, jina lake halisi ni Joseph Haule na kwa sasa ni Mbunge wa Mikumi, lakini alianza fani akiwa chini ya Hard Blasters, baada ya kujitoa jina lake likawa kubwa zaidi na zaidi.

Shaa

Kipaji chake kilionekana kwenye shindano la kuibua vipaji la Cocacola Popstar ambapo yeye alikuwa mmoja wa washindi akiwa na wenzake, Witness na Langa Kileo (marehemu), kwa umoja wao wakazaa Kundi la Wakilisha lililokuja kutoa ngoma ya Hoi ambayo ilisumbua kwa miaka hiyo.

Shaa naye aliamua kula kona na kulipa kundi lake kisogo na kugeukia kufanya nyimbo akiwa mwenyewe na kweli tangu ajitenge amefanikiwa kwa kiasi kikubwa.

Chris-tian Bella

Mfalme wa Masauti ndiyo jina ambalo mashabiki wake wanamuita mara nyingi ambalo hubeba ule utamu wa sauti yake ambayo inanogesha nyimbo mbalimbali.

Umaarufu mkubwa aliupata akiwa na Bendi ya Akudo Impact ambayo ilikusanya vichwa kama Tasis Masela na Canal Top, lakini Bella aliamua kuchapa lapa kwenye bendi hiyo na kufanya kazi peke yake na tangu achukue uamuzi huo hajawahi kurudi nyuma kutokana na mafanikio ambayo alijipatia.

Makala Said Ally,Dar es Salaam

Leave A Reply