The House of Favourite Newspapers

Wanafunzi Sekondari/ Msingi Mvomero Wapewa Elimu ya Kujikinga na Ukatili

Julai 23, 2024 Katibu Tawala wa Wilaya ya Mvomero Bw. Said Nguya akiwa ameambatana na viongozi wa dini, maafisa Halmashauri na kutoka Tume ya Taifa ya Maadili kwa Umma na wadau wengine wametembelea shule za Diongoya na Lusanga Sekondari, Lusanga na Muungano Shule za Msingi katika muendelezo wa Kampeni ya kutoa elimu kwa wanafunzi kujiepusha na kujikinga dhidi ya vitendo vya ukatili na mmomonyoko wa maadili.
Akiwa katika Shule ya Sekondari Lusanga na Diongoya, Nguya amewataka wanafunzi hasa wa kike kuachana na matumizi ya dawa za majira kwani matumizi holela ya Dawa hizo katika Umri Mdogo kuna weza kuwaletea madhara makubwa kwa baadae ikiwemo ugumba na maradhi yasioambukiza.
Ameongeza kuwa, “mtu yeyote anayempa binti mdogo vidonge vya kujikinga na mimba, maana yake anachochea mapenzi katika umri mdogo huyo ni adau yetu namba Moja katika malezi na makuzi ya Taifa endelevu, lazima tumkemee kwani, jambo hilo ni hatari maana unaweza kujikinda na Mimba lakini ukapata magonjwa ya zinaa na mengine ni hatari kuliko mimba yenyewe.”
Katibu Tawala ametoa Rai hiyo baaada ya wanafunzi wa kike kukiri kutumia dawa hizo Ili kijikinga na mimba.
Katika hatua nyingine, Afisa kutoka Tume ya Maadili ya Viongozi wa Umma Bw. Yahaya Tumba amewasiistiza wanafunzi kuwa na maadili mema, kwani ndoto zao walizo nazo, msingi wake ni maadili yalio mema, hivyo ni vema wakawa wasikivu wa walimu wao, wazazi na walezi Ili kuyafikia malengo yao.
Diwani wa Kata ya Diongoya, Mhe Abdalah Botto amewasisitiza wanafunzi kuwafichua wale wote wanaowafanyia vitendo vya kikatili kwani, kukaaa kimya kwao kutaendeleza vitendo hivyo na kuwafanya wasiwe salama.
Aidha, Mwanafunzi wa Shule ya Sekondari Lusanga Zainab Salum Bigo, ameishushukuru Serikali kwa kuja na mpango huo wa kuelimisha wanafunzi, kwani kwa kufanya hivyo kunaweza kuokoa watoto wengi ambao wangeweza kujiingiza kwenye tabia zisizofaa kwa kutokujua madhara yake baadae.