The House of Favourite Newspapers

Wanachama 113 Wajitokeza Kuwania Uenyekiti UVCCM

0
Viongozi wa Umoja wa Vijana wa CCM (UVCCM).

Wanachama wa Umoja wa Vijana wa CCM (UVCCM) 113 kutoka bara na visiwani wamejitokeza kuwania nafasi ya uenyekiti Taifa katika uchaguzi utakaofanyika mwaka huu, idadi ambayo haijawahi kutokea tangu kuanzishwa kwa umoja huo.

Kwa sasa nafasi hiyo inashikiliwa na Mbunge wa Donge Visiwani Zanzibar, Sadifa Juma Khamis ambaye alichaguliwa katika uchaguzi uliofanyika mwaka 2012.

Akizungumza leo Kaimu Katibu Mkuu wa Umoja huo, Shaka Hamidu amesemma wajumbe wa Kamati ya Utekelezaji ya Baraza Kuu la UVCCM linafanya usahili wagombea waliomba nafasi mbalimbali za uongozi.

Amesema usahili huo unafanyika kwa waliomba kugombea wa nafasi za mwenyekiti, makamu, wajumbe watano wa halmashauri kuu ya Taifa (NEC), wajumbe watano wa baraza kuu la umoja huo Taifa na wajumbe wa kuwakilisha jumuiya hiyo katika jumuiya nyingine za chama.

Amesema zoezi hilo ambalo limeanza tangu Aprili limefanikisha kupatikana kwa viongozi mbalimbali wa ngazi za shina hadi wilaya na kwamba kinachofanyika hivi sasa ni mchakato wa kuwapata wagombea wa nafasi za kitaifa.

“Vijana 113 wamejitokeza kuomba nafasi ya uenyekiti. Huu utakuwa ni uchaguzi wa kihistoria kati ya chaguzi zote zilizowahi kufanyika tangu mwaka 1978 ilipoanzishwa jumuiya hii mwaka huu. Kwa maneno mengine tumevunja rikodi,”amesema.

Amesema kwa upande wa nafasi ya umakamu mwenyekiti waliomba kugombea ni 23 wakati ujumbe wa Nec 118 wanachuana kugombea nafasi tano zilizopo kikatiba.

Shaka amesema jumla ya wagombea ambao wanawafanyiwa usahili katika kikao cha Kamati ya Utekelezaji wa baraza la Kuu la UVCCM ni 375 huku nafasi ya uenyekiti Taifa ikiongoza kwa waombaji wengi katika zoezi hilo.

Kwa mujibu wa Shaka, Kamati ya utekelezaji ni kikao cha awali ambacho kitatoa mapendekezo kwa Baraza Kuu la Taifa la umoja huu ambalo litakutana kesho kutwa kutwa (Oktoba 17) kwa ajili ya kupokea mapendekezo ya kamati hiyo.

“Baraza Kuu litakutana hapa hapa Dodoma kwa ajili ya kupokea na kupendekeza nafasi zilizoombwa katika mikoa na Taifa. Sisi (Baraza Kuu la umoja huo) tunapendekeza kwa Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya Taifa,”amesema .

Kwa mujibu wa utaratibu CCM kikao kitakachowachuja wagombea wa nafasi zote ambazo zinauwakilishi wa chama taifa ni Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM inayoongozwa na Mwenyekiti wake wa Taifa Dk John Magufuli.

Akizungumzia kuhusu chaguzi zilizopita za mashina hadi wilaya, Shaka alisema kuwa mambo yamekwenda vizuri katika chaguzi zote.

Alijitapa kuwa chama chao siku zote kimekuwa kikisimamia haki na usawa ili vijana waweze kupata fursa kwa nafasi wanazoziomba katika chaguzi mbalimbali nchini.

“Katika ngazi wilaya kuna changamoto mbalimbali kwenye uchaguzi ambazo zimejitokeza lakini jumuiya hii inaongozwa na kanuni na katiba ya chama chetu kwa hiyo tumeagiza viongozi wetu kuhakikisha kuwa wanashughulikia malalamiko yaliyojitokeza,”amesema

Amesema malalamiko yaliyojitokeza katika chaguzi hizo ni pamoja na hofu kuwa kuna wagombea wamezidisha umri na dhana ya kutumia rushwa.

Hata hivyo, alisema chama hicho kimekuwa kikikemea vitendo vya rushwa na hivyo itakapodhibitiki uvunjaji wa kanuni watachukua hatua zinazopaswa kuchukuliwa.

“Hatutadharau malalamiko yoyote yake, yote yatashughulikiwa na atakeyabainika kuvunja kanuni hatua zitachukuliwa,”amesema

Leave A Reply