The House of Favourite Newspapers

Wanafunzi Kidato Cha Sita St Anne Marie Academy Daraja la kwanza Kuzawadiwa Simu Janja ya iphone

0
Mkurugenzi wa shule ya St Anne Marie Academy, Dk. Jasson Rweikiza akizungumza kwenye mahafali ya 15 ya kidato cha sita yaliyofanyika shuleni hapo Mbezi Kimara kwa Msuguri jijijini Dar es Salaam.

 

WANAFUNZI wa shule ya St Anne Marie Academy watakaofiwa na wazazi wakiendelea na masomo hawatafukuzwa shule na badala yake wataendelea na masomo.

Ahadi hiyo ilitolewa mwishoni mwa wiki na Mkurugenzi wa shule za St Anne Marie Academy, Dk. Jasson Rweikiza, kwenye mahafali ya 15 ya kidato cha sita.

Alisema aliwahi kutoa ahadi hiyo na kwamba anarudia tena kwamba wanafunzi wa awali, msingi au sekondari watakaofiwa wakiwa shuleni hapo wataendelea na masomo bure.

Sehemu ya wahitimu wakiwa kwenye mahafali ya 15 ya  shule ya St Anne Marie Academy kidato cha sita yaliyofanyika shuleni hapo Mbezi Kimara kwa Msuguri jijijini Dar es Salaam.

Pia alisema wanafunzi wote watakaopata daraja la kwanza atawazawadiwa simu janja ya iphone macho matatu.

Alisema kwa namna wanafunzi hao walivyoandaliwa na kupata matokeo mazuri kwenye mitihani ya majaribio ana mayumaini kwamba asilimia kubwa watapata daraja la kwanza.

“Nimeahidi iphone macho matatu lakini kutokana na namna mlivyoandaliwa nimeanza kuwa na wasiwasi kwamba iwapo wote mtapata Division I nitapata wapi fedha za kuwanunulia iphone nyinyi wote,” alisema

Mgeni rasmi Kamishna wa Elimu Tanzania, Dk. Lyambwene Mutahabwa akimpa cheti cha kuhitimu kidato cha sita mwanafunzi wa shule hiyo ya St Anne Marie Academy ya Mbezi Kimara kwa Msuguri jijini Dar es Salaam kwenye mahafali ya 15

Alisema matokeo mazuri ya shule hiyo yanatokana na mazingira mazuri ya kusomea ikiwemo chakula kizuri, maji ya uhakika na umeme na maktaba za kisasa.

Alisema shule imeendelea kuhakikisha inakuwa na madarasa bora nay a kutosha ili darasa likae na wanafunzi wachache kumwezesha mwalimu kumiliki darasa vizuri ili wanafunzi wamwelewe.

Alisema shule hiyo ina maktaba nzuri iliyosheheni vitabu vingi vya kiada na ziada na mazingira safi ya kusomea kama viyoyozi na huduma ya afya ya uhakika kwa wanafunzi.

Alisema shule imeendelea kujiimarisha zaidi na imeweka uzio eneo lote la shule na ina askari wa kutosha wenye mafunzo na uwezo wa kutumia silaha za moto pamoja na mbwa wakali kwaajili ya ulinzi wa shule.

Wanafunzi wa kidato cha sita wa St Anne Marie Academy wakikata keki wakati wa mahafali ya 15 ya shule hiyo

Alisema kutokana na sababu za kuwepo kwa majanga ya moto  kwenye maeneo mbalimbali shule imechukua tahadhari ya kujikinga na ajali zitokanazo na moto kwa kuweka vifaa vya kuzimia moto.

Dk. Rweikiza aliiomba serikali kuwapunguzia kodi wamiliki wa shule ambao alisema wanalipa kodi 18 hali inayofanya kiwango cha ada kuwa juu hivyo kuwabebesha mzigo wazazi.

Alisema iwapo kodi hiyo ingepungua huenda ada nayo ingeshuka hivyo kuwapunguzia mzigo wazazi na kwamba kupungua kwa ada kungesababisha wanafunzi wengi kupata elimu.

“Kodi ni nyingi sana michango Manispaa Kata, kodi za moto na leseni mbalimbali tunaomba ziangaliwe kwa maana ya kumpunguzia mzigo wazazi,” alisema

Dk. Rweikiza alirudia ahadi yake kwamba hakuna mwanafunzi wa shule zake ambaye atafukuzwa shule iwapo atafiwa na wazazi akiwa anasoma kwenye shule hizo.

Wanafunzi wa St Anne Marie Academy wakionyesha umahiri wa kucheza nyimbo za Bongo fleva kwenye mahafali ya kidato cha sita

“Hii ni ahadi yangu ya muda mrefu na narudia tena mwanafunzi yeyote ambaye atafiwa na mzazi akiwa kwenye shule hizi hatafukuzwa shule, awe shule ya awali, msingi au sekondari ataendelea kusoma hadi amalize,” alisema Dk. Rweikiza.

Kwenye hotuba yake, Kamishna wa Elimu, Dk. Lyambwene Mutahabwa aliipongeza shule hiyo kwa namna ambavyo imekuwa ikifanya vizuri kwenye mitihani yake ya kitaifa.

Alimpongeza Mkurugenzi wa shule hizo, Dk. Rweikiza kwa uwekezaji mkubwa alioufanya kwenye elimu na kwamba amekuwa msaada mkubwa kwa serikali ya awamu ya sita.

Alielezea kufurahishwa na umahiri ulioonyeshwa na wanafunzi kwenye lugha ya Kiswahili na Kingereza na kuwataka walimu wa shule hiyo wasibweteke na badala yake waendelee kufundisha kwa bidii.

Leave A Reply