The House of Favourite Newspapers

WALTER, KADJA NITO; BONGO FLEVA BAHATI MBAYA?

Walter Chilambo

KABLA ya kuanza kuimba, staa wa Bongo Fleva, Nasibu Abdul ‘Diamond Platnumz’ alianza kwa kurap.

 

Kipaji hicho cha kurap ndicho kilichomkutanisha na Prodyuza Bob Junior wa Sharobaro Records lakini baadaye prodyuza huyo hakupendezwa na kurap kwake na kumuomba afanye nyimbo za kuimba ndipo zilipozaliwa nyimbo za Kamwambie na Mbagala.

 

Ukizungumzia Diamond kwenye Muziki wa Bongo Fleva ni wazi utamzungumzia Diamond wa kuimba na siyo kurap tena. Kumbe kule kwenye kurap ilikuwa bahati mbaya lakini mafanikio yake yalikuwa kwenye kuimba maana baada ya kufanya hivyo, ametusua kinomanoma!

 

Kwa kawaida wasanii huwa wana-badilika badilika kulingana na vipaji vyao au furaha ya mioyo yao na ndio maana najaribu kujiuliza, wanamuziki waliowahi kutamba kwenye Bongo Fleva, Walter Chilambo na Kadja Nito ambao sasa wanafanya muziki wa Injili, awali walikosea?

 

Kadja alipata kuusumbua ulimwengu wa Bongo Fleva na kibao chake cha Maumivu, Si Ulisema na Sina Maringo lakini miaka ya hivi karibuni, amebadili uelekeo na kuimba wimbo wa Injili unaojulikana kama Mfariji. Mapema mwaka jana, alianza kuusumbua ulimwengu wa muziki wa Injili baada ya kufanya kava ya Wimbo wa Shukurani wa mwanamuziki Goodluck Gozbert.

 

Kadja ambaye alikuwa ni zao la Jumba la Vipaji Tanzania (T.H.T), mapema mwaka huu amepokelewa vyema kwenye Muziki wa Injili kutokana na wimbo kugusa wengi na mastaa mbalimbali wamejikuta wakiuposti bila kupenda kwenye mitandao yao ya kijamii.

 

Awali, mwanamuziki huyu alikuwa akiimba nyimbo zake za kwa hisia kabisa na kuoenesha wazi kipaji cha Muziki wa Bongo Fleva lakini aliweza kubadilika kama kinyonga baada ya kubadilisha dini kisha kuokoka.

Related image

Mbali na kubadili aina ya muziki na kuokoka, maisha ya mrembo huyo yalibadilika jumla kwani alibadili jina baada ya kuolewa na jamaa anayefahamika kwa jina la Lisimo na sasa Kadja anaitwa Natasha Lisimo. Kama hiyo haitoshi, Natasha alibadili pia aina ya mavazi na kuanza kuimba kwenye majukwaa kwenye kumbi za kanisa au mikutano ya Injili.

 

Akizungumzia mabadiliko hayo ya kimaisha, Natasha anasema ni mipango ya Mungu na anamshukuru kwa kuonesha mahali pake sahihi tofauti na kule alikokuwa. “Kila mtu Mungu amempangia sehemu yake sahihi hapa nilipo mimi ndipo nastahili kabisa nafanya kazi ya Mungu kwa kumsifu na nyimbo zangu,” anasema Natasha.

 

Ukiachana na Natasha, mwanamuziki mwingine aliyetoka kwenye Bongo Fleva na kwenda kwenye Injili ni Walter Chilambo, ambaye pia ni mshindi wa Shindano la Bongo Star Search (BSS) 2013.

 

Mkali huyu alianza vizuri kupitia Bongo Fleva na kufanikiwa kutoa nyimbo ambayo ilitikisa kidogo ya Siachi lakini hata hivyo, aliamua kukacha muziki huo wa kidunia na kuhamia kwenye Injili na kuibuka na nyimbo kibao nzuri kama Only You, Najiona na Siri huku akisema kuwa japokuwa muziki huo haumuingizii fedha lakini ana imani anafanya kitu anachopenda toka ndani ya moyo.

 

Chilambo anasema kuwa, Bongo Fleva alikuwa akifanya lakini moyo wake wote ulikuwa kwenye nyimbo za Injili kwani alipokuwa kwenye muziki wa kidunia hakuwa na mashabiki wengi kama ilivyokuwa hivi sasa kwenye Muziki wa Injili.

 

“Sasa hivi ninaona kabisa hata watu wameongezeka na nimekuwa nikisafiri sana sehemu mbalimbali kwa ajili ya muziki huu wa Injili ingawa huku hakulipi badala yake umjue Mungu zaidi ndio faida yake kwa njia ambayo atakuongoza wewe,” anasema Walter.

 

Wabongo wengi wamewapokea vizuri wasanii hawa katika upande wa Injili lakini bado baadhi ya watu wana wasiwasi kwamba hawawezi kurejea kwenye muziki wa kidunia kwani ipo mifano ya baadhi ya wasanii akiwemo Stara Thomas ambaye alianzia kwenye Bongo Fleva, akaingia Injili kisha akarejea tena kwenye Bongo Fleva!

Comments are closed.