The House of Favourite Newspapers

Wanachokiona watoto hawa ni Mateso 100%

PWANI: FAMILIA ya Hamisi Sabiri na mkewe Zena Mari, wakazi wa Kitongoji cha Mkanzi, wilayani Mkuranga, Mkoa wa Pwani ipo katika mateso kwa asilimia 100 kufuatia watoto wao watatu waliozaliwa wakiwa wazima na baadaye kupatwa na magonjwa ya ajabu kisha kupata ulemavu wa kupooza miguu hadi kushindwa kutembea.

 

Watoto hao ambao ni Hamidu Sabri (19), Hussein Sabiri (13) na Shani Sabiri (11) wote wakiwa wamepata ulemavu wa miguu baada ya kuugua homa kali na mafua makali wakiwa watoto wadogo, hivyo walipofikia umri wa kutembea, wakashindwa kutembea.

 

Akizungumza kwa masikitiko baba mzazi wa watoto hao, Hamisi Sabiri amesema amekuwa na wakati mgumu kwa matatizo yaliyotokea kwa watoto wake kufikia hatua ya kumkosesha raha.

 

Alisema hali hiyo imewatokea watoto wake wakiwa wakubwa kwani walizaliwa wakiwa na afya njema lakini walipofikisha umri wa mwaka mmoja (miezi 12) kila mmoja akaanza kuugua kwa kupatwa na homa kali na mafua, ndipo tatizo lilipoanzia.

 

“Wanangu wote walizaliwa wakiwa wazima na baadaye wakaugua walipofikia umri wa miezi 12, tuliwakimbiza hospitali na kuambiwa wana malaria, tukapewa tiba na kuruhusiwa kurudi nyumbani, lakini wakati tunaendelea kuuguza, tukashitukia miguu inapooza na wakashindwa kutembea na kufanya chochote hatima yake wamekuwa hivyo unavyowaona,”alisema Sabiri.

 

Alisema kupooza kwao miguu kumewafanya washindwe kusimama hiyo ina maana kwamba kila kitu hukifanya hapohapo alipokaa, kama ni haja ndogo au kubwa.

Alisema wanapata mateso makubwa kwa sababu yeye akiwa ni mzazi hulazimika kuwaacha watoto hao nyumbani peke yao naye na wakeze kwenda kutafuta riziki.

 

Alisema mama yao naye huwa anaenda kutekeleza majukumu ya shamba na kulea watoto hao huku mmoja mdogo anayemlea akiwa mgongoni hivyo inakuwa ngumu kuwatimizi mahitaji yao yote tukiwa mbali na wao katika kutafuta riziki

Alisema watoto hao walitakiwa kuwa wanasoma lakini inakuwa vigumu kutokana na ulemavu walionao na umbali wa sehemu wanayoishi na shule.

 

“Tunaomba wasamaria wema kutusaidia kwani kikubwa kinachotusumbua ni kuhusiana na chakula pamoja na vifaa vya kuwasaidia wakati wa kujipatia haja ndogo na kubwa pamoja na baiskeli za magurudumu matatu.

 

“Kwa watoto watatu, kiukweli ziwezi kabisa kuwapatia mahitaji hayo kutokana na uwezo wangu kiuchumi,” alisema baba huyo na kuongeza kwamba ili wasogee kutoka sehemu moja kwenda ingine inabdi wabebwe naye na mkewe wanashindwa kutokana na kukua kwa watoto hao.

 

Naye Zena, mama mzazi wa watoto hao alisema anashangaa sana watoto wake wote kupata ulemavu baada ya kuzaliwa wakiwa wazima hali inayomfanya ajisikie mnyonge kwani kila uzazi anategemea amepata wa kumtegemea uzeeni lakini kwake sivyo.

 

Zenna amesema hali hiyo imemfanya mumewe aamue kuoa mke mwingine ambapo kwa uzazi wa mke mwenziye watoto wake wote ni wazima hakuna hata mmoj amwenye ulemavu.

Kwa yeyote aliyeguswa na habari hii na anataka kuisaidia familia hii awasiliane nao kwa namba 0788 74 81 73.

Stori: ZAINA MALOGO, RISASI MCHANGANYIKO

Comments are closed.