Wamiliki Wa Malori Walia Na Bei Ya Mafuta Kupanda, Waomba Serikali Iwasaidie

Dar es Salaam, 8 Septemba 2023: Chama cha Wamiliki wa Malori nchini (TAMSTOA) kimelia na kupanda kwa gharama za mafuta na kuomba serikali iingilie kati na kuangalia wapi Tanzania Bara tunakwama kwakuwa Zanzibar bei ina unafuu ukilinganisha na bara.
Akizungumza kwenye mkutano na wanahabari, Mwenyekiti wa TAMSTOA, Chuki Shabani ameiomba serikali kuingilia kati suala hilo kwakuwa kitendo hicho kinaweza kusababisha waendesha malori kujazia mafuta ya kutosha nchi jirani ambapo bei zao ni nafuu na kuikosesha serikali mapato jambo ambalo si la kiungwana.
Chuki ameishauri serikali kuangalia upya mfumo wa uagizaji mafuta na mifumo ya kodi zinazotozwa.
Ameendelea kusema kuwa japo kuwa watu wanaona imeongezeka pesa ndogo kama shingi mia tatu lakini kwakuwa wao wananunua mafuta mengi haswa kwenye safari zao za masafa marefu kama vile kutoka hapa nchini mpaka Zambia na kurudi unatumia zaidi ya lita 2000 ambapo kwa ongezeko la 300 ni zaidi ya laki sita.
“Hiyo laki sita ni ongezeko la bei ya mafuta ya lori moja sasa unakuta mtu ana malori mia moja yote yanasafiri je unafikiri ni pesa ndogo hiyo?”
Kwa hesabu za haraka mwenye malori mia kwa safari moja atakumbana na ongezeko la shilingi milioni sitini.
“Hivyo chondechonde tunaiomba serikali yetu itusaidie kwa kuliangalia vizuri suala hili”. Alimaliza kusema Chuki aliwawakilisha wamiliki wa malori hapa nchini.