The House of Favourite Newspapers

WAMEPIGA TATU LIGI YA WANAWAKE

MZUNGUKO wa pili wa Ligi ya Wanawake inayodhamini na bia ya Serengeti Lite unazidi kushika kasi kwa timu shiriki kupambana kuchukua pointi kwa mpinzani wake.

 

Mzunguko huu umekuja na utamu wa aina yake kwani kando ya kuwania pointi kuna bonge la vita kwa wachezaji kuwania kiatu cha ufungaji.

 

Kwa sasa staa wa JKT Queens, Fatuma Mustapha ndiye anaongoza akifuatiwa kwa ukaribu na Asha Rashid ‘Mwalala’. Katika vita ya wawili hawa kila mara wamekuwa wakifunga mabao mengi kila wanapopata nafasi.

 

Miongoni mwa mabao mengi ambayo wameyafunga ni pamoja na yale matatu ‘hat trick’ ambayo licha ya kuwaongezea idadi ya mabao waliyonayo pia wamefanikiwa kuchukua mipira.

 

Je unajua nje ya Fatuma na Asha nani mwingine amefunga mabao hayo matatu ‘hat trick’? Makala haya yanakupa orodha ya wachezaji ambao wamepiga mabao matatu.

FATUMA MUSTAPHA – JKT QUEENS

Huyu ndiye wa kwanza kufunga mabao matatu kwenye ligi hii ya Wanawake. Fatuma ambaye ni straika kiwembe wa JKT Queens hadi sasa amefunga ‘hat trick’ tano.

Hat trick hizo tano zenye mabao 15 jumla kwa kiasi kikubwa ndizo zimempa nafasi ya kuongoza kwenye chati ya wafungaji akiwa na mabao 22.

 

ASHA HAMZA – SISTERZ

Nahodha huyu msaidizi wa Kigoma Sisterz ndiye anamkimbiza Fatuma katika suala zima la kufunga hat trick kwenye ligi hiyo ya wanawake. Asha maarufu kama Kadosho ameshajikusanyia mipira miwili hadi sasa baada ya kufunga hat trick mbili.

 

ASHA RASHID – JKT QUEENS

Huyu ni pacha wa Fatuma ndani ya kikosi cha JKT Queens, lakini pia ni mshindani wake katika kusaka kiatu cha ufungaji bora. Ushindani wao hauishii tu katika mbio za kiatu kwani hadi huku kwenye kutupia mabao matatu ndani ya mechi moja napo wanachuana.

Asha hadi mzunguko wa 13 unakamilika ana hat trick mbili tu akiwa amepitwa kwa hat trick tatu na Fatuma.

DONISIA MINJA – JKT QUEENS

JKT Queens kwenye ligi hii ni kama wamekosa mpinzani kwani hawajafungwa, wana mabao mengi, wana kinara wa mabao na pia wanaongoza kwa kufunga mabao matatu kwa mechi moja.

Nje ya Asha na Fatuma, JKT wanaye Donisia Minja ambaye naye yumo kwenye chati ya waliowatungua makipa mabao matatu katika mechi moja. Donisia ana hat trick mbili.

 

MWANAHAMISI OMARI – SIMBA

Nahodha wa Simba Queens, Mwanahamisi Omari ‘Gaucho’ naye hayupo mbali kwa wale ambao wamewatesa makipa kwa kuwapiga mabao matatu. Mwanahamisi ambaye alitwaa ubingwa wa ligi hii akiwa na Mlandizi Queens misimu miwili nyuma, yeye ana hat trick moja.

 

FAUSTA THOMAS – YANGA

Tangu kuanza kwa mzunguko wa pili wa ligi hii ya wanawake, Yanga Princess wameamka kinoma na kushinda mechi zao mbili walizocheza ikiwa tofauti na mzunguko ule wa kwanza.

Staa wao Fausta ni miongoni mwa nyota walioondoka na mipira kwenye mechi baada ya kufunga hat trick moja.

 

AMINA RAMADHAN – SIMBA

Nje ya JKT Queens, Simba ni timu nyingine ambayo ina wafungaji wengi wa hat trick katika ligi hii ya wanawake. Simba yenyewe ina wawili huku JKT ikiwa na wanne.

Nje ya Mwanahamisi, Amina naye ni nyota wa Simba ambaye ameweka kambani mabao matatu katika ligi hii. Amina kapiga hat trick moja.

 

STUMAI ABDALLAH – JKT

Winga huyu wa JKT Queens anafunga pazia la nyota waliofunga hat trick wanaokitifua katika ligi hii ya wanawake. Stumai yeye ana hat trick yake moja tu.

Stori: Said Ally, Dar es Salaam

Comments are closed.