The House of Favourite Newspapers
gunners X

Walter chilambo: Chuki, majivuno vimetawala mastaa wa Injili

0

ANAITWA Walter Chilambo, msanii aliyepata umaarufu baada ya kuibuka mshindi kwenye mashindano ya kusaka vipaji vya kuimba ya Bongo Star Search mwaka 2012. Baada ya hapo aliendelea na gemu ya Bongo Fleva na akaachia ngoma yake iliyofanya vyema iliyoitwa Siachi. Hakuishia katika Bongo Fleva kwa wakati mrefu, akabadilisha mawazo na kuhamia katika muziki wa Injili.

Only You ndio jina la kazi ya kwanza iliyomtambulisha vyema katika muziki huo na mashabiki wakampokea vizuri kutokana na sauti yake ya kuvutia na uandishi mzuri wa mashairi yake, sasa anaendelea kukinukisha na wimbo wake mpya unaoitwa Lord Of Mercy.

Risasi Vibes ilipiga stori na Chilambo kuhusu mambo mbalimbali yanayohusu kazi na maisha yake binafsi, karibu:

Risasi Vibes: Hongera sana kwa ujio wako mpya, wimbo ni mzuri. Kipi kilikufanya ukakaa kimya?

Chilambo: Ahsante, ni maandalizi tu. Kwanza nilikuwa nafanya marekebisho ya studio yangu inayoitwa Love Record ambayo mimi ndio producer hapa lakini pia nilikua nawaandalia kitu cha tofauti mashabiki zangu.

Risasi Vibes: Wewe ni moja ya mazao ya Bongo Star Search, unazungumziaje shindano hilo kwa sasa?

Chilambo: Kwanza kabisa nashukuru timu nzima ambayo iliandaa mashindano yale kwani ndio njia iliyotufanya tukapata majina na mpaka sasa bado tupo, ila naona kipindi kile yalikuwa bora kuliko sasa kwani hata ukiangalia vipaji vilikuwa vingi na bado vinaishi. Lakini sasa hivi mashindano yakiisha hatuwaoni na wao wanapotea.

Risasi Vibes: Ni kipi hasa kilikufanya ghafla ukaacha muziki wa Bongo Fleva na kuhamia muziki wa Injili?

Chilambo: Ni wito tu, niliitwa kufanya kazi ya Mungu nikaitika na wala hakuna mtu yeyote aliyenishawishi.

Risasi Vibes: Mashabiki wako walipokeaje taarifa za wewe kuimba Injili.

Chilambo: Nashukuru mimi ni miongoni mwa wasanii wa Gospo ambao nyimbo zinasikilizwa na watu wa dini tofautitofauti, awali walishtuka lakini nashukuru bado wanaendelea kuwa na mimi na wanasapoti sana kazi zangu.

Risasi: Je una mpango wowote wa kurudi kuimba Bongo Fleva.

Chilambo: Huko mimi sipo tena, sina mpango wa kurudi. Nimeamua kumtumikia Mungu tu.

Risasi Vibes: Wewe ni muimbaji na muandishi mzuri sana, vipi tangu uanze kuimba Injili umeshamuandikia wimbo msanii yeyote wa Bongo Fleva?

Chilambo: Wakati naanza kuimba Gospo nilikuwa nawaandikia wasanii wengi tu hasahasa Jux, nyimbo zake nyingi nimeandika mimi lakini kwa sasa nimeacha kabisa japo bado nina nyimbo za namna hiyo ambazo nilizirekodi kitambo ila sina mpango wa kuziachia.

Risasi Vibes: Kuna madai kuwa wasanii wa Injili ambao kidogo wapo juu wanaringa na wanajitenga, je kuna ukweli wowote juu ya hilo?

Chilambo: Ukweli upo tena mkubwa sana na si kujitenga tu, upendo baina yetu hakuna, chuki imetawala. Msanii akishapata kaumaarufu kidogo tu akawa na kagari, anasahau hata Mungu aliyemuinua, maringo yanakuwa mengi sijui hata wanamtumikia Mungu gani.

Risasi Vibes: Vipi unaweza kuwataja angalau wawili ili waweze kujirekebisha.

Chilambo: Hahahahaha kaka hiyo vita sasa, siwezi kuwataja lakini wanajijua, kwa kusema hivi nina imani kabisa ujumbe utawafikia.

Risasi Vibes: Ni msanii gani ndani na nje ya Tanzania anayekupa hamasa kila ukimtazama na una ndoto za kufanya naye kazi?

Chilambo: Kaka unanipa changamoto sana, kiufupi mimi mwenyewe nyimbo zangu huwa sizisikilizi sana, huwa naachia tu halafu namuomba Mungu ifike mahala sahihi. So siyo msikilizaji mkubwa wa wasanii, wa hapa nyumbani huwa nasikiliza tu kujifunza kitu, kuhusu kazi huwa natamani sana kufanya kazi na wasanii kutoka nje ya Tanzania na wanaofanya vitu vikubwa kama kina Glorious Salivation, The Spirit na wengine wengi kutoka Afrika Kusini.

Risasi Vibes: Tunaona muziki wa Injili kutoka nje hasa Afrika Kusini na Nigeria unapenya sana Bongo, vipi kwa upande wenu tatizo ni nini maana tunaona mnafanya vizuri hapa nyumbani pekee?

Chilambo: Kwanza ni kutojitambua kwa wasanii wengi wa Gospo, wengi siyo wafuatiliaji wazuri wa kazi zao hata kuzifanyia promo katika mitandao ya kijamii hawawezi, na kuna wasanii wengi hata account za YouTube hawana, nyimbo zao wanaweka kwenye account za watu wengine.

Risasi Vibes: Nyie kama wasanii wa Injili mna mikakati gani ya kuhakikisha Gospo kutoka Tanzania inapaa zaidi Kimataifa?

Chilambo: Siwezi zungumzia wengine lakini binafsi nyimbo zangu nyingi feedback napata kutoka nje, hapa Tanzania siyo sana. Napokea simu nyingi kutoka nje, lakini hata comment nyingi katika mitandao ya kijamii zinatoka nje ya Tanzania. Nimejipanga kujitangaza zaidi kimataifa.

Risasi Vibes: Tangu umeanza kufanya muziki, kuna kitu gani hasa ambacho unajivunia mpaka sasa?

Chilambo: Kwanza kabisa ninachojivunia ni ndoa, nimeingia huku tu Mungu akanipa mke. Moja ya watu ambao wananishauri mambo mengi ya kunijenga na kunipa heshima.

Risasi Vibes: Kumekuwa na jinamizi la ndoa za mastaa wengi kuvunjika, wewe kama miongoni mwa wasanii walioko kwenye ndoa unafanya nini kuhakikisha unadumu?

Chilambo: Hawamtangulizi Mungu katika kuliendea jambo hilo, ndoa ni maombi, Mungu akupe mke siyo umchague kwa akili yako. Mke mwema anatoka kwa Bwana. Mimi naamini huyu nimechaguliwa na Mungu na ndiye atakayeisimamia ndoa yangu na itadumu milele. Mbali na kutimiza majukumu yangu kama mume, nafanya sana maombi.

Risasi vibes: Unazungumziaje baadhi ya mashabiki kusema kuwa umeoa mwanamke aliyekuzidi umri na hamuendani?

Chilambo: Hakuna kitu kama hicho, kwanza naomba watambue kuwa mke wangu ni mdogo kwangu, ni umbo tu na ni mtu sahihi kwangu na ndio maana ni mke wangu, nampenda sana.

Risasi vibes: Unawaahidi nini mashabiki wako?

Chilambo: Hawatajuta kuwa mashabiki wangu, waendelee kunisapoti na ninawapenda sana.

Leave A Reply