The House of Favourite Newspapers

Wamepitia Magumu, Wakasimama Tena!

KATIKA maisha kuna vipindi vya furaha na huzuni. Kuna wakati binadamu anapitia maisha magumu mno na kujikuta akijiuliza amemkosea nini Muumba wake licha ya kwamba wakati wa furaha wengi wetu tunasahau kabisa kwamba ipo siku zitakuja nyakati za taabu na shida.

 

Kama ilivyo kwa watu wa kawaida ambao wanapitia nyakati ngumu maishani kama kusumbuliwa na magonjwa, kufungwa gerezani na misukosuko ya kila namna, hata kwa mastaa nako hali hii ipo kwa sababu nao ni binadamu.

WEMA SEPETU

Mwanadada huyu ambaye ni Miss Tanzania 2006 aliye pia staa mkubwa wa filamu za Kibongo, amekuwa akipitia mapito magumu ya kupatwa na misala ya kutupwa lupango na kuburuzwa kortini kwa kesi mbalimbali.

Wema amepitia misala mingi ya polisi, lakini katika siku za hivi karibuni imefululiza kwani mpaka sasa anakabiliwa na kesi inayoendelea

mahakamani ya kusambaza picha za ngoni.

 

Mwaka jana Wema alikabiliwa na kesi ya kukutwa na madawa ya kulevya ambapo alihukumiwa miaka miwili jela au faini ya shilingi milioni mbili ambapo alilipa kiasi hicho cha pesa na kuachiwa huru.

 

Mwishoni mwa mwaka jana huohuo aliingia kwenye msala mwingine wa kusambaza picha za ngono ambapo kesi inaendelea kwenye Mahakama ya Hakimu Mkazi, Kisutu jijini Dar na wiki iliyopita alipelekwa katika Gereza la Segerea na kukaa siku saba kwa kosa la kukiuka dhamana.

ELIZABETH MICHAEL ‘LULU’

Lulu ambaye akiwa na umri mdogo, mwaka 2012 alijikuta kwenye wakati mgumu baada ya kushtakiwa kwa kosa la kuua bila kukusudia aliyekuwa staa mkubwa wa filamu Bongo, Steven Kanumba.

Kutokana na kesi hiyo, mwaka 2017, Mahakama Kuu ilimuhukumu Lulu kwenda gerezani miaka miwili baada ya kukutwa na hatia.

 

Mungu akawa upande wake ambapo Mei, mwaka 2018 alibadilishiwa kifungo na kutumikia kifungo cha nje hadi alipomaliza Novemba, mwaka jana.

Lulu kwa sasa yupo huru na anaendelea na maisha yake kwa furaha na amani.

KAJALA MASANJA

Licha ya kwamba kwa sasa yupo vizuri na anafurahia maisha kama kawaida, Kajala ambaye ni staa wa filamu amewahi kuonja magumu kutokana na kuswekwa lupango.

Mwaka 2013, Kajala alihukumiwa kwenda jela miaka 7 au kulipa faini ya shilingi milioni 13 kwa kesi ya kuuza nyumba iliyowekwa kizuizini na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru).

Kajala aliponea chupuchupu baada ya kuokolewa na aliyekuwa shoga’ke, Wema Sepetu ambaye alimlipia shilingi milioni 13 na kuachiwa huru baada ya kusota Segerea kwa muda mrefu.

WASTARA JUMA

Mwanamama huyu anayefanya vizuri kwenye filamu za Kibongo ameingia kwenye orodha hii kutokana na kupitia kwenye misukosuko mingi ya kuugua.

Wastara alipata ajali na kuvunjika mguu ambapo ulikatwa na mpaka sasa anatumia wa bandia. Mguu huo umekuwa ukimsumbua mara kwa mara kiasi cha kufikia hatua ya kuomba michango kwa Watanzania kwa ajili ya matibabu aliyoenda kufanyiwa nchini India.

OMARY NYEMBO ‘OMMY DIMPOZ’

Mwanamuziki huyu wa Bongo Fleva naye amepitia kwenye wakati mgumu kutokana na kuugua kwa muda mrefu ambapo alikuwa akisumbuliwa na koo.

Baada ya kutibiwa hapa nchini Tanzania, Dimpoz alienda nchini Afrika Kusini alikogundulika kuwa alikunywa kimiminika chenye sumu ambapo alizidiwa na kulazwa ICU.

Dimpoz alifanyiwa oparesheni kubwa ya koo na sasa anaendelea vizuri na anafanya kazi zake za kimuziki kama kawaida.

Makala: GLADNESS MALLYA

Comments are closed.