The House of Favourite Newspapers

Wanachama wa Yanga Wajifunze Kutii Mamlaka za Soka

Mashabiki wa Yanga.

MAMLAKA zinazosimamia michezo Tanzania zimesisitiza kwamba sasa imetosha Yanga ifanye uchaguzi kujaza nafasi zilizoachwa wazi. Tayari uchaguzi umetangazwa kufanyika Januari 13 na nafasi zitakazowaniwa ni Mwenyekiti, Makamu panoja na wajumbe waliojiuzulu. Fomu zilitolewa kwenye ofisi za Shirikisho na wanachama kadhaa wakajitokeza na kupitishwa kwa mujibu wa kanuni za kamati ya uchaguzi ya TFF.

 

Lakini wakati hilo likiendelea kumekuwa na malumbano ya hapa na pale baina ya wanachama wa Yanga wenyewe kwa wenyewe na mengine dhidi ya mamlaka za soka na kufikia hatua ya kuitisha mkutano wa dharura ambao hatahivyo,polisi waliuzuia jana.

Kikosi cha timu ya Yanga.

Wanachama hao wanadai kwamba bado wanamtambua Yusuf Manji kama Mwenyekiti wao na hawataki kujaza nafasi yake kama TFF na mamlaka nyingine zinavyoamuru. Lakini vilevile baadhi yao wamekuwa wakiwaona wale waliokwenda TFF kuchukua fomu za kugombea ni kama wanakiuka masharti ya Yanga.

 

Lakini mwisho wa siku lazima Yanga kuanzia wanachama mpaka viongozi wajifunze kufuata taratibu na sheria zilizopo bila kujali wao ni wakongwe kiasi gani. Huwezi kufanikiwa kwenye jambo lolote bila kufuata utaratibu hata
kama wewe ni maarufu au unapendwa kiasi gani. TFF na mamlaka zingine zimeangalia kwamba Yanga pana tatizo na ndio maana wakaamuru nafasi zilizoko wazi zijazwe.

 

Wameona kwamba kuna mambo mengi ambayo yanashindwa kufanyika kutokana na kutokuwepo kwenye mamlaka na utendaji wa kila siku kwa mtu kama Mwenyekiti, Makamu wake na wajumbe.

 

Lazima klabu zetu zikubali kufuata utaratibu na kuweka ushabiki au mapenzi pembeni. Huwezi kufanya mambo ya maana bila ya kuwa na uongozi imara kwenye klabu husika na ukikosa uongozi thabiti au viongozi wanaojielewa ndio mwisho wa siku timu inaishia kufanya vibaya au kubeba misalaba mikubwa ya madeni kama inayowakabili Yanga kwasasa.

 

Yanga imekuwa na migomo ya hapa na pale kwa wachezaji lakini ukija kuangalia utaona kwamba tatizo ni kutokuwa na uongozi imara na unaoeleweka huku wakiamini kwamba hakuna mtu sahihi wa kuwa kwenye nafasi ya mwenyekiti zaidi ya Manji. TFF inapaswa kuwasaidia Yanga kwa kutumia busara kukutana na pande zote kuwaelewesha umuhimu wa kuwa na viongozi wanaoeleweka na kutoa nafasi kwa watu wengine.

 

Wanachama wa Yanga lazima wafundishwe kuacha kukariri majina ya watu,waangalie viongozi sahihi na klabu isonge mbele. Hakuna mdhamini yoyote anayeweza kukubali kuweka fedha yake sehemu ambako kuna mvutano au kuna sintofahamu kama Yanga.

 

Ndio maana tunashauri kwamba busara itumike zaidi kwenye ishu ya uchaguzi wa Yanga kwa wanachama kukubali kufuata utaratibu ili kuinusuru klabu na kuchochea maendeleo ambayo kwa sasa yanaonekana kukwama.

Wanachama Yanga lazima wakubali kwa moyo mmoja kwenda kwenye uchaguzi na kutoa nafasi kwa watu wengine kwavile mambo mengi yanaonekana kukwama. Yanga si ya mtu mmoja, watoe nafasi na watu wengine mambo yaende.

Comments are closed.