Wami/Ruvu Kuwaondoa Wanaoishi Chini Ya Daraja La Mto Morogoro
Morogoro, 27 Aprili 2023: Bodi ya Maji Bonde la Wami Ruvu imeanza oparesheni ya kusafisha mito iliyopo mkoani Morogoro pamoja na kuwaondoa watu walioweka makazi katika maeneo ya madaraja na kusababisha uharibifu mkubwa wa vyanzo vya maji na kuhatarisha usalama wa madaraja hayo.
Katika opareheni hiyo jumla ya vijana 08 wanaosadikika kutumia madawa ya kulevya walikutwa wakiwa wameweka makazi chini ya daraja la Mwere katika mto Morogoro.
Vijana hao walidai sababu ya wao kuweka makazi katika eneo hilo ni kutokana na kukosa makazi ya kudumu hali inayosababishwa na ugumu wa maisha kwasababu wametoka katika maeneo mbalimbali nje ya mji wa Morogoro na walifika mji huu kutafuta maisha wengine wakiwa hawana ndugu.
“Nilifika mji huu miaka miwili iliyopita kwaajili ya kutafuta maisha ndipo nikajikuta naingia kwenye kazi ya kuokota makopo na kwakuwa sikuwa na pakuishi nikaungana na wenzangu kuishi chini ya daraja hili” alisema Rashid Yassin.
Rashid aliendelea kusimulia kuwa changamoto za maisha ndio chanzo cha yeye kukosa makazi ya kudumu na kusababisha aweke makazi katika eneo hilo kwasababu hana ndugu yeyote zaidi ya ndugu zake aliowaacha kijijini kwao Mgeta Halmashauri ya Morogoro.
Martin Kasambala, Meneja wa Rasilimali za Maji Bodi ya Maji Bonde la Wami Ruvu amesema kuwa zoezi hilo litakuwa endelevu katika maeneo yote na kwamba vijana watakaokutwa katika maeneo kama hayo watapatiwa elimu juu ya utunzaji wa mazingira na kutafutiwa shughuli mbadala. HABARI/PICHA ZOTE NA MWAJUMA RAMBO/ GLOBAL TV ONLINE