Watoto wa Kikwete, Nkamia na Rubeya wameng’ara katika mashindano ya Kimataifa na kuibuka na Medali za dhahabu nchini Marekani na kuiletea sifa kubwa Tanzania.
Ilikuwa katika mashindano ya wanafunzi wenye vipaji maalumu kutoka nchi mbalimbali duniani yanayotambulika kama Genius Olympiad ambayo hufanyika katika Chuo Kikuu cha Uswego nchini Marekani kila mwaka ambapo wanafunzi watatu kutoka Tanzania walijinyakulia medali za dhahabu.
Mashindano hayo husaidia kukuza uelewa wa wanafunzi katika masuala ya mazingira, sayansi, sanaa, uhandisi, ubunifu na maendeleo ya biashara.
Pia mashindano haya hutoa nafasi kwa wanafunzi wa shule za sekondari kote duniani kupata ujuzi na maarifa ya kuwa raia wema, kuwa viongozi, wanasayansi, wasanii, waandishi, wahandisi, wataalamu wa sheria kwa siku zijazo ambao watasaidia kwa kiwango kikubwa katika usimamizi wa mazingira siku zote za maisha yao.
Mwaka huu wa 2017 mashindano haya yalipokea wanafunzi 1200 kutoka mataifa 69 kote duniani ambao walishiriki katika vipengele tofauti kama sayansi, sanaa na ubunifu wa kuandika pamoja na vipengele vingine.
Tanzania iliwakilishwa na wanafunzi 22 kutoka shule ya Feza International ambapo wanafunzi watatu, Abdulrazack Juma Mkamia, Rashidi Jakaya Kikwete na Abdallah Rubeya walishinda medali za dhahabu na kuipa fahari kubwa shule hiyo na taifa kwa ujumla.
Kiongozi wa shule ya Feza Mr. Ibrahim Yunus alisema kuwa wanafunzi wa Tanzania wana vipaji vikubwa, kama wakipewa mahitaji maalumu na kuwezeshwa wanaweza kuonyesha maajabu kama vijana hao walivyofanya. Elimu haipatikani darasani tu bali wanafunzi wanahitaji fursa za aina hii kutambua vipaji vyo vilivyojificha.
Mama Salma Kikwete alifika katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere kuwapokea wanafunzi hao akiwemo mwanaye Rashidi na baada ya mapokezi hayo alipata fursa ya kuzungumza na waandishi wa habari na kusema kuwa ni fahari kubwa sana kwa taifa kupata washindi watatu wa medali za dhahabu na kuwapongeza wanafunzi hao pamoja na kuwatia moyo wanafunzi wote Tanzania kwamba wanaweza kufanya makubwa hata zaidi ya hayo.